Na Innocent Kansha – Mahakama, Bukoba
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wote wa
Mahakama kujiandaa kuingia kwenye matumizi ya teknolojia kwa kuwa Mahakama
imewekeza zaidi kwenye eneo hilo.
Akizungumza
na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba mara baada ya
kukamilisha ziara ya ukaguzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili
inalojengwa Bukoba Vijijini 2021 Jaji Mkuu aliwaambia watumishi wa Mahakama kuwa, safari ya Mahakama
kuingia kwenye matumizi ya mtandao ni sehemu ya karne ya 21 ya mapinduzi ya nne ya viwanda na ya Taasisi nzima hivyo hakuna atakayeachwa nyuma.
“Nawahimiza
kutumia tovuti ya Mahakama ambayo ina taarifa na nyaraka nyingi zitakozowasaidia
kujielimisha ili tuweze kuendana na kasi ya utendaji wa shughuli za Mahakama
mtandao”, alisema.
Alisema
hivi karibuni zimetungwa kanuni za uendeshaji wa mashauri kwa kutumia Mahakama
mtandao hivyo watumishi hawana budi kuzisoma na kuzielewa ili waweze kutoa
maamuzi yatakayokubalika. Aliwakumbusha watumishi wa Mahakama kuwa dunia ya
sasa inahitaji mtumishi anayeweza kujitafutia mwenyewe taarifa muhimu na huku
akitolea mfano taarifa za mageuzi ya shughuli za Mahakama.
Jaji
Mkuu aliwatoa hofu watumishi kwamba matumizi ya mtandao (TEHAMA) hayatasababisha
nafasi zao za kazi kuchukuliwa bali zitabaki zilivyo isipokuwa zitarahisishwa,
kwa mfano mlinzi unayezunguka na rungu kila sehemu, teknolojia hii itamtaka
ukae kwenye screen ya kompyuta na kuangalia kila sehemu na endapo atamwona mtu
ambaye hakupaswa kuwa kwenye eneo lake ataweza kutoa taarifa kwa polisi.
Jaji
Mkuu alisema safari ya Mahakama mtandao inategemea Mhimili wa Serikali kama
ambavyo mkongo wa Taifa wa mawasiliano unavyomilikiwa na serikali na ndiyo
wanamiliki barabara ya mageuzi ya Mahakama mtandao hivyo tunategemea sana sera
za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. “Mahakama ni wapangaji ni
lazima ifuatilie maendeleo na maelekezo yote yanayotolewa na maamuzi
yanayofanywa na serikali kuhusu mtandao, alieleza Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu Prof. Juma aliwakumbusha watumishi kuwa mageuzi ya Mahakama mtandao na
huduma zake hazitawatenga wananchi pia, wanapofuata huduma za utoaji haki
kutoka kwa watumishi, hali kadhalika wadau wa Mahakama, wanavyo vigezo vyao
wanavyotumia kuwapima kila siku.
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba, Mhe. Temi Kilekamajenga akisoma ripoti ya utendaji kazi wa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba alisema, kasi ya umalizaji wa mashauri imeongezeka kwa asilimia 100 kwa mwezi Julai, 2021. Alifafanua kuwa jumla ya Mashauri 125,760 kati ya mashauri 125,746 yaliyofunguliwa katika Mahakama ngazi zote yalisikiliwa ambapo ni sawa na asilimia 100. Taarifa hii ikilinganishwa na taarifa ya mwezi Juni umalizaji wa mashauri ulikuwa ni asilimia 99.
Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni kutofungwa kwa mashauri ya Mirathi. Alisema kati ya mashauri 32,673 ya mirathi yaliyopo mahakamani, mashauri 29,259 hayajafungwa. Taarifa hii ikiliganishwa na taarifa ya mwezi Juni inaonesha kuwa mashauri ambayo hayajafungwa yameongezeka kutoka 28,129 hadi 29,259.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba (hawapo pichani) amewataka watumishi wote wa
Mahakama kujiandaa kuingia kwenye matumizi ya tecknolojia kwa kuwa Mahakama
imewekeza zaidi kwenye eneo hilo, kushoto ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Temi Kilekamajenga na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbet Chuma.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Temi Kilekamajenga na kulia akisoma taarifa ya utekelezaji wa kazi mbele ya watumishi(hawapo pichani) wakati wa kikao hicho, (katikati ni) Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbet Chuma.
Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mhe. Angaza Mwaipopo (aliyesimama) akitoa neno la shukrani kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa niaba ya watumishi wote wa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba mara baada ya kikao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mwenye kizibao cha orange) akizungumza na baadhi ya Wakandarasi wanaosimamia ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili linalojengwa Wilaya ya Bukoba Vijijini.
Mmoja ya mkandarasi anayesimamia ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili linalojengwa Wilaya ya Bukoba Vijijini akimwongoza kukagua na akimwelekeza jinsi ujenzi unavyoendelea Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alipofanya zoezi hilo.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo Nyakibimbili linalojengwa Wilaya ya Bukoba Vijijini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni