Na Innocent Kansha – Mahakama
Mahakama ya Wilaya ya
Temeke kwa kushirikiana na wadau kutoka katika Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na Chama cha
Wanansheria Tanganyika (TLS) wamefanikiwa kuendesha na kutoa elimu ya Haki
Mirathi Wajibu Wangu kwa Viongozi wa ngazi mbalimbali wapatao 282 wa Chama cha
Mapinduzi Manispaa ya Temeke Jijini Dar es salaam
Akifungua kampeni hiyo ya
siku moja kwa viongozi hao mnamo Julai 22, 2021 iliyofanyika katika ukumbi wa New Taifa Pub iliyoko
Manispaa ya Temeke, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe.
Suzan Kihawa aliwakumbusha wajumbe hao kuwa tatizo la mirathi limekuwa
likiisumbua jamii kutokana na changamoto ya watu wengi kutokuwa na elimu
ya kutosha ya namna ya kusimamia utaratibu mzima hasa pale inapotokea kifo.
“Tumeamua kwa dhati kwa
kushirikiana na wadau kuanzisha kampeni hii ya haki mirathi kwa Wilaya ya Temeke kwani uzoefu
unaonesha kwamba ukosefu wa elimu ya masuala ya mirathi miongoni mwa wanajamii
ni mkubwa ikilinganishwa na migogoro mingi tunayoipokea na kuitolea maamuzi
mahakamani”, alisisitiza Mhe.Kihawa.
Hakimu Mkazi Mfawidhi
huyo alisema uelewa wa mambo ya mirathi na wosia utakuwa chachu ya kuwaleta
wadau wote kwa pamoja na hatimaye kupunguza migogoro katika eneo hilo muhimu.
Jambo lolote likifanyika kwa wakati linaleta matunda yaliyokusudiwa na
likicheleweshwa linazalisha hasara.
Mhe. Kihawa aliongeza
kuwa, elimu hiyo ikipatikana kwa wakati itasaidia kutatua migogoro isiyo ya
lazima kwa jamii. Aidha watu wasipokuwa na uelewa wananchelewa kufahamu haki
zao, hivyo wanachelewa kuzitafuta na kupelekea kuchelewa kuzipata.
“Tunategemea baada ya
mafunzo haya, mkawe mbegu njema katika mashina mnayofanya kazi, kusaidia watu
kujua na kufuatilia haki zao kwa wakati hasa katika eneo la mirathi”, aliongeza
Mfawidhi huyo
Mhe. Kihawa aliongeza kuwa mashauri yakifunguliwa
kwa wakati ni wajibu wa Mahakama kuyasikiliza kwa wakati na wasimamizi wa Mirathi
watekeleze wajibu wao wa kufunga hesabu za mirathi husika kwa wakati na hivyo
kutimiza malengo ya kauli mbiu ya Haki Mirathi, Wajibu Wangu.
Naye, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Temeke, Mhe. John Ngeka aliwakumbusha wajumbe wa mafunzo hayo kuwa Mirathi ni mchakato unaojumuisha kuwasilisha ombi la kuteua msimamizi wa mirathi mahakamani, uteuzi wa msimamizi wa mirathi ambaye atakuwa na majukumu ya kukusanya mali za marehemu, kulipa madeni kama yapo pia kulipwa madeni kama itathibitika marehemu alikuwa akidai na hatimaye kugawanya mali za marehemu kwa warithi.
Mhe. Ngeka aliongeza kuwa
Sheria zinazosimamia mirathi hapa nchini (sheria ya Serikali, sheria ya Mila na
sheria ya Kiislamu) zinatamka kuwa mtu yoyote ili mradi asiwe chini ya miaka 18,
mwenye uaminifu na uadilifu anafaa kuwa msimamizi wa mirathi bila kujali kuwa
ni ndugu wa marehemu au la.
Mhe. Ngeka aliendelea
kusema, kwa utaratibu uliopo baraza la ukoo ndio huteua msimamizi wa mirathi
ambaye baadae anathibitishwa na Mahakama, lakini iwapo baraza la ukoo
likashindwa kumteua msimamizi kwa kushindwa kuafikiana katika kikao basi mtu
yoyote anaweza kwenda mahakamani kuomba kuteuliwa na Mahakama kuwa msimamizi wa
mirathi husika.
Wakati huo huo, Afisa
Usajili kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Joseph
Mwakatobe aliwaasa washiriki kuwa migogoro mingi inayoigumbika mirathi mingi kwenye
jamii ni kutokana na marehemu kuacha mali na njia bora ya kuondokana migogoro
huyo ni kuandika Wosia wenye kukidhi vigezo vyote usioweza kupingika hata mahakamani.
“Usipoandika wosia
unajiondolea au kupoteza nguvu na mamlaka ya kisheria ya mali zako zote
ulizochuma ili zisaidie familia yako, wosia utasaidia kutofuja mali za marehemu
na hivyo warithi kunufaika bila kuingia kwenye mgogoro wa aina yoyote”,
alifafanua Bw. Mwakatobe.
Moja ya mshiriki wa mafunzo ya Haki Mirathi Wajibu Wangu akiuliza swali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni