Na Innocent Kansha – Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza Majaji wateule wa Mahakama ya Rufani
kwa kuteuliwa kwao na kuwaomba watakapo kuwa wakisiliza mashauri zingatieni kupunguza
mbinu za kiufundi ili haki ionekane ikitendeka kwa wananchi.
Akizungumza katika tukio
hilo mapema leo asubuhi Mei 17, 2021 Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam Jaji
Mkuu Prof. Juma alisema mbinu za kiufundi zinachelewesha upatikanaji wa maamuzi
ya kimahakama moja ya maeneo ya maboresho ni hilo, msisite kuwasilisha
mapendekezo na maoni yenu kwenye Kamati ya Jaji Mkuu ya Maboresho ya Sheria na
Kanuni hasa kwenye maeneo mnayoona yanahitaji kufanyiwa hivyo.
“Mmeteuliwa kutoka miongoni mwa idadi kubwa ya
Majaji waliopo Mahakama Kuu, ni matarajio yetu mtatenda kazi zenu kwa ufanisi,
uwazi na kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu mkitambua ninyi ni tegemeo la
Mahakama ya Tanzania na mtatoa huduma katika nafasi zenu kwa muda mrefu zaidi”,
alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu alisema taswira
ya utoaji haki nchini inawategemea ninyi mkiwa kama Majaji wa Mahakama ya
Rufani. Mahakama inapitia Maboresho mengi mbalimbali yakiwemo ya Sheria na
Kanuni. Aidha akifafanua alisema, mmeteuliwa kutenda haki katika ngazi ya juu
kabisa na mtatazamwa sana na kila mtu hata hivyo mtapimwa kwa kupitia maamuzi
mtakayo yatoa kila siku.
Aliongeza kuwa Taaluma ya
Sheria inapitia mageuzi makubwa kutokana na utandawazi wananchi wengi
wanauelewa mpana wa masuala ya kisheria hasa katika karne ya 21 yenye ushindani
mkubwa na inatawaliwa na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Profesa Juma alitoa angalizo
kwa Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani kwamba itawalazimu kuendelea
kujielimisha kwa mambo mengi zaidi ili kuendana na kasi hiyo, Mahakama
inategemea kujifunza mambo mengi mazuri kutoka kwao.
Naye Jaji Mteule wa
Mahakama ya Rufani, Mhe Patricia Fikirini akitoa neno kwa niaba ya Majaji
wenzake alimshukuru Jaji Mkuu kwa kuwaalika na akamuhakikishia Jaji Mkuu kwamba
wapo tayari kupokea majukumu na kutenda kazi waliyoaminiwa.
“Tunaahidi atutakuangusha
wewe Jaji Mkuu wala Mahakama ya Tanzania, sisi sote kwa pamoja tumefanya kazi
kwa muda mrefu kwa ushirikiano wa karibu, tutakupa ushirikiano uliotukuka
wakati wote wa utumishi wetu”, alisistiza Jaji huyo Mteule wa Mahakama ya
Rufani.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele ya picha ya Rais) akiwa kwenye
kikao cha pamoja na Majaji Wateule wa Mahakama ya Rufani walipomtembelea
Ofisini kwake leo Mei 17, 2021.
Baadhi ya Majaji Wateule
wa Mahakama ya Rufani wakiwa Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania walipomtembelea
na kukutana nae kwa mazungumzo wa kwanza kushoto ni Jaji Mteule wa Mahakama ya
Rufani Mhe.Lilian Leonard Mashaka, na wa pili kushoto ni Jaji Mteule wa
Mahakama ya Rufani Mhe. Patricia Saleh Fikirini, wa pili kulia ni Jaji Mteule
wa Mahakama ya Rufani Mhe Abraham Mwampashe na wa kwanza kulia ni Jaji Mteule wa
Mahakama ya Rufani Mhe. Issa John Maige.
Baadhi ya Majaji Wateule
wa Mahakama ya Rufani wakiwa Ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania walipomtembelea
na kukutana nae kwa mazungumzo wa kwanza kulia ni Jaji Mteule wa Mahakama ya
Rufani Mhe. Pentelni Mlisa Kente, katikati ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani
Mhe. Lucia Gamuya Kairo na kushoto ni Jaji Mteule wa Mahakama ya Rufani Mhe.
Dkt. Paul Kihwelo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni