Na Innocent Kansha – Mahakama Makete.
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania ametoa rai kwa wadau wote wa Mahakama hususani wa haki Jinai
kujipanga vizuri na kutekeleza wajibu wao wa kisheria kuwahudumia wahalifu ili
kuisaidia Mahakama kuweza kutoa haki kwa wakati na kwa wote.
Akizindua rasmi Jengo la
Mahakama ya Wilaya Makete mkoani Njombe mnamo Aprili 28, 2021 Mhe. Dkt. Feleshi
alisema kila linapoanzishwa eneo la kiutawala kwa mujibu wa sheria Mahakama ya
Wilaya inapaswa kuwepo na kutoa huduma kwa wananchi, hivyo ni wito wa Mahakama
kwa wadau wake kama vile Ofisi ya Mwendesha Mashitaka, Polisi na Magereza kuhakikisha
wanatoa ushirikiano wa hali na mali ili haki ionekane ikitendeka kwa wananchi.
“linapokuja swala la haki
jinai popote utakapopeleka huduma ni lazima Magereza, Ofisi ya Mwendesha Mashitaka
pamoja na Polisi wawe wamejipanga kuwaleta wahalifu au kuwachukua na kuwapeleka
kule ambako wanatakiwa kuhifadhiwa kwa mujibu wa taratibu”, aliongeza Jaji
Kiongozi.
Jaji Kiongozi alisema
yote hayo yatawezekana kwa kuzingatia misingi ya haki bila kushadadia na
kutoruhusu matumizi mabaya ya sheria kama vile kunyima watu dhamana kwa makosa
yanayo dhaminika au kutoa mashariti magumu ya dhamana. Lengo la Mahakama ni
kuona kwamba mtu kuwa na kesi kusiathiri shughuli zake za kiuchumi lakini vilevile
shughuli za kifamilia na mahusiano yake katika kijamii inayomzunguka.
Niwakumbushe watumishi wa
Mahakama kutunza jengo hilo zuri na la kisasa, na kuendelea kuboresha huduma
zenu kwa wateja na wadau wote watakao pata huduma hapa, pamoja na haya yote Mahakama
imeazimia kusimamia maadili ya watumishi wa Mahakama kwani ni ukweli
usiopingika kwamba mafanikio ya Taasisi hutokana na watumishi wachapakazi na wenye
maadili, alisisitiza Jaji Kiongozi.
Mhe. Dkt. Feleshi
aliwahakikishia wananchi na wadau wa Mahakama kwamba, Mahakama inao mfumo mzuri
na mathubuti wa kushughulikia kero na malalamiko kwa mfano kila Mahakama ina
rejista maalumu ya kupokelea malalamiko pia Viongozi wa Mahakama wenye dhamana
hiyo kama Mahakimu Wakazi Wafawidhi, Maafisa Utumishi na Tawala na Watendaji.
Aidha, Jaji Kiongozi alisema kwa mtu yeyote ambaye hawezi kuwasilisha lalamiko lake moja kwa moja mahakamani, Mahakama ipo wazi kupimwa na kuchunguzwa na vyombo vingine, kwahiyo Mahakama inasisitiza kwamba iwapo kuna vitendo visivyofaa vinavyofanywa na watumishi vinaweza kuwasilishwa Takukuru na kwenye Mamlaka zingine za kiuchunguzi ili vikibainika hatua zichukuliwa dhidi ya vitendo hivyo.
“Ni imani yangu
pia kuwa Wananchi na wadau wetu wa Mahakama watapata mahitaji yao ya msingi
kwenye mazingira bora kabisa wakati mashauri yao yanasikilizwa na hata pale
watakapokuwa wanasubiri kupata huduma”, alibainisha Jaji Kiongozi.
Majengo haya ya
kisasa yapo kwa sababu moja kubwa ya kuwarahisishia wananchi kupata huduma.
Tunawahakikishia kwamba tutaendelea kuwatendea haki wananchi ili maana halisi
ya umuhimu wa majengo haya ionekane kwa wananchi wetu tunaowahudumia,
alisistiza Jaji Kiongozi.
Wakati huo huo,
Mkuu wa Wilaya ya Makete Bi. Veronica Kessy alisema watumishi watao bahatika
kufanya kazi kwenye jengo hilo watakuwa wamefarijika na kufanya kazi kwa
utulivu lakini pia hata wananchi wataofika kupata huduma hapa wataamini kweli Serikali
ipo
“Serikali ya
Wilaya imefarijika sana kushiliki kwenye uzinduzi wa jengo hili na mara kwa
mara tulikuwa tunafika kuona namna ujenzi ulivyokuwa ukiendelea tukihakikisha
kwamba thamani ya jengo hili inaendena na kiwango cha pesa halisi, hii yote
ilikuwa ni kuhakikisha kwamba hakuna fedha ya serikali inayokwenda kupote kwani
ni kodi ya wananchi”, alisema Mkuu wa Wilaya.
Naye, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente alisema anapenda kumshukuru Mkuu wa Wilaya na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama, hii ni kutona na kwamba ukilinganisha Wilaya za Wanging’ombe na Njombe takwimu zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji na ubakaji ni machache sana kwa yale yanayotufikia Mahakama Kuu.
“Uwepo wa jengo
hili la kisasa sio kwamba Mahakama imejiandaa ili wananchi wengi waje washitakiwe
hapa la hasha hata kama hapatakuwepo na kesi nyingi Mahakimu wetu hawata lala
tutashirikiana na wanasheria wa halmashauri na viongozi wengine hata kutoa
elimu kwa wananchi kwani kutoa elimu ya kisheria ni moja ya kazi yetu”,
aliongeza Jaji Mfawidhi.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akikata utepe kuashiria
uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Makete mkoani Njombe Wengine ni Mkuu
wa Wilaya ya Makete Bi. Veronica Kessy (wa kwanza kushoto), Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente (wa tatu
kulia) pamoja na viongozi waandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifunua kitambaa kuashiria
uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Makete mkoani Njombe Wengine ni Mkuu
wa Wilaya ya Makete Bi. Veronica Kessy (wa kwanza kushoto).
Meza Kuu wakiwa
kwenye picha ya pamoja na makundi ya Wachungaji na watumishi wa Mahakama walishiriki hafla ya uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Makete.
Picha na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni