Jumatatu, 13 Septemba 2021

JAJI DKT. FELESHI AAPISHWA KUWA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

 Na Magreth Kinabo-Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amemwapisha aliyekuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi, kuwa Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali.

Dkt Feleshi anachukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi na mtangulizi wake, Prof. Adelardus Kilangi, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi. Hafla ya uapisho huo ilifanyika Ikulu Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma, amemwelezea Dkt Feleshi ambaye amefanya naye kazi tangu April 4, 2018 hadi leo alipopata kiapo cha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa ni mwadilifu na mtiifu sio tu kwa Rais bali hata kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Dkt Feleshi ni mtiifu sana kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwako Rais. Ni mwadilifu sana, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Maafisa wa Mahakama. Yeye ni mtu wa maboresho, ambaye anapenda Tehama na aliitumia kikamilifu katika kusimamia Mahakama ambazo zimetapakaa nchi nzima,” alisema.

Mhe. Jaji Mkuu alibainisha kuwa kwa mujibu wa Ibara ya 109(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni msaidizi maalumu wa Jaji Mkuu ambaye anasimamia uendeshaji wa  Mahakama Kuu na Mahakama ambazo zipo chini yake, ambazo zinabeba asilimia 80 ya mashauri yote ambayo  yanasikilizwa katika Mahakama za Tanzania.

Bila Tehama usimamizi wa Mahakama ungekuwa mgumu sana. Chai yake asubuhi ni kuangalia mashauri mangapi yamesajiliwa, mangapi yametolewa hukumu, mlundikano wa mashauri upo katika hali gani, Mahakama ipi imemeba mzigo zaidi, kwa hiyo anasimamia kazi hiyo kila siku,” alisema Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu alimwelezea pia Dkt Feleshi kama mtu anayependa kuwasaidia watumishi wa chini kwa vile ana uwezo wa kutambua vipaji, kuvijenga na kuviendeleza. Hivyo, ni imani yake Dkt Feleshi ataweza kusaidia katika eneo hilo kwa nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu wa serikali.

Prof. Juma alitumia nafasi hiyo kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania kuwapongeza viongozi waliopishwa kwa kupewa imani kubwa na Mheshimiwa Rais, kwamba wataweza kusimamia ustawi wa wananchi.

“Mawaziri wa Wizara zote mlioapishwa leo ni muhimu sana kwa taifa na Mahakama ya Tanzania. Ulinzi, Mawasiliano na Teknolojia, Nishati na Ujenzi ni muhimu kwa Tanzania na kwa Mahakama,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahamaka ya Tanzania inamtegemea Waziri wa Tehama kuisaidia kuingia katika karne ya 21, karne ambayo mheshimiwa Rais amewahi kusema  inasukumwa na  Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.

Dkt Feleshi anakuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa kumi tangu nafasi hiyo ilipoanziashwa hapa nchini. Mwanasheria Mkuu wa kwanza alikuwa Roland Brown aliyehudumu nafasi hiyo kuanzia mwaka 1964 hadi 1965 na kufuatiwa na Hayati Jaji Mark Bomani aliyeshika wadhifa huo tangu 1965 hadi 1976.

Wengine ni Jaji Joseph Sinde Warioba (1976-1985), Jaji Damian Lubuva (1985-1993), Andrew Chenge (1993-2005), Johson Mwanyika (2005-2009), Jaji Frederick Werema (2009-2014), Jaji George Masaju (2014-2018) na Prof. Adelardus Kilangi (2018-2021).

 

Jaji Mhe. Dkt Eliezer Mbuki Feleshi, aliyekuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania akiapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Mwanasheria Mkuu mpya wa Serikali leo. Hafla hiyo imefanyika leo Ikulu ya Chamwino mjini Dodoma.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni