Na Innocent Kansha – Mahakama, Ngara
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma awataka watumishi kujielimisha katika eneo la teknolojia ili kuendana na kasi ya mageuzi yanayotekelezwa na
Mahakama ya uboreshaji wa miundombinu na matumizi ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA).
Akizungumza wakati wa
ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Wilaya ya Ngara na
Mahakama ya Mwanzo Kabanga mkoani Kagera leo Agosti 30, 2021 Jaji Mkuu Prof.
Juma alisema Mahakama inatarajia kuachana na utaratibu wa kawaida wa kuendesha mashauri kwa njia ya karatasi ifikapo mwaka 2025.
Aliwataka watumishi kujitayarisha kufanya kazi katika mazingira yanayotegemea teknolojia kwa kuwa Mahakama tayari imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye mifumo hiyo na kuwa matumizi hayo yataifanya huduma ya
utoaji haki kuwa karibu zaidi na wanachi, kuongeza uwazi zaidi na kupunguza
malalamiko.
“Kutokana na kukua kwa
teknolojia na dunia kuingia kwenye karne ya nne ya mapinduzi ya viwanda
shughuli zetu nyingi za Mahakama zimeanza kutawaliwa na matumizi ya Tehama, siyo
lazima ukae darasani, unaweza kutumia mitandao kujielimisha, mafunzo ya namna
hii mengi hutolewa na Chuo chetu cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, kwa
kuzingatia matumizi ya teknolojia hii yatatufikisha dunia ya kwanza”,
alisisitiza Jaji Mkuu.
Kwa upande wa malalamiko,
Jaji Mkuu alisema wakati mwingine malalamiko mengi yanayotokana na wananchi kutofahamu taratibu za Mahakama za uendeshaji wa shughuli zake, lakini kwa
kutumia teknolojia hii itawafanya wananchi na wadau kujua vizuri taratibu hizo.
Jaji Mkuu alisema Mpango
Mkakati wa Mahakama wa kuboresha miundombinu hasa ya majengo ni njia mojawapo ya kurahisisha matumizi ya teknolojia ili kuwafika wananchi wengi zaidi katika
utoaji wa haki nchini.
Prof. Juma aliwapongeza watumishi hao kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi kwani kazi zao zinaonekana kupitia mifumo ya JSDS II, Usajili wa mashauri kupitia mtandao na akawataka kuongeza juhudi katika utendaji wao wa kazi bila kuchoka ili kurejesha imani ya Mahakama kwa wadau wake.
"Natambua kuwa bado tun achangamoto ya majengo karibu nchi nzima na mpaka sasa Mahakama imeshajenga takribani theluthi moja hivi ya majengo yake hivyo nawahakikishia watumishi na wadau kuwa ifikapo mwaka 2021/2022 hadi 2025/2025 Mahakama itakuwa imekamilisha miradi mingi na kutatua hiyo kero", alisema Jaji Mkuu.
Aidha, aliwakumbusha
wenyeviti wa kamati za maadili ya Maafisa wa Mahakama, kamati za usalama na
wadau wa Mahakama wa Wilaya za Ngara, Biharamulo na Muleba kufikiria uwezekano
wa kufikisha umeme kwenye maeneo yenye miundombinu ya Mahakama ili kurahisha
matumizi ya Tehama na kuondoa changamoto hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania ataendelea na ziara yake ya kikazi Agosti 31,
2021 katika Wilaya ya Bukoba Vijijini na kisha kuhitimisha kwa kukutana na
kuzungumza na watumishi wa Mahakama kanda ya Bukoba.
Baadhi ya watumishi na Viongozi waandamizi wa Mahakama waliofika kwenye jengo la Mahakama ya Wilaya Ngara kushuhudia ukaguzi uliofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo pichani).
Mtathimini kutoka Mamlaka
ya Usimamizi wa Majengo (TBA) Jackson Charles (aliyenyoosha mkono) akimpitisha kwenye michoro ya jengo la Mahakama ya Mwanzo Kabanga Wilayani ngara Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye kofia ya bluu) alipofika mahali hapo kwa shughuli za ukaguzi wa jengo hilo.
Picha na Innocent Kansha - Mahakama
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni