Ijumaa, 21 Mei 2021

UJENZI WA KITUO JUMUISHI CHA UTOAJI HAKI MOROGORO WAFIKIA ASILIMIA 76

Na Lydia Churi-Mahakama, Morogoro

 Ujenzi wa jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre-IJC) katika Mkoa wa Morogoro umefikia asilimia 76 na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Morogoro waliofanya ziara kwenye jengo hilo kwa lengo la kufahamu juu ya ujenzi ili kuuhabarisha Umma, Mhandisi wa Mahakama ya Tanzania, Fabian Kwagilwa alisema jengo hilo lilianza kujengwa Januari 2020 na linatarajiwa kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

“Jengo hili linalojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na kusimamiwa na Mahakama ya Tanzania litagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 9.1 mpaka kukamilika kwake”, alisema Mhandisi Kwagilwa.

Alisema jumla ya majengo sita ya vituo Jumuishi vya Utoaji Haki yanajengwa katika miji ya Arusha, Dodoma, Mwanza, Morogoro pamoja na wilaya za Kinondoni na Temeke jijini Dar es salaam. Alisongeza kuwa kupitia majengo haya, wananchi wataweza kufikia huduma za Mahakama kwa urahisi zaidi.

Akifafanua, Mhandisi Kwagilwa alisema usanifu wa majengo hayo umezingatia masuala muhimu ikiwemo kutengezeza miundombuinu rafiki, bora na ya kisasa kwa wafanyakazi wa Mahakama pamoja na wananchi watakaofika kwenye majengo hayo kupatiwa huduma za kimahakama.

Alisema majengo hayo yatatumia mifumo ya Tehama kwa ajili ya kurahisisha utendaji wa kazi na pia yamejengwa kwa kuzingatia ubora utakaowezesha wananchi wa rika zote kuingia kwa urahisi kwenye jengo hili na kupata huduma.  

Alisema majengo ya vituo Jumuishi vya Utoaji Haki yatahusisha ngazi zote za Mahakama pamoja na baadhi ya ofisi za wadau ndani ya Jengo moja. Ngazi hizo ni Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, pamoja na Mahakama Kuu.

Mahakama ya Tanzania kwa sasa inaboresha miundombinu yake kwa kukarabati majengo ya zamani na kujenga mengine mapya, hivi karibuni inatarajia kuanza ujenzi wa majengo 25 ya Mahakama za wilaya katika maeneo mbalimbali nchini yasiyokuwa na huduma ya Mahakama za wilaya.

Kupitia Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Miundombinu (Five Year Infrastructural Development Plan) 2016/2017-2020/2021 unaohusu ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, maeneo ya kipaumbele yaliainishwa kwa kuzingatia vigezo vya idadi ya Watu, wingi wa mashauri, maeneo mapya ya utawala, iumbali kwa wananchi kufuata huduma shughuli za kiuchumi, na mazingira ya kijiografia.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza la wafanyakaza wa Mahakama ya Tanzania leo mjini Dodoma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru alisema katika utekelezaji wa Mpango Mkakati huo, Mahakama imekamilisha ujenzi na ukarabati wa jengo la Mahakama Kuu Sumbawanga, Mbeya na Tanga, ujenzi wa Mahakama Kuu kanda za Kigoma na Musoma pamoja na ujenzi wa Mahakama za Hakimu Mkazi tano (5), Mahakama za Wilaya 17 na Mahakama za Mwanzo 18 katika maeneo mbalimbali nchini.

 

Aidha, Miradi mingine iliyokamilika ni ile ya ujenzi wa nyumba nne (4) za Makazi za Majaji Kigoma na Musoma, ukarabati wa nyumba tatu (3) za kufikia Majaji mkoani Mtwara na ujenzi ya nyumba 3 za Mahakimu katika wilaya za Ngorongoro na Bagamoyo.

“Tunaendelea na ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama mjini Dodoma, Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Lindi, Katavi na Songwe, ukarabati wa jengo la Mahakama Kuu Tabora na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, Ujenzi wa Mahakama za Wilaya Kilindi, Bunda, Rungwe, Sikonge, Same, Mwanga, Ngara, Tandahimba na Mahakama za Mwanzo Nyakibimbili (Bukoba), Kimbe (Kilindi), Chanika (DSM), Hydom (Mbulu), Kabanga (Ngara) na Matiri (Songea)” alisema.

 

Katika mwaka wa fedha 2021/22, Mahakama itaanza ujenzi wa majengo ya Mahakama za Wilaya katika wilaya za Kwimba, Manyoni na Liwale na Mahakama za Mwanzo za Ukonga na Bunju (DSM), Kinesi (Rory), Luilo (Ludewa), Usevya (Mlele) na Mahenge (Kilolo).

Jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre)-IJC linaloendelea kujengwa katika Mkoa wa Morogoro. Majengo mengine matano kama hili yanaendelea kujengwa katika miji ya Mwanza, Dodoma, Arusha, na Dar es salaam katika wilaya za Temeke na Kinondoni.

Jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre)-IJC linaloendelea kujengwa katika Mkoa wa Morogoro. Majengo mengine matano kama hili yanaendelea kujengwa katika miji ya Mwanza, Dodoma, Arusha, pamoja na Dar es salaam katika wilaya za Temeke na Kinondoni.

Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama baada ya waandishi hao kutembelea jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre)-IJC linaloendelea kujengwa katika Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kuuhabarisha Umma. Wa tisa kushoto ni Mhandisi wa Mahakama ya Tanzania, Fabian Kwagilwa na wa sita kulia ni Afisa Habari wa Mahakama, Bi. Lydia Churi. 

Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Morogoro wakijadiliana jambo na Mhandisi wa Mahakama ya Tanzania, Fabian Kwagilwa (wa tatu kushoto) walipofanya ziara kwenye Jengo la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre)-IJC linaloendelea kujengwa katika Mkoani humo. Wa pili kulia ni Afisa Habari wa Mahakama, Bi. Lydia Churi.


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni