Jumatatu, 26 Julai 2021

MSUMBIJI YAAHIDI KUTOA USHIRIKIANO KWA MAHAKAMA YA TANZANIA

Na Mary Gwera, Mahakama

Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Bw. Ricardo Mtumbuida ameahidi kutoa ushirikiano kwa Mahakama ya Tanzania katika masuala mbalimbali ambayo Mahakama itahitaji ushiriki wake ili kuchangia katika maboresho ya Mahakama nchini.

Akizungumza na Mhe. Jaji Mkuu mapema leo Julai 26, 2021 pindi alipomtembelea ofisini kwake Mahakama ya Rufani (T) jijini Dar es Salaam, Balozi Mtumbuida alimueleza Mhe. Jaji Mkuu kuwa, lengo la kumtembelea ni pamoja na kujitambulisha na kumuhakikishia ushirikiano wakati wowote.

“Mhe. Jaji Mkuu nimefurahi kukutana na wewe leo, hivyo naomba nikuhakikishie ushirikiano wangu wakati wowote utakaponihitaji,” alisema Balozi Mtumbuida.

Naye, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alionyesha kufurahishwa na ujio wa Balozi huyo, ambapo nae alimuhakikishia kumpa ushirikiano katika shughuli mbalimbali kwa ustawi wa Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Msumbiji.

Sambamba na hilo, Mhe. Jaji Mkuu alimueleza Balozi huyo juu ya masuala mbalimbali  yanayohusu Mahakama ikiwa ni pamoja na maendeleo ya matumizi ya TEHAMA Mahakamani, mfumo wa Mahakama ya Tanzania na mengineyo.

“Mahakama ya Tanzania imepiga hatua katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kurahisisha utoaji wa huduma zake kwa kutumia TEHAMA, mfano katika kipindi hiki cha Ugonjwa wa Korona, baadhi ya Mashauri yamekuwa yakiendelea kusikilizwa kwa njia ya Mahakama mtandao ‘Virtual court’ kwa hiyo hii imerahisisha,” alisema Mhe. Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akimsikiliza Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Bw. Ricardo Mtumbuida wakati alipotembelewa na Balozi huyo mapema leo Julai 26, 2021.

Mhe. Jaji Mkuu akizungumza jambo na Balozi Mtumbuida (hayupo pichani).

Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Bw. Ricardo Mtumbuida akizungumza jambo na Mhe. Jaji Mkuu pindi alimpomtembelea ofisini kwake Mahakama ya Rufani, Dar es Salaam.Baadhi ya Maafisa walioambatana na Balozi huyo wakiwa pamoja na Maafisa wa Mahakama wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Jaji Mkuu na Mhe. Balozi huyo ambao wote wameahidi kushirikiana.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni