Na Innocent Kansha, Mahakama - Lushoto
Jaji Mstaafu wa Mahakama
ya Rufani Mhe. John Mrosso amefunga rasmi mafunzo elekezi ya Majaji 24 wapya wa
Mahakama Kuu ya Tanzania na Zanziba na kuwaomba wakatende haki ili wananchi
waone kweli kuwa haki inatendeka na si vinginevyo.
Akizungumza na Majaji hao
wakati wa hafla ya kufunga mafunzo elekezi hayo yaliyoanza Mei 31, 2021 na
kuhitimishwa Juni 18, 2021. Jaji Msataafu Mhe. Mrosso alisema moyo wa kupenda
kutoa haki na kutetea maslahi ya wananchi kwa njia ya kutafsiri sheria ndilo
liwe lengo la kwanza katika kazi zenu.
“Kupitia kwenu natamani kuona
maboresho makubwa ya Chombo hiki kiwe kimbilio la watu wenye kiu ya kupata haki
na hili litawezekana kama mtakuwa mnakumbuka viapo vyenu mara kwa mara”,
alisema Jaji Mrosso.
Jaji Mrosso alisema, Jaji
kazi yako kubwa ni kutenda haki hata kama mbingu itashuka ili kuondoa dhana na
kasumba iliyojengeka miongoni mwa baadhi ya watu kuwa mahakamani kuna sheria na
pengine hakuna haki. Nendeni mkajaribu sana kuilinda na kuitetea sifa nzuri ya
Mahakama na kurudisha imani kwa wadau.
Akiongelea suala ya
Maadili kwa Majaji, Jaji Mrosso alisema wakati wa kutimiza majukumu yako epuke
kuonyesha mrengo au itikadi, epukeni kuonyesha hisia za chama chochote cha
siasa na hamtakiwi kufanya siasa mkiwa mahakamani.
“Maadili hayakuzuii Jaji
kushiriki mijadala ya nje ya tasnia yako, ondokaneni na dhana ya kujikweza
tafuteni namna bora ya kushirikiana na wadau wengine kwa namna isiyo athili viapo
vyenu”, alisisitiza Jaji Mrosso.
Jaji Mrosso aliendelea kuwakumbusha
Majaji wapya kuwa watakapo kuwa wanaamua mshauri na kutatua migogoro sheria
imewapa mamlaka ya utashi (Descretion powers) wakati wa kutoa adhabu, busara
hii itumike kwa uangalifu mkubwa bila kupoteza imani kwa wadau.
Jaji Mrosso aliwataka
Majaji hao wapya wakawatumikie wananchi wakati wote bila uoga, chuki, huba, wala
upendeleo na kumtanguliza Mungu katika majukumu yao ya kila siku ya kutafsiri
sheria na kutenda haki.
Bila shaka kwa kupitia programu
hiyo ya masomo 30 na wawezeshaji 25 Mahakama ina imani kuwa mmepikwa na mkaiva
na kwamba mpo tayari kwenda kufanya kazi yenu ya ujaji kwani vigezo vya
kuteuliwa kuwa Jaji ni tofauti na vigezo vya kupandishwa cheo, alieleza Jaji
Mrosso.
Kwa upande wake Jaji wa
Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe.
Dkt. Paul Kihwelo aliushukuru uongozi wa Mahakama kwa kuanzisha sera ya mafunzo
iliyowezesha kuratibu na kuandaa mafunzo elekezi hayo kwa Majaji wapya.
Aidha, Jaji Kihwelo
aliwapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuonyesha utulivu na usikivu wa hali
ya juu pia michango yao wakati wa kujifunza ilidhihilisha umahili mkubwa
walionao Majaji hao.
“Hakuna kazi ngumu kama
Mchekeshaji, unachekesha watu alafu watu hao wasicheke hii ni sawa na
uwezeshaji watu wanapokaa kimya utafikiria mambo mengi lakini kwa Majaji hawa hali
ilikuwa tofauti kabisa”, alisema Jaji Kihwelo.
Naye Jaji Msataafu wa
Mahakama ya Rufani aliyekuwa Mkurugezi wa Mafunzo hayo elekezi Mhe. Salum
Massatti alisema Majaji wapya wamepitia masomo 30 kati ya hayo 13 yalilenga
kuwajengea uwezo wa kazi za ujaji na masomo 17 yalikuwa ni mafunzo ya ziada
kama vile afya, maadili, itifaki, usalama wa Taifa na wa Majaji na mengine
mengi.
Jaji Massatti aliongeza
kuwa kazi ya ujaji itawataka Majaji kuendelea kujisomea muda wote, na aliwaomba
Majaji hao wakalisaidie Taifa kwa maslahi mapana kwa ustawi wa wananchi.
Jaji Msataafu wa Mahakama
ya Rufani ya Tanzania Mhe. John Mrosso akiwa anazungumza na Majaji wapya (hawapo pichani)
Jaji Msataafu wa Mahakama
ya Rufani ya Tanzania na ambaye alikuwa Mkurugenzi wa mafunzo elekezi ya Majaji wapya Mhe. Salum Massatti akielezea namna mafunzo hayo yalivyowajengea uwezo washiriki (hawapo pichani) wakati wa hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo elekezi.
Jaji wa Mahakama ya
Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul
Kihwelo akiushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuanzisha sera ya mafunzo
iliyowezesha kuratibu na kuandaa mafunzo elekezi hayo kwa Majaji wapya.
Baadhi ya Majaji wapya wakifuatilia mazungumzo ya kuwajengea uwezo kutoka kwa mgeni rasmi
Meza Kuu wakiwa kwenye
picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi (Majaji wapya) mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.
Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo elekezi (Majaji wapya) mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.
Meza Kuu wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Chama cha Mahakimu na Majaji wanawake Tanzania (TAWJA) na pia wakiwa washiriki wa mafunzo elekezi (Majaji wapya) mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo.
Picha na Innocent Kansha na Ibrahim Mdachi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni