-Atoa rai kwa Watumishi wa umma kujituma kwa manufaa ya Taifa
Na Mary Gwera, Mahakama
Mtendaji
Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru leo amemkabidhi
rasmi Ofisi Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole
Gabriel aliyeapishwa Agosti 21, 2021 baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kushika wadhifa huo.
Akizungumza
kabla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika leo Septemba 08, 2021, Bw. Kabunduguru
ametoa wito kwa Watumishi wa Mahakama na Watumishi wa umma kwa ujumla kufanya
kazi kwa kujituma kwa maendeleo ya Taifa.
“Harakati
za kujenga Taifa zinahitaji ushiriki wa Watumishi wake ili kufikia azma ya maendeleo
ya wananchi na Taifa kwa ujumla, hivyo natoa wito kwa watumishi walioko kazini
kuwajibika ipasavyo ili kujenga Taifa,” alisema.
Alisema
kuwa Utumishi wa umma umelenga katika kutoa huduma kwa umma, hivyo ni muhimu
watumishi kuendelea kuwahudumia vyema wananchi.
Kwa upande wa Mahakama, Mtendaji Mkuu huyo mstaafu
alimuhakikishia Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa Mahakama ipo katika hali nzuri
huku akimuomba kuendeleza maboresho yaliyopo na ambayo yapo kwenye michakato
mbalimbali.
Naye
Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel alimshukuru Bw. Kabunduguru kwa
mapokezi mazuri, vilevile kumpongeza kwa kazi nzuri ya kutumikia Taifa na Mahakama
katika utumishi wake.
“Napenda
nikushukuru Kaka yangu kwa mapokezi mazuri na zaidi ya yote nikushukuru kwa kazi
nzuri kwa Mahakama, nami nikuhakikishie kuwa sikuja hapa kutengua torati bali kukamilisha
torati, pale mlipoishia watangulizi wangu nami nitaendeleza,” alisema Mtendaji
Mkuu.
Aliongeza
pia atashughulikia yale yote aliyoelekezwa na Mhe. Rais kuhusu kuboresha
maslahi ya watumishi, mirathi ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya
kufanyia kazi, matumizi ya TEHAMA Mahakamani na mengineyo.
Nae
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma amemuhakikishia kumpa
ushirikiano Mtendaji Mkuu wa Mahakama, vilevile amemshukuru Bw. Kabunduguru kwa
utumishi wake mahakamani na kumuomba kutosita kutoa msaada kwa Mahakama pale
atakapohitajika.
Prof. Elisante Ole Gabriel ni Mtendaji Mkuu wa tatu wa Mahakama ya
Tanzania tangu kuanzishwa kwa nafasi hiyo ndani ya Mhimili huo kwa mujibu wa
Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Namba 4 ya mwaka 2011. Mtendaji Mkuu wa Kwanza
alikuwa ni Mhe. Balozi Hussein Athuman Kattanga (Sasa Katibu Mkuu Kiongozi)
ambaye alifuatiwa na Bw. Mathias Kabunduguru ambaye amestaafu kwa mujibu wa
sheria.
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru (kulia) akikabidhi nyaraka za Ofisi kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel Ofisini kwake Mahakama ya Rufani Jijini Dar es Salaam leo Septemba 08, 2021.
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu Mstaafu, Bw. Kabunduguru (kulia) akitoa neno wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyoshuhudiwa na baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo wa Mahakama pamoja na Waandishi wa Habari waliohuddhuria. Kushoto ni Prof. Elisante Ole Gabriel akimsikiliza kwa umakini.
Mtendaji Mkuu akizungumza jambo mara baada ya kukabidhiwa rasmi ofisi na Mtangulizi wake, Bw. Mathias Kabunduguru.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.
Wilbert Martin Chuma akitoa neno la shukrani mara baada ya hafla hiyo ya
makabidhiano.
Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania,Prof. Elisante Ole Gabriel ( aliyeketi katikati) akiwa
kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Menejimenti ya Mahakama mara baada ya
hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Mtendaji Mkuu, wengine ni (kulia) Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Martin Chuma na kushoto ni aliyekuwa
Mtendaji Mkuu wa Mahakama Bw. Mathias Kabunduguru.
Mtendaji Mkuu Mstaafu, Bw. Kabunduguru (kushoto) akiagana na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Martin Chuma (kulia) mara baada ya hafla ya kukabidhi Ofisi, anayeshuhudia (katikati) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Ole Gabriel.
(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni