Jumatano, 1 Septemba 2021

WATANZANIA WATAKIWA KUBADILI FIKRA KUHUSU UTENDAJI KAZI WA MAHAKAMA

Na Lydia Churi-Mahakama

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Watanzania kubadilisha fikra zao kuhusu utendaji kazi wa Mahakama kwa kuwa Mhimili huo sasa umeingia katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha shughuli za utoaji haki nchini.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa jengo la makao makuu ya Mahakama na Kituo Jumuishi cha utoaji haki yanayoendelea kujengwa jijini Dodoma, Mtendaji Mkuu amesema Mahakama ya sasa imepiga hatua kubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa majengo bora na ya kisasa pamoja na matumizi ya TEHAMA yanayosaidia kurahisisha kazi na kuongeza uwazi kwenye shughuli za utoaji haki.

“Wananchi wanapaswa kubadili fikra walizonazo kuhusu Mhimili wa Mahakama na kufahamu kuanzia sasa kuwa wanaweza kufungua mashauri hata wakiwa majumbani kwao, Mahakama ya sasa inatumia mifumo ya Tehama katika uendeshaji wa shughuli zake”, alisema Prof. Ole Gabriel.

Aidha, Mtendaji Mkuu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa wakati na kusisitiza Mhimili huo kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya Watumishi wa Mahakama.

Naye Kaimu Mkuu wa kitengo cha Usimamizi wa Maboresho ya Mahakama (Judiciary Delivery Unit) Dkt. Angelo Rumisha alisema majengo hayo yamewekewa mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi ikiwemo kumwezesha mwananchi kufungua shauri kwa njia ya mtandao na kuweza kufuatilia kuanzia shauri linapofunguliwa mpaka linapomalizika.

“Katika vituo Jumuishi vya utoaji haki vinavyotarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni, tumeweka vigezo vya kupima utendaji kazi kwa Majaji na Mahakimu  tofauti na Mahakama nyingine, ambapo Mahakama za Mwanzo tumepunguza muda wa kusikiliza shauri kutoka miezi sita hadi siku 30, kwa Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi kutoka miezi 12 hadi siku 45 na Mahakama Kuu kutoka miezi 24 hadi miezi sita”, alisema Dkt. Rumisha.

Naye Msanifu Majengo kutoka Kampuni ya Arques Africa inayoshauri, kusanifu na kusimamia ujenzi wa jengo la makao Makuu ya Mahakama, Rosemary Nestory amesema kuwa jengo hilo limezingatia mahitaji ya watu wenye mahitaji maalum kwa kuwawekea ngazi maalum zitakazowawezesha kufikia huduma ndani ya jengo pamoja na pia huduma nyingine muhimu kwao zimezingatiwa. Alisema pia jengo hilo litakuwa na mfumo wa umeme wa jua utakaosaidia kupunguza gharama uendeshaji.   

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania anaendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama ambapo tayari amekagua ujenzi wa jingo la makao makuu ya Mahakama, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini Dodoma na jingo la Mahakama ya wilaya ya Bahi na Mahakama ya Mwanzo Bahi.

Mahakama ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa majengo manne ya vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika miji ya Dodoma, Arusha, Morogoro na Mwanza. Mahakama pia imekamilisha ujenzi wa kituo kidogo Jumuishi cha Utoaji haki kilichopo Kinondoni Dar es salaam pamoja na kituo maalum (One Stop Centre) kitakachoshughulikia mashauri ya Mirathi, Ndoa, Talaka na Watoto wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyenyoosha mkono) akikagua ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania linaloendelea kujengwa jijini Dodoma. 
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati mwenye nguo ya rangi ya blue) akiwa pamoja na viongozi wengine wa Mahakama kwenye eneo la ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania linaloendelea kujengwa jijini Dodoma. 
Sehemu ya jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania linaloendelea kujengwa jijini Dodoma. 
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Bw. Solanus Nyimbi (kushoto) na mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Leonard Magacha (kulia) wakiwa kwenye  eneo la ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania wakati Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania alipokagua jengo hilo. 
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Maboresho ya Mahakama Dkt. Angelo Rumisha akizungumza wakati Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea na kukagua jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma. 
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua chumba cha kutunzia kumbukumbu kwenye jengo jipya la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Jijini Dodoma. 


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza kukagua jengo jipya la kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma.


Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akikagua jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Bahi ambalo pia linajumuisha Mahakama ya Mwanzo Bahi. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa majengo, Mhandisi Khamadu Kitunzi. 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni