Na Innocent Kansha – Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania
ameahaidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Mahakama ya Haki ya Afrika
Mashariki na kuwapongeza Wakuu wa nchi wanachama kwa kuwaamini Viongozi hao
kusimamia majukumu ya Mahakama hiyo, kwani haki ni msingi wa amani pasipo haki hakuna utangamano.
Akizungumza na viongozi hao walioongozwa
na Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki waliomtembelea Ofisini kwake
Jijini Dar es salaam mapema leo Septemba 10,2021, Jaji Mkuu Prof. Juma alisema
Mahakama ya Tanzania inaongozwa na Mpango Mkakati wake, wenye nguzo kuu tatu
ambazo ni Utawala bora, uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali, Upatikanaji na
utoaji haki kwa wakati na Kuimarisha Imani ya wananchi na Ushirikishwaji wa
wadau.
“Kwa sababu tunaamini
kwamba ukiwa na utawala bora, uwajibikaji, matumizi mazuri ya rasilimali watu
na fedha kwa kutumia viwango hivi utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa haki kwa
wote na kwa wakati, kwani haki ni msingi wa amani bila haki hakuna utangamano”,
alieleza Jaji Mkuu.
Prof. Juma alisema kwa
upande wa nguzo zinazoijenga Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kama vile mtangamano
wa kisiasa, ushuru wa forodha, soko huru na sarafu ya pamoja kwa nchi wananchama
wa Jumuiya ya Afrika Masharika bila shaka hakukosekani usuluhishi wa migogoro mara
nyingi nchi hizi hazitumii vizuri chombo hiki kutatua migogoro yao.
Jaji Mkuu akaongeza kuwa
changamoto ya kuhakikisha wananchi wanapata haki ya kweli bado ni kubwa
ukiangalia jiografia ya nchi hii utaona kuna maeneo mengi ya vijijini mwananchi
anatembea mwendo mferu kuifuata haki, wengi hawafahamu sheria na taratibu na
miundo mbinu mingine sio rafiki kama umeme, barabara na miundombinu ya majengo
hususani ya Mahakama kwa kushirikiana na Mahakama yenu haki inaweza kufikiwa
kwa haraka zaidi.
Naye, Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mahariki
Jaji Nestar Kayobela alisema anamshukuru Jaji Mkuu kwa niaba ya uongozi wa
Mahakama ya Tanzania, ujumbe wake ni kuendeleza mazuri ya mtangulizi wake kwa
kipindi chake cha miaka saba ijayo ya uongozi kwa kuzingatia mambo makuu
matatu.
Akielezea mambo hayo
makuu matatu ambayo ndiyo dira ya uongozi wake kwa kipindi cha miaka saba ni
falsafa ya kufanya kazi kwa kushirikiana (team work), jambo lingine ni kuongoza
kwa nia njema (good faith) pamoja na shughuli za kimahakama kuendeshwa
kidiplomasia (Judicial Diplomacy).
Jaji Kayobela akaongeza
kuwa wamefufua mashirikiano na kuendesha mikutano ya Majaji Wakuu wa nchi
wanachama wa Jumuiya inayounda Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na Majaji
hao walikutana mjini Kigali mwezi mei 2021 na kuazimia mkutano mwingine
utafanyika mwezi Disemba 2021 Jijini Nairobi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha programu
ya kuwafunza Majaji na Mahakimu wa nchi wanachama wa Jumuiya kwa kuanzia Mahakama
imetoa mafunzo Jijini Bujumbura kwa wadau hao wapatao 420 na hatua inayofuata
mafunzo yanarajiwa kufanyika South Sudani na hatimaye kuzunguka Jumuiya nzima.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel ameuhakikishia ujumbe huo kuupa ushirikiano wa
asilimia mia moja na kuwaambia Mahakama imepiga hatua kubwa sana katika
maboresho mbalimbali ya kuhakikisha mwananchi anapata haki kwa wakati mathalani
matumizi ya TEHAMA, maboresho ya miundombinu ya majengo kwa kujenga mapya na
kukarabati mengine kuanzia ngazi ya Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama Kuu.
Maboresho mengine aliyoyaeleza Mtendaji Mkuu huyo ni Matumizi ya Ofisi mtandao (E- Office), matumizi ya aplikasheni utoaji mrejesho wa huduma za Mahakama kwa mteja (Online Feedback Application), matumizi ya kusajili mashauri kwa njia ya mtandao (E- Failing), utunzaji wa amri na hukumu za Mahakama Kuu na rufani kwa njia ya mtandao (Tanzilii) na kusajili na kuhuisha masahuri kwa njia ya mtandao (JSDS II) na usikilizwaji wa mashauri kwa njia ya mtandao maarufu (Video Conference).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni