Na Mwandishi wetu, Mahakama
Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali maombi ya Mawakili wa Serikali
waliyoiomba Mahakama hiyo kusikiliza utetezi wa mapingamizi yaliyowasilishwa
mahakamani hapo na upande wa Serikali kwa njia ya maandishi.
Uamuzi
huo umefikiwa leo Agosti 30 mbele ya Mahakama hiyo baada ya upande wa
Mlalamikaji kushindwa kuwasilisha viapo vya ziada kama walivyotakiwa
kuwasilisha viapo hivyo mahakamani hapo tangu tarehe agosti, 2021 na badala
yake wameamua kuendelea na viapo vilivyowasilishwa awali.
Akizungumza
mbele ya Mahakama hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Bw. Hangi Chang’a ameiomba
Mahakama kuridhia ombi hilo kwa madai kuwa baada ya upande wa mlalamikaji
kushindwa kuwasilisha hoja zao za ziada, kama walivyotakiwa na Mahakama hiyo
wao walitekeleza wajibu wao wa kisheria kwa kuwasilisha mapingamizi manne kwa
lengo la kupinga hoja za upande wa mlalamikaji.
Mapingamizi
yaliyowasilishwa leo yanalenga kuiomba Mahakama hiyo kuliondoa Shauri hilo
Mahakamani kwa kuzingatia kuwa taratibu zilizotumika kufungua na kuwasilisha
shauri hilo la kikatiba zilikiuka taratibu za kisheria.
Mlalamikaji
katika shauri hilo analalamikia utaratibu uliotumika kumkamata na kumfikisha
Mahakamani katika shauri analotuhumiwa kufadhili vitendo vya kigaidi kuwa
ulikiuka na kuvunja haki zake za kikatiba.
Baada
ya kusikiliza maelezo kutoka pande zote mbili Jaji anayesikiliza shauri hilo
Mhe. John Mgetta ameutaka upande wa serikali kuwasilisha hoja zake kwa
maandishi ifikapo tarehe 6 Septemba huku upande wa mlalamikaji ukitakiwa kujibu
hoja hizo tarehe 09 Septemba na kama kutakuwa na hoja za kujibu kutoka upande
wa serikali basi wawasilishe hoja hizo tarehe 13 Septemba mwaka 2021.
Mhe.
Jaji. Mgetta ameahirisha Shauri hilo mpaka tarehe 23 septemba saa 8:00 mchana
litakapotajwa tena Mahakamani hapo huku akueleza kuwa hakutakuwa na sababu Mhe. Mbowe kuhudhuria Mahakamani hapo na
badala yake atawakilishwa na wakili wake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni