Na Mary Gwera, Mahakama-Mwanza
Jumla
ya mashauri 1,208 yamesikilizwa na kumalizwa na Mahakama inayotembea ‘mobile
court’ huku watu 13,668 wakiwa wamenufaika na huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo
katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari wa mkoani Mwanza Juni 17, 2021, Hakimu Mkazi ambaye pia
ni Mratibu wa Mahakama zinazotembea ‘mobile court’, Mhe. Moses Ndelwa alisema
kuwa idadi hiyo ya mashauri na wanufaika wa huduma hizo ni tangu kuanza kutolewa
rasmi kwa huduma hiyo Julai, 2019 hadi kufikia mwezi Mei, 2021.
“Mahakama
hii imeleta mafanikio katika mikoa hii miwili ambapo imesikiliza na kumaliza
jumla ya mashauri 1,208, huku Mwanza pekee mashauri 520 yalifunguliwa na kumalizika
katika kipindi hicho,” alisema Mhe. Ndelwa.
Mratibu
huyo aliongeza kuwa usikilizwaji wa Mashauri katika Mahakama inayotembea ni wa
haraka huku akieleza kuwa mashauri yote husikilizwa na kumalizika ndani ya siku
30.
Kwa
upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Mhe.
Monica Ndyekobora ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kuitumia
Mahakama hiyo kwa kuwa muitikio wa kufungua mashauri bado si mkubwa sana.
“Mahakama
inayotembea imesaidia kupunguza mlundikano wa mashauri, hivyo ni rai yangu kwa
wanawanchi wa mkoa huu kujitokeza kutumia Mahakama hii endapo wana kesi za
kufungua kwa kuwa inawapunguzia gharama wananchi, inatoa haki kwa wakati na
kadhalika” alisema Mhe. Ndyekobora.
Naye
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo-Mkuyuni ambaye pia anahudumu katika
Mahakama inayotembea, Mhe. Jenipher Nkwabi alibainisha kuwa mashauri
yanayofunguliwa kwa wingi katika Mahakama hiyo ni mashauri ya ndoa na talaka,
huku akiongeza kuwa kwa upande wa Mwanza hususani eneo la Mkolani/Buhongwa
kumekuwa na muitikio mkubwa wa wananchi kutumia Mahakama hiyo.
Mahakama
ya Tanzania iliandaa ziara maalum ambayo iliwahusisha Waandishi wa Habari wa mkoani Mwanza lengo likiwa ni kuwapa
uelewa zaidi juu ya huduma zitolewazo na Mahakama hiyo pamoja na mafanikio yake
ili waweze kuwajuza wananchi juu ya Mahakama hiyo.
Kwa
upande wa Mwanza huduma hutolewa maeneo ya Buswelu siku ya Jumatatu, Igoma-Jumanne
na Jumatano na Buhongwa huduma hutolewa Alhamis na Ijumaa.
Aidha,
kwa upande wa Dar es Salaam ambapo pia huduma hii inapatikana, Mahakama
inayotembea hutoa huduma zake maeneo ya Bunja ‘A’ Jumatatu ya kila wiki,
Kibamba siku ya Jumanne, Buza-Jumatano na Chanika-Alhamis.
Mbali
na usikilizaji wa mashauri, Mahakama inayotembea inatoa pia huduma nyingine
kama kufanya usuluhishi kwa wadaawa, kutoa elimu kuhusiana na masuala ya
kimahakama, kutoa fomu za viapo na kuthibitisha nyaraka mbalimbali pamoja na
kupokea malalamiko.
Mahakama
inayotembea ilizinduliwa rasmi Februari 06, 2019 katika sherehe za kilele cha
maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Mpango
wa Mahakama ni kuendelea kusogeza huduma hii katika maeneo mengine kadri bajeti
itakavyoruhusu.
Hakimu
Mkazi ambaye pia ni Mratibu wa Mahakama inayotembea-Tanzania, Mhe. Moses Ndelwa
(mwenye suti nyeusi) akitoa elimu kwa Waandishi wa Habari waliotembelea Mahakama
inayotembea iliyokuwa ikitoa huduma Mkolani-Mwanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni