Jumatatu, 7 Juni 2021

MAHAKIMU WA MKOA WA DODOMA WAASWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA WELEDI

Na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Angelo Rumisha amewataka Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu wa Mahakama za Mkoa wa Dodoma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, bidii na uadilifu.

Akifungua mafunzo ya ndani hivi karibuni yaliyoandaliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma yaliyohusisha Mahakimu wote wa Mkoa huo pamoja na baadhi ya Wasaidizi wa Kumbukumbu, Mhe. Dkt. alisema lengo la mafunzo hayo ni kubadilishana ujuzi, kuwajengea uwezo, kukumbushana majukumu na viwango bora vya utendaji kazi kupitia mada mbalimbali zilizoandaliwa ikiwemo, Rushwa na athari zake katika Utoaji Haki, Uendeshaji wa Masijala (Registry Management), Maadili kwa Maafisa wa Mahakama, na utoaji wa Adhabu (Setencing process).

“Hatutafanikiwa kwa kutegemea uwezo tulionao katika kutekeleza majukumu yetu tu; bali kwa namna gani tunakuwa waadilifu na wenye bidii katika kutekeleza majukumu yetu pamoja na kusimamia vyema maboresho yanayoendelea kufanywa na Mahakama ya Tanzania,” alisema Msajili huyo.

Mhe. Dkt. Rumisha aliongeza kwa kuwataka Mahakimu hao kuongeza kasi katika usikilizaji wa mashauri na kusimamia vyema utendaji kazi wa masijala zao huku wakiendana na kasi ya maboresho makubwa yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania ikiwemo matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki.

Aliendelea kubainisha kuwa, “sote tupo katika ulimwengu wa TEHAMA na tunapaswa kuendana na Teknolojia ya kisasa” huku akiwataka Mahakimu hao kuendelea kujifunza na kujiimarisha katika matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki, hii ikiwa ni pamoja na uratibu wa mashauri kwa njia ya mtandao (e-filling), matumizi ya video conference pamoja na kuimarisha mfumo wa makusanyo wa maduhuli ya Serikali kupitia mfumo wa malipo wa Serikali maarufu kama Government Electronic Payment Gateway (GePG) kwa kusimamia tozo na ada kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa Sheria.

Vilevile aliwasisitiza Washiriki hao wa Mafunzo kuhusu umuhimu wa kuzingatia matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kutoharibu hadhi ya mhimili wa Mahakama na kuaminiwa katika jamii yetu.

Naye  Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Sylivia Lushasi amewataka Mahakimu hao kuzingatia maelekezo ya Viongozi na yale yanayotolewa na Mahakama za juu kuhusu Mamlaka waliyonayo katika upokeaji na usikilizaji wa mashauri, utekelezaji wa hukumu pamoja na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu kwa mapana yake.

Sambamba na hilo, amewataka Mahakimu wote na Wasaidizi wa Kumbukumbu kuimarisha mifumo ya masijala ili kuongeza kasi katika upokeaji na ufunguaji wa mashauri, kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi kwa wakati pamoja na kuhakikisha wateja wanapatiwa nakala za maamuzi katika muda wa kimkakati uliowekwa.

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma Bw. Sosthenes Kibwengo aliipongeza Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma kwa ushirikiano ulioimarishwa baina yao na Taasisi nyingine katika Mkoa huo katika adhma ya utoaji haki na kuwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuiepuka Rushwa ili kutoichafua Mahakama. 

“Rushwa ni adui wa haki, huondoa usawa na hata kuathiri uchumi na ustawi wa Taifa husika, hivyo ni vyema kuthamini nafasi mlizokasimishwa, kuepuka tamaa mbaya na migongano ya maslahi mahala pa kazi ili kuweza kutenda haki na hatimaye wananchi kuona haki ikitendeka dhahiri,” alisema Bw. Kibwengo.

Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Angelo  Rumisha (Kushoto) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, katikati ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, Mhe. Elizabeth Nyembele na kulia ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Sylivia S. Lushasi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Mhe. Lushasi akifafanua jambo katika mafunzo hayo.
Sehemu ya Mahakimu wa Mahakama za Mkoa wa Dodoma waliohudhuria katika mafunzo hayo.
Picha ya pamoja ya Mahakimu na Wasaidizi wa Kumbukumbu waliohudhuria mafunzo hayo pamoja na Wawezeshaji; walioketi katikati ni Naibu Msajili Mfawidhi , Mhe. Dkt. Angelo Rumisha, kulia Bw. Sosthenes Kibwengo (Mkuu wa TAKUKURU (M) Dodoma na kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi (M) Mhe. Sylivia S. Lushasi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni