Na Lydia Churi- Mahakama, Moshi
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wametakiwa kutoa
huduma bora kwa wananchi zinazoendana na ubora wa majengo ya Mahakama
yaliyojengwa na yanayoendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania
kanda ya Arusha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole
Gabriel amewataka watumishi hao kuzingatia maadili na weledi na kutoa huduma
bora kwa Watanzania ili haki iweze kupatikana kwa wakati.
“Tumejenga majengo sita ya vituo Jumuishi vya Utoaji
haki katika miji ya Dodoma, Morogoro, Mwanza na hapa Arusha kwa lengo la
kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi hivyo huduma mnazotoa ni lazima
ziendane na uzuri wa majengo haya” alisema.
Aliwataka watumishi wa Mahakama kuzingatia mambo matano
muhimu wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku. Prof. Ole Gabriel aliyataja
mambo hayo kuwa ni kutobaguana kwa namna yoyote, kuacha uvivu na uzembe, kutojihusisha
na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili, pamoja na kutochelewesha mashauri
mahakamani pasipokuwa na sababu za msingi.
Aidha, Mtendaji Mkuu pia aliwasisitiza watumishi wa
Mahakama Kuu kanda ya Arusha kuongeza kasi kwenye matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha utendaji kazi, kuongeza uwazi
katika mnyororo wa utoaji haki na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa
watumishi wa kada mbalimbali.
“Mahakama inakabiliwa na upungufu wa watumishi 10,320
wa kada mbalimbali hivyo matumizi ya Tehama yatasaidia kupunguza changamoto
hiyo kwa kiasi kikubwa. Hivi sasa Mahakama ina jumla ya watumishi 5,835 kwa
nchi nzima”alisema Prof. Ole Gabriel.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania anaendelea na ziara yake ya
kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama na kuungumza na watumishi wa
Mahakama kwa lengo la kujitambulisha. Tayari amekagua ujenzi wa jengo la makao
makuu ya Mahakama, Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki vilivyopo Dodoma na Arusha pamoja
na majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya yaliyopo Dodoma,
Manyara na Arusha.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kamda ya Arusha wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alipozungumza nao wakati wa ziara yake kwenye kanda hiyo . Lengo la ziara hiyo ni kujitambulisha kwao na kutoa maelekezo ya utendaji kazi.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kamda ya Arusha wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (Mbele katikati) mara baada ya kuzungumza wakati wa ziara yake kwenye kanda hiyo
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akitazama ramani ya Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kilichopo jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni