-Katibu Mstaafu naye aagwa rasmi na Tume
Na
Mary Gwera, Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amemuapisha rasmi Mtendaji Mkuu
mpya wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel kuwa Katibu wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Katibu wa Tume hiyo, Bw.
Mathias Kabunduguru.
Hafla
hiyo fupi ya uapisho wa Katibu wa Tume imefanyika leo Septemba 10, 2021 katika
Ofisi ndogo za Bunge zilizopo jijini Dar es Salaam huku hafla ikiwa imehudhuriwa na
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, Makamishna
wa Tume hiyo, Katibu Mstaafu, Naibu Katibu wa Tume hiyo pamoja na Watumishi wa
Tume.
Akizungumza
mara baada ya kuapishwa rasmi, Prof. Ole Gabriel alimuhakikishia Jaji Mkuu
pamoja na Viongozi wote wa Mahakama kuwa atajitahidi kufanya kazi kwa pamoja na
kwa ushirikiano ‘team work’ kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa na Mahakama
pamoja na Tume yanafikiwa.
“Naomba
niwahakikishie kuwa nitatumia nguvu zangu zote, uwezo wangu nilionao kuhakikisha
kuwa tunafanya kazi kwa pamoja na kufikia matarajio tuliyo nayo hususani katika
suala la kutoa haki kwa wakati kwa wananchi,” alisema Profesa.
Awali,
akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mstaafu wa Tume hiyo, Bw. Mathias Kabunduguru
alimkaribisha Katibu mpya huku akimdokeza masuala kadhaa ambayo Tume inakabiliwa
nayo ikiwa ni pamoja na upungufu wa Watumishi ambapo idadi ya Watumishi iliyopo
kwa sasa ni 16 na mahitaji halisi ni Watumishi 34.
Hata
hivyo; Prof. Ole Gabriel ameahidi kushughulikia suala hilo la upungufu wa
Watumishi kwa kufanya taratibu stahiki ili kuongeza idadi ya watumishi wa Tume
hiyo ili kuipa nguvu zaidi Tume yenye mamlaka makubwa kitaifa ya kuisimamia
Mahakama nchini.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Kamishna wa Tume
ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, Jaji Kiongozi, Mhe. Dkt. Feleshi, Msajili Mkuu,
Mhe. Wilbert Chuma na Naibu Katibu wa Tume, Bi. Enziel Mtei walimshukuru Bw.
Kabundunguru kwa kufanya kazi kwa kushirikiana kipindi chote alichokuwa Mahakama
na Tume vilevile walimkaribisha Katibu mpya wa Tume na kumuahidi kushirikiana
nae bega kwa bega katika kutekeleza majukumu yake.
Kufanyika kwa tukio hili la uapisho ni kwa mujibu wa Sheria
namba nne (4) ya mwaka 2011 ya Uendeshaji wa Mahakama kifungu cha 16 (ii) ambacho kinamtaka
Jaji Mkuu wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama, kumuapisha Mtendaji Mkuu wa
Mahakama kuwa Katibu wa Tume hiyo.
Katibu Mstaafu wa Tume hiyo, Bw. Kabunduguru akizungumza jambo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni