Jumatatu, 21 Juni 2021

JAJI KIHWELO: KUBORESHA USHIRIKISHWAJI WA WADAU NI KUIMARISHA MISINGI YA UTOAJI HAKI

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amefungua rasmi mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama na kuwaeleza washiriki kuwa moja ya lengo la Mahakama ni kuimarisha ushirikishwaji wa wadau ili kuboresha misingi ya utoaji haki nchini.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya ufunguaji wa mafunzo hayo yatakayoendeshwa kwa kipindi kisichopungua wiki mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam mapema Juni 21, 2021 Mhe. Dkt. Kihwelo alisema, mojawapo ya maboresho yanayoendelea ndani ya Mahakama ya Tanzania hivi sasa ni kuwajengea uwezo Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama kutambua na kutekeleza majukumu hayo kwa kufuata misingi ya Mwongozo wa Kanuni za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama inayokubalika.

“Kwa muda mrefu Mahakama imekuwa ikilalamikiwa katika eneo hili kwa kufanya kazi na Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wasiokidhi vigezo na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo”, alisema Mhe. Dkt. Kihwelo

Jaji Kihwelo aliongeza kuwa ili waweze kutambua majukumu hayo watapitishwa katika masomo mbalimbali ikiwemo Kanuni zinazosimamia nidhamu, malipo na uteuzi wa Wasambaza nyaraka na Madalali wa Mahakama ili kujenga uelewa wa pamoja katika kutekeleza majukumu hayo.

Mkuu huyo wa Chuo aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania kupitia maboresho na Mwongozo wa Madalali na wasambaza nyaraka za Mahakama imeifanya kazi hii kuwa  ya kitaaluma na kuwa kila mshiriki atakaefaulu mafunzo hayo na kuteuliwa na mamlaka zinazohusika atakuwa ni Afisa wa Mahakama na kwa msingi huo aliwaeleza washiriki kuwa watapimwa kupitia ushiriki wao kwenye masomo na mada zitakazowasilishwa na watoa mada, mahudhurio darasani na mazoezi mtakayopewa.

“Niwaomba muongeze bidii na kujituma katika mafunzo haya ulizeni msipo elewa na wawezeshaji watawaelewesha ili muweze kuitendea haki ada yenu mliyoilipa ya ushiriki na mwishowe muweze kufauli mitihani mtakayoifanya”,aliwakumbusha washiriki Jaji Kihwelo.  

Mhe. Dkt. Kihwelo alisema lengo sio kuwapima washiriki kwa kuwakomoa bali ni kuwapima kwa kuwajengea uwezo unaokidhi vigezo vya kutekeleza majukumu yanayoendana na kazi za Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama.

Aidha aliendelea kueleza kuwa, Mahakama ya Tanzania ina uhitaji mkubwa wa Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini hadi hivi sasa kuna mikoa isiyokuwa na Maafisa hao, na lengo la kuwapatia elimu hiyo sio kushiriki mafunzo hayo kwa kutengeneza ajira tu bali pia ni kuboresha huduma za utoaji haki zitolewazo na Mahakama.

Kwa upande mwingine Jaji Kihwelo amewaomba washiriki hao kuendelea kutoa maoni ili kuwezesha kuboresha zaidi ya utoaji wa mafunzo hayo na mengine yajayo katika nyaja mbalimbali kwa kutoa wingo mpana zaidi kwa watu wengine kuvutiwa na kushiriki.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, kwa kutambua sera ya mafunzo ya Mahakama ya Tanzania Chuo kimepewa jukumu la kufanya Mafunzo na Utafiti kwa Maafisa wake wa ngazi mbalimbali pamoja na wadau wengine ikiwemo wale wanaojiandaa kufanya kazi ya udalali na kusambaza nyaraka za Mahakama, alieleza Mkuu huyo wa Chuo. 


Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo akifungua rasmi mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama (hawapo pichani) yatakayoendeshwa kwa kipindi kisichopungua wiki mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo Jijini Dar es salaam mapema Juni 21, 2021

 

Meza Kuu wakiwa kwenye Picha ya Pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yaliyofunguliwa rasmi na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Meza Kuu wakiwa kwenye Picha ya Pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yaliyofunguliwa rasmi na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.


Meza Kuu wakiwa kwenye Picha ya Pamoja na Secretarieti ya mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama yaliyofunguliwa rasmi na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama wakiwa darasani wakifuatilia mada mara baada ya mafunzo hayo kufunguliwa rasmi na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Mmojawapo wa washiriki wa mafunzo ya Madalali na Wasambaza Nyaraka za Mahakama akiwasilisha mada darasani mbele ya washiriki wenzake (hawapo pichani) wakati wa mafunzo hayo.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni