Na Rosena Suka- IJA, Lushoto
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ambaye
pia ni na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo ametoa wito
kwa Naibu Wasajili na Mahakimu kuzingatia miongozo ya utoaji adhabu na
utekelezaji wa hukumu na amri za Mahakama.
Jaji Kihwelo ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo
ya siku mbili kuhusu utekelezaji wa hukumu na amri za Mahakama kwenye mashauri ya
madai na utoaji adhabu kwenye mashauri mbalimbali ya jinai yaliyotolewa kwa
Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja
na Mahakama za wilaya wapatao 24.
“Mafunzo haya mliyoyapata yakawe na matokeo chanya
hasa kwa vile wawezeshaji wa mafunzo wamebobea katika maeneo husika na wamewapa
mbinu nyingi za utoaji wa adhabu na utekelezaji wa amri za mahakama na hukumu
mbalimbali”, alisema Mhe. Kihwelo.
Jaji Kihwelo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuwapatia
watumishi wengine wa Mahakama ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo
kile walichokipata ili kusaidia kuimarisha utendaji kazi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mtwara Mhe. Amir Msumi alisema kuwa
mafunzo waliyopatiwa ni ziada ya faida ya kuimarisha uwezo kwao ikiwa ni pamoja
na uwezo wa kufanya ukaguzi wa Mahakama za chini.
“Kama Mahakama zetu zitaimarika katika usahihi wa adhabu na ukazaji wa hukumu kwa kadri ya miongozo inavyoeleza, Imani ya wadau na Taasisi zingine itaongezeka na hivyo kujenga heshima kwa Mahakama ya Tanzania kwa upande mmoja na amani na ustawi wa nchi na wananchi kwa upande mwingine” alisema Mhe. Msumi.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) chini ya ufadhili wa Mradi wa Kujenga Uwezo Endelevu wa Kupambana na Rushwa (Building Sustainable Anti-Corruption Action in Tanzania yaani BSAAT).
Hili ni kundi la pili kushiriki mafunzo ya aina hiyo ikiwa
ni muendelezo wa mafunzo yanayotarajiwa kutolewa pia kwa Naibu Wasajili na
Mahakimu Wakazi Wafawidhi wengine. Kundi la tatu la mafunzo hayo linatarajiwa
kupatiwa mafunzo Mei 04 na 05, 2021 chuoni hapo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni