Lydia Churi na Innocent Kansha-Mahakama
Mtendaji
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Watumishi wa Mahakama
nchini kujiepusha vitendo vya rushwa ili waweze kuwatumikia wananchi kwa
uadilifu na kuhakikisha wanapata haki kwa wakati.
“Kazi
kubwa ya Mhimili huu ni kutoa haki hivyo watumishi wa Mahakama hawana budi kuvipinga
kwa nguvu zote vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili ili Mahakama iendelee
kuwa ni sehemu takatifu”, alisema Mtendaji Mkuu.
Akizungumza
na Watendaji wote wa Mahakama (Court Administrators) walioko katika mikoa mbalimbali nchini kwa kutumia
teknolojia ya Mahakama mtandao maarufu kama ‘Virtual Court’, Prof. Ole Gabriel pia
aliwataka Watendaji hao kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na kuzingatia
maadili.
Aidha
aliwataka watendaji wote kuongeza kasi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari
na Mawasilianao (TEHAMA) na kuwahimiza watumishi kujielimisha zaidi juu ya
matumizi hayo kwa kuwa sasa Mahakama inaelekea kuachana na matumizi ya karatasi
katika shughuli zake za kiutendaji.
Alisema
matumizi ya Tehama mahakamani yatarahisisha utendaji kazi wa hasa kupunguza
idadi ya mashauri pamoja na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi
wa kada mbalimbali ndani ya Mhimili huo. Alifafanua kuwa hivi sasa Mahakama ina
watumshi 5,835 kwa nchi nzima wakati mahitaji halisi ni watumishi 10,350.
Kuhusu
ushirikiano baina ya watumishi, Mtendaji Mkuu ametoa wito kwa viongozi pamoja
na watumishi wa aina zote kushirikiana katika kutoa huduma ili wananchi wapate
haki kwa wakati.
“Watumishi
wa Mahakama ni kama shilingi yenye pande mbili ambapo ni lazima pande zote
mbili zionekane, na ndivyo tunavyotakiwa kufanya kazi zetu kila siku za kutoa
haki na kumhudumia mwananchi”, alisisitiza Prof. Ole Gabriel
Prof. Elisante Ole
Gabriel ni Mtendaji Mkuu wa tatu wa Mahakama ya Tanzania tangu kuanzishwa kwa
nafasi hiyo ndani ya Mhimili huo kwa mujibu wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama
Namba 4 ya mwaka 2011. Mtendaji Mkuu wa Kwanza alikuwa ni Mhe. Balozi Hussein
Athuman Kattanga (Sasa Katibu Mkuu Kiongozi) ambaye alifuatiwa na Bw. Mathias
Kabunduguru aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akisisitiza jambo wakati akizungumza na Watendaji wa Mahakama (Court Administrators) akiwa ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni