Na Mary Gwera, Mahakama
Mahakama
ya Tanzania imejipanga kuanza rasmi matumizi ya Ofisi Mtandao (E-Office) kesho Septemba
01, 2021 lengo likiwa ni kurahisisha utendaji kazi na kuhakikisha kuwa ndoto ya
kuwa Mahakama Mtandao (e-Judiciary) inatimia.
Katika kikao chake cha kwanza na Menejimenti ya Mahakama kilichofanyika Agosti 23, 2021, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliwaeleza masuala kadhaa wajumbe hao huku akiweka bayana dhamira yake kuhusu matumizi ya TEHAMA mahakamani ambapo alielekeza kuwa ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, mfumo wa Ofisi mtandao ‘e-office’ uanze kufanya kazi.
Akizungumza
katika mahojiano maalum leo Agosti 31 yaliyolenga katika kufahamu hatua
zilizofikiwa katika maandalizi ya kuanza kwa Ofisi mtandao, Kaimu Mkurugenzi wa
Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Agnes Bulyota amebainisha
kuwa hatua za maandalizi zinakwenda vizuri na kesho Septemba 01, 2021 Mahakama
itaanza kutumia mfumo huo katika ngazi ya Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya
Rufani pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.
“Mahakama
inaendelea na maboresho ya ufanyaji kazi katika nyanja mbalimbali, mojawapo ikiwemo
kuongeza kasi katika utoaji maamuzi mbalimbali ya kikazi, kwa kutambua hili
Mahakama tumeamua kuungana na baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali zaidi ya
100 ambazo tayari zimeshaanza matumizi ya Ofisi Mtandao (e-office),” alisema Bi.
Agnes.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa, mpango wa Mahakama ni kuhakikisha kuwa mfumo huu unatumika
katika ngazi zote za Mahakama nchini, ambapo ameeleza kuwa kwa upande wa
Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu wataanza mafunzo ya Ofisi mtandao Septemba 02 mwaka huu ili
kujiweka tayari kwa ajili ya kuanza matumizi ya mfumo huo.
“Zoezi
hili litakuwa likifanyika kwa awamu ili kuhakikisha kuwa Mahakama nzima inatumia
mfumo huu, vilevile mafunzo tajwa yamepangwa kutolewa pia kwa Watumishi wa
Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nchini (IJCs) ili nao waweze kutumia mfumo huu
katika majengo hayo mapya ya Mahakama,” alieleza.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo anaainisha faida za matumizi ya mfumo huo ikiwa ni
pamoja na kurahisisha utendaji kazi kwa kutumia TEHAMA kwa kuwa taarifa zote muhimu za kufanyia kazi zinawekwa kiielektroniki, kuongeza ufanisi wa kazi,
kuongeza kasi ya kufanya maamuzi kwa wakati, kupunguza matumizi ya karatasi, kudhibiti
matumizi mabaya ya taarifa za kiofisi na kadhalika.
Mbali
na mfumo huu, Mahakama ina mifumo ya TEHAMA kadhaa ikiwemo Mfumo wa Kusajili na
kuratibu mashauri kwa njia ya Kieletroniki (JSDS), ‘TAMs’ na mingineyo yote ikilenga
katika kumrahisishia mwananchi kupata huduma ya haki kwa wakati.
Mfumo
huu wa Ofisi Mtandao ‘e-office’ umesainifiwa na mamlaka ya Serikali Mtandao
(e-GA) kwa kushirikiana na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa (RAMD) ambao
wanasimamia taratibu na mifumo ya Masjala nchini.
HATUA NZURI
JibuFuta