Na Lydia Churi-Mahakama
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante
Ole Gabriel amewataka watumishi wote wa Mahakama nchini kutobaguana na badala
yake wawasaidie Majaji na Mahakimu kuwawekea mazingira bora ya utendaji kazi ili
waweze kutekeleza jukumu lao la msingi la kutoa haki.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Dodoma leo, Mtendaji Mkuu amesema Mtumishi yeyote wa Mahakama hapaswi
kukwamisha shughuli za utoaji haki kwa namna yeyote ile ili wananchi wanaofika
mahakamani wapate haki kwa wakati.
“Haki ya Mbinguni hutolewa na Mungu lakini haki ya hapa
duniani hutolewa na Mahakama kwa maana ya Majaji na Mahakimu, hivyo tuwasaidie wenzetu
watekeleze majukumu yao ya kutoa maamuzi katika mazingira mazuri”, alisema
Prof. Ole Gabriel.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amewataka watumishi
wote wa Mahakama kutofanya dhambi ya kubaguana kazini na badala yake
washirikiane na kuheshimiana katika kazi ili Watanzania waweze kupata haki.
Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
ndani ya Mahakama, Prof. Ole Gabriel amesisitiza umuhimu wa matumizi ya Tehama
kwa kadri itakavyowezekana ili kurahisisha shughuli za utoaji haki.
“Hivi sasa idadi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania
kwa nchi nzima ni watu 5,835 wakati mahitaji ya watumishi ni watu 10,350, idadi
ambayo kubwa kwa kuwapata wote hao lakini kwa kupitia Tehama tutaweza kufanya
kazi licha ya upungufu mkubwa wa watumishi tulionao”, alifafanua Mtendaji Mkuu.
Akizungumzia suala la rushwa na ukosefu wa Maadili,
Prof. Ole Gabriel amewataka watumishi wote wa Mahakama kutojihusisha na vitendo
hivyo bali wawahudumie wananchi kwa uadilifu na kutumia lugha zenye staha.
“Tuwashughulike wale wachache wanaojihusisha na rushwa
ili wasiwaharibu walio wengi wazuri, hao tutawasafisha, sitakuwa na utani kwenye
suala linalohusu haki”, alisisitiza.
Mtendaji Mkuu amewataka viongozi wa Mahakama wa ngazi
mbalimbali kutumia vizuri fedha za Umma na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu masuala
yanayohusu maslahi ya watumishi na pia kuwajali na kuwaheshimu watumishi na hasa
wale wa ngazi za chini.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania anaendelea na ziara yake ya
kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama na kuungumza na watumishi wa
Mahakama kwa lengo la kujitambulisha. Tayari amekagua ujenzi wa jengo la makao
makuu ya Mahakama, Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini Dodoma, jengo
la Mahakama ya wilaya ya Bahi na Mahakama ya Mwanzo Bahi na kuzungumza na
Watumishi wa Kanda ya Dodoma.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakam Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alipozungumza nao.
Maafisa Utumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (mbele katikati) mara baada ya kuzungumza nao.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma mara baada ya kuzungumza nao.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Madereva Mahakama Kuu kanda ya Dodoma mara baada ya kuzungumza na watumishi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni