Na Innocent Kansha – Mahakama Wanging’ombe.
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameuhakikishia Uongozi na
Serikali ya Wilaya ya Wanging’ombe kuwa Mahakama ya Tanzania inatambua, inajali
na itaendelea kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi na wananchi bila
kujali mazingira yoyote yale na hasa kuwahudumia wananchi wenye uwezo wa chini.
Akizindua rasmi Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe Aprili 29, 2021 Mhe. Dkt. Feleshi alisema Mahakama kupitia utekelezaji wa Mpango Mkakati wake inaendelea kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kujenga majengo bora na ya kisasa maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Njombe.
"Kitendo cha mwananchi kulazimika kufuata huduma umbali mrefu kwa namna moja au nyingine ni sawa na kuinunua huduma
hiyo ambayo Serikali imeshamhakikishia kuipata kupitia Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Mahakama ya Tanzania inayo nia ya dhati ya kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi", alisisitiza.
Hata hivyo, Jaji Kiongozi alitanabaisha kuwa Mahakama haina budi kukiri kwamba utekelezaji wa mipango na mikakati ya ujenzi wa jengo hilo la Mahakama unatokana na kodi za wananchi wa Wanging’ombe na watanzania wote kwa ujumla, rasilimali fedha ambazo zinasimamiwa vizuri na Serikali.
Jaji kiongozi aliwakumbusha Viongozi na wananchi kwa ujumla wao kwamba kufungua shughuli za kimahakama katika Wilaya hiyo si kitu cha anasa au starehe bali ni hitaji muhimu la kuwafikia wananchi na kuwasogezea huduma ya utoaji haki kama matakwa ya kisheia yanavyoelekeza.
Alisema Mahakama ya Tanzania inathamini na kutambua mchango wa wananchi wote wa Tanzania wanaolipa kodi ambayo inaiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati, ikiwemo majengo ya Mahakama. Aliongeza kuwa ni matumaini ya Mahakama kwamba majengo haya yanayojengwa kwa fedha za wananchi yatatumika kutoa haki kwa kila mtanzania na kwa wakati unaostahili.
Mhe. Dkt. Feleshi akasisistiza kwamba majengo haya ya kisasa yapo kwa sababu moja kubwa ya kuwarahisishia wananchi kupata huduma. Mahakama inawahakikishia kwamba itaendelea kuwatendea haki wananchi ili maana halisi ya umuhimu wa majengo haya ionekane kwa wananchi wake inaowahudumia.
Aliwakumbusha Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo wilayani Wanging'ombe kuhakikisha wanawasaidia wananchi kupitia taasisi wanazozisimamia ili kuwezesha ustawi wa jamii.
Jaji Kiongozi alisema anatambua changamoto ya upatikanaji wa fedha kwenye maeneo mbalimbali nchini hivyo aliwashauri viongozi hao kuweka mikakati itakayowezesha kupatikana kwa gereza la mahabusu wilayani humo. "Kama Wilaya mnaweza kuanza kujenga hata kwa kutumia nguvu za wananchi na wahisani walio tayari kushirikiana nanyi kwa kupitia Mkurugezi na Mwenyekiti wa Halmashauri", alishauri.
Kuhusu matumizi ya Tehama, Mhe. Dkt. Feleshi alitoa wito kwa uongozi kupitia Mkuu wa Wilaya kuangalia uwezekanao wa kupeleka vifaa vya TEHAMA kwenye gereza la Mpechi litakalo tumiwa na Mahakama ya Wilaya ili kurahisisha usikilizwa wa mashauri ya mahabusu na wafungwa watakao kuwa wakihudumiwa na Mahakama ya Wilaya hiyo.
Alisema Mahakama ilishajipanga na
inaendelea kutumia mifumo ya TEHAMA kusikiliza mashauri na shughuli mbalimbali Mahakama. Alisema jengo hilo lilizinduliwa litatumia mifumo ya Tehama kwa kuwa tayari limeunganishwa na Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano ambao utarahisisha matumizi ya teknolojia hiyo ya kutolea
huduma.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mhe. Lauteri John Kanoni alisema ni faraja kubwa kuona wilaya yake inapata moja ya nguzo muhimu ya Serikali ya utoaji haki kwa maana ya Mhimili wa Mahakama, ambapo awali iliwalazimu wananchi kutumia gharama kubwa kwa kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya haki.
“Kuna wananchi
walilazimika kwenda umbali wa kilomita 100 hadi Njombe kufuata huduma hii kwa mashauri
ya ngazi ya Wilaya, kwa umbali huo kwenda na kurudi ni kilometa 200 hii
inaonyesha jinsi gani huyu mwananchi alitumia muda mrefu na kwa gharama kubwa
kupata haki”, alisema Mkuu wa Wilaya huyo.
Mhe. Kanoni
aliwaomba wananchi wote kuwa na amani, utulivu na furaha kwamba huduma ya
utoaji haki waliyokuwa wakiisubiri kwa muda mrefu na kuifuata Njombe sasa
itapatikana wilayani hapo.
Mkuu wa Wilaya huyo akatanabaisha sababu muhimu na za msingi za uwepo wa Mahakama hiyo na jinsi itakavyo kuwa suluhisho la changamoto ya matukio mengi ya kiuhalifu miongoni mwa jamii hii ikiwemo mauaji, ubakaji, utiaji mimba wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, wizi wa mali za aina mbalimbali usio na tija, uvunjanji, uchomaji wa nyumba, na matukio mengine mengi.
Wakati huo huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe, Penterine Kente alisema Mahakama ya Tanzania inazindua huduma za Mahakama ya wilaya wilayani Wanging'ombe kwa kuwa awali hakukuwa na Mahakama ya wilaya.
“Ni bahati kubwa kwa Wilaya iliyochanga kama hii kuanzishwa muda mfupi na kupata Mahakama yake kwa muda mfupi huo huo ni jambo la kujivunia, hivyo nawaomba wana Wanging’ombe kupunguza matukio ya kiuhalifu kwani hata Daktari hapendi kuona wodi yake imejaa wagonjwa”, alisema Jaji Kente.
Jaji Kente aliwataka wana Wanging’ombe kuachana na kasumba ya ushirikina kwa kuwa huchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa matukio ya mauaji yanayotokea eneo hilo na badala yake aliwataka wananchi hao kujikita katika kujielimisha, kuomba ushauri kwa viongozi wa dini na wa kiserikali na kujijengea utamaduni wa kusameheana na kuvumiliana panapotokea sintofahamu miongoni mwao.
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (aliyeshikilia mkasi) akikata utepe
kuashiria uzinduzi rasmi wa Jengo Mahakama ya Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe Bw. Lauteri John Kanoni (wa nne kutoka kushoto),
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa
Kente (wa pili kushoto) Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt pamoja na viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiteta jambo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Iringa Mhe. Pentelni Mlisa Kente wakati wa uzinduzi rasmi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya Wanging'ombe Wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe Bw. Lautari Kanoni (wa pili kulia), Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt (wa kwanza kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe Bi Agnetha Mpangile (wa kwanza kulia)
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akipanda Mti wa matunda kama ishara na kumbukumbu ya uzinduzi rasmi wa jengo hilo.
Meza Kuu ikiwa kwenye picha ya pamoja na makundi ya wananchi na watumishi wa Mahakama mara baada ya zoezi la uzinduzi rasmi wa jengo la mahakama ya Wilaya Wanging'ombe.
Picha na Innocent Kansha Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni