Jumanne, 18 Mei 2021

TATUENI TATIZO LA UCHELEWESHAJI WA KESI MAHAKAMANI; RAIS SAMIA

Na Mary Gwera, Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewaapisha jumla ya Majaji wapya 28 huku akiwa na imani kuwa ongezeko hilo la Majaji saba (7) wa Mahakama ya Rufani na 21 wa Mahakama Kuu ya Tanzania litasaidia kupunguza tatizo la ucheleweshwaji wa kesi Mahakamani.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha rasmi Majaji hao Mei 17, 2021 jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kuwa tatizo la ucheleweshaji wa kesi Mahakamani bado lipo hivyo Majaji hao wanapaswa kuongeza nguvu katika kutatua changamoto hiyo.

“Tatizo la ucheleweshwaji wa kesi katika Mahakama zetu bado lipo, kama mnavyosema Wanasheria haki inayocheleweshwa ndio haki inayokataliwa, hivyo ni imani yangu kuwa baada ya upatikanaji wa Majaji hawa ucheleweshaji wa kesi Mahakamani utapungua na hatimaye haki kupatikana kwa wakati,” alisema Mhe. Rais Samia.

Aidha, Mhe. Rais aliviagiza vyombo vya upelelezi nchini kufanya kazi zake za upelelezi kwa wakati ili kuwezesha kesi kumalizika kwa wakati ili wananchi waweze kupata haki zao kwa muda muafaka.

Hali kadhalika, Mhe. Rais aliwataka Majaji hao wapya kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu huku wakiongozwa na utu na nafsi zao katika kutoa huduma ya utoaji haki huku akisisitiza kuwa haki ni msingi wa maendeleo katika taifa lolote.

“Jukumu lililo mbele yenu ni kubwa sana, kama inavyosema Ibara ya (107) A ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mamlaka ya utoaji haki ni Mahakama, hivyo jukumu lililopo mbele yenu ni kubwa sana, basi ni vyema mkatekeleze majukumu yenu mliyopewa kwa uaminifu, mkaongoze vyema na mkaongozwe na utu na nafsi zenu katika kuwatumikia wananchi,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, Rais Samia aliwataka Majaji Wanawake walioteuliwa ambao ni jumla ya Majaji 13 wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, kujiamini katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa amewaamini na hivyo hategemei Majaji hao kufanya vinginevyo.

Naye, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alimshukuru Mhe. Rais kwa uteuzi wa Majaji hao wapya huku akiwa na imani kuwa idadi hiyo italeta mabadiliko makubwa ambayo yataonekana mara moja.

“Mhe. Rais napenda nichukue fursa hii kukushukuru kwa kutupatia Majaji hawa, idadi hii itasaidia kupunguza mzigo wa mashauri kwa Majaji waliopo na hivyo kusaidia kuleta mabadiliko ambayo yataonekana mara moja,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu alisema kwamba ongezeko la Majaji hao utasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani huku akifafanua kuwa ongezeko la Majaji wapya saba (7) wa Mahakama Rufani utaongeza idadi ya majopo ya Mahakama  hiyo na  idadi ya Majaji wapya wa Mahakama Kuu ambao kwa sasa itakuwa 86 na hivyo kila Jaji atasikiliza jumla ya mashauri 252 kwa mwaka tofauti na ilivyokuwa awali ambapo kila Jaji alikuwa akisikiliza jumla ya mashauri 342 kwa mwaka.

“Mhe. Rais idadi ya Majaji inapanda na kupungua kulingana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kustaafu kwa Majaji pamoja na Majaji wengine kupangiwa majukumu mbalimbali, hivyo bado tunaomba kuendelea kupatiwa Majaji kadri nafasi zinapopatikana ili kuendelea kutoa huduma ya haki kwa kuwa wananchi wengi kwa sasa wanafahamu haki zao na hivyo kufungua kesi kwa wingi,” alieleza.

Akizungumzia mchakato wa upatikanaji wa Majaji hao, Mhe. Jaji Mkuu aliwatoa hofu wananchi kuwa taratibu zote stahiki za upatikanaji wa Majaji hao walioteuliwa ulifuatwa.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai amewapongeza Majaji hao huku akiahidi kuwa Bunge litaendelea kutunga sheria nzuri zinazotekelezeka.

“Mmekabidhiwa jukumu kubwa la uamuzi hapa duniani, kazi ya uamuzi ni kazi ya Mungu hivyo ni vyema kuamua sahihi kwakuwa si suala tu la kuamua kwenye karatasi bali ni uamuzi dhidi ya hatma ya maisha ya watu,” alisema.

Waheshimiwa Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania wakila kiapo cha uadilifu wa utumishi wa umma mara baada ya kuapishwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Mei 17, 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam.

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni