Na Innocent Kansha – Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amekutana na kuwapokea Naibu Wakuu wawili (2) wapya
kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) kwa lengo la kujitambulisha. Watumishi hao ni Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri Bw.
Goodluck Chuwa na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Fatihiya
Massawe.
Akizungumza katika tukio
hilo mapema leo Mei 12, 2021 Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam Jaji Mkuu Prof.
Juma aliwapongeza kwa kuteuliwa kwao kuwa Watumishi wa Chuo na kuwataka watumie
muda wao kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na chuo ili kumudu
majukumu yao ya kitaasisi, katika kuboresha na kuimarisha huduma za utoaji haki. Mahakama inasisitiza matumizi ya mifumo ya kiteknolojia ili kutoa haki kwa haraka na uwazi zaidi.
“Matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni miongoni mwa shabaha ya Mahakama ya
Tanzania katika kuboresha utendaji kazi na kuleta mapinduzi makubwa katika
mfumo wa utoaji haki nchini ili tuondokane na matumizi ya karatasi na hii ndiyo
dhana halisi ya Mapinduzi ya nne (4) ya Viwanda inavyojitanabaisha”, aliongeza Jaji
Mkuu.
Aidha, Jaji Mkuu
aliwakaribisha na kuwaahidi kutoa ushirikiano wa kitaasisi katika kutekeleza
majukumu yao.
Awali katika utambulisho
huo, Watumishi hao waliambatana na mwenyeji wao ambaye ni Mkuu wa Chuo hicho, na Jaji mteule wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo kwa lengo la
kujitambulisha kama watumishi wapya kwa ngazi za Unaibu Mkuu wa Chuo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye tai nyekundu) akiwa kwenye picha ya pamoja na Naibu Wakuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto (IJA) waliofika Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujitambulisha kama watumishi wapya wa Chuo hicho mapema leo Mei 12, 2021, wengine ni Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (mwenye suti nyeusi), kulia ni Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri Bw. Goodluck Chuwa na kushoto ni Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Fatihiya Massawe.
Naibu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Huduma za Ushauri Bw. Goodluck Chuwa (kulia) na Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Dkt. Fatihiya Massawe (kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kujitambulisha kama watumishi wapya wa Chuo hicho mapema leo Mei 12, 2021, Ofisini kwa Jaji Mkuu.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni