Jumanne, 31 Agosti 2021

MAHAKAMA YA TANZANIA KUANZA MATUMIZI YA MFUMO WA OFISI MTANDAO SEPTEMBA MOSI

Na Mary Gwera, Mahakama

Mahakama ya Tanzania imejipanga kuanza rasmi matumizi ya Ofisi Mtandao (E-Office) kesho Septemba 01, 2021 lengo likiwa ni kurahisisha utendaji kazi na kuhakikisha kuwa ndoto ya kuwa Mahakama Mtandao (e-Judiciary) inatimia.

Katika kikao chake cha kwanza na Menejimenti ya Mahakama kilichofanyika Agosti 23, 2021, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliwaeleza masuala kadhaa wajumbe hao huku akiweka bayana dhamira yake kuhusu matumizi ya TEHAMA mahakamani ambapo alielekeza kuwa ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, mfumo wa Ofisi mtandao ‘e-office’ uanze kufanya kazi.

Akizungumza katika mahojiano maalum leo Agosti 31 yaliyolenga katika kufahamu hatua zilizofikiwa katika maandalizi ya kuanza kwa Ofisi mtandao, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Agnes Bulyota amebainisha kuwa hatua za maandalizi zinakwenda vizuri na kesho Septemba 01, 2021 Mahakama itaanza kutumia mfumo huo katika ngazi ya Makao Makuu ya Mahakama, Mahakama ya Rufani pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni.

“Mahakama inaendelea na maboresho ya ufanyaji kazi katika nyanja mbalimbali, mojawapo ikiwemo kuongeza kasi katika utoaji maamuzi mbalimbali ya kikazi, kwa kutambua hili Mahakama tumeamua kuungana na baadhi ya Wizara na Taasisi za Serikali zaidi ya 100 ambazo tayari zimeshaanza matumizi ya Ofisi Mtandao (e-office),” alisema Bi. Agnes.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa, mpango wa Mahakama ni kuhakikisha kuwa mfumo huu unatumika katika ngazi zote za Mahakama nchini, ambapo ameeleza kuwa kwa upande wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wataanza mafunzo ya Ofisi mtandao Septemba 02 mwaka huu ili kujiweka tayari kwa ajili ya kuanza matumizi ya mfumo huo.

“Zoezi hili litakuwa likifanyika kwa awamu ili kuhakikisha kuwa Mahakama nzima inatumia mfumo huu, vilevile mafunzo tajwa yamepangwa kutolewa pia kwa Watumishi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nchini (IJCs) ili nao waweze kutumia mfumo huu katika majengo hayo mapya ya Mahakama,” alieleza.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo anaainisha faida za matumizi ya mfumo huo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utendaji kazi kwa kutumia TEHAMA kwa kuwa taarifa zote muhimu za kufanyia kazi zinawekwa kiielektroniki, kuongeza ufanisi wa kazi, kuongeza kasi ya kufanya maamuzi kwa wakati, kupunguza matumizi ya karatasi, kudhibiti matumizi mabaya ya taarifa za kiofisi na kadhalika.

Mbali na mfumo huu, Mahakama ina mifumo ya TEHAMA kadhaa ikiwemo Mfumo wa Kusajili na kuratibu mashauri kwa njia ya Kieletroniki (JSDS), ‘TAMs’ na mingineyo yote ikilenga katika kumrahisishia mwananchi kupata huduma ya haki kwa wakati.

Mfumo huu wa Ofisi Mtandao ‘e-office’ umesainifiwa na mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Idara ya Nyaraka na Kumbukumbu za Taifa (RAMD) ambao wanasimamia taratibu na mifumo ya Masjala nchini.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama) akifafanua jambo. Miongoni mwa vitu anavyosisitiza kufanyika ni pamoja na matumizi ya TEHAMA Mahakamani.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Agnes Bulyota akieleza hatua iliyofikiwa kuelekea kuanza rasmi kwa matumizi ya huduma ya ofisi mtandao 'e-office' inayotarajiwa kuanza rasmi kesho Septemba 01, 2021.


 

Maoni 1 :