Jumamosi, 4 Septemba 2021

KAMPENI YA HAKI MIRATHI WAJIBU WANGU YAWAFIKIA WANANCHI WAPATAO 5984

Na Innocent Kansha – Mahakama.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke Mhe. Nyigulila Mwaseba amefunga rasmi kampeni ya mafunzo ya Haki Mirathi wajibu wangu ilyofanyika Wilaya ya Temeke kwa takribani siku sitini (60) na kuwafikia wananchi wapatao 5984 walojiandikisha kupata elimu hiyo.

Akifunga kampeni hiyo iliyobeba kauli mbiu ya Haki Mirathi wajibu wangu katika ukumbi wa mikutano wa Iddi Nyundo uliopo Manispaa ya Temeke na kuwashirikisha wadau Jana Septemba 3, 2021. Kwa niaba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Temeke Mhe. Ilvin Mugeta, Jaji Mwaseba aliema kuwa Elimu iliyotolewa ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Mahakama wa miaka mitano ulioanza mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021 na mafunzo haya yanaifafaua nguzo ya tatu ya mpango huo, ushirikishwaji wa wadau na kurejesha imani ya wananchi kwa Mahakama katika wajibu wa utoaji wa haki.

“Elimu hii iliyotolewa kwa viongozi na wananchi wa Wilaya hii imefanyika kwa muda muafaka hasa ukizingatia kuwa, tuna jengo jipya la Mahakama Divisheni ya Familia lililopo Temeke, lina ngazi zote za Mahakama, yaani Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu Divisheni Maalumu ya Familia ambalo litakuwa na wajibu mkubwa wa kusikiliza mashauri ya Ndoa na Mirathi tuu”, akinukuu Jaji Mwaseba

Jaji Mwaseba alisema Kampeni hii itakuwa imetoa ufumbuzi na kuondoa sitofahamu nyingi kwa wananchi mathalani; Mabadiliko ya Sheria ya Mirathi mfano; ni kiwango kipi cha thamani ya Mirathi kifunguliwe katika Mahakama ipi kwani kiwango cha thamani kwa sheria ya zamani na ya sasa ni tofauti.

Mambo mengine ya msingi ni umuhimu wa uandishi wa Wosia hivyo Wanachi wa Wilaya ya Temeke sasa mtaanza kuwa na utamaduni wa kuandika wosia ili kuepusha migogoro ya Mirathi. Uandishi sahihi wa wosia ambao una nguvu ya kisheria na warithi ni watu wa aina gani na sababu ya mrithi kunyimwa urithi, alieleza Jaji Mwaseba

Jaji huyo aliongeza kuwa Elimu hii imetoa mwanga kuwa, umuhimu wa mirathi kutangazwa kwa umma kabla ya kuanza kusikilizwa na muda wa kutangazwa hadi kuanza kusikilizwa, majukumu ya Msimamizi wa Mirathi na kuwezesha Mirathi kufungwa kwa wakati na hakutakuwa na upotevu wa mali za marehemu na migogoro katika familia haitakuwepo na vile vile umuhimu wa kufunga Mirathi na pia kujua madhara ya kutofunga Mirathi husika kwa wakati.

Naye, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mhe. Susan Kihawa akisoma ripoti ya utekelezaji wa kampeni hiyo alielezea mafanikio mbalimbali yaliyotokana na zoezi hilo, ikiwa ni pamoja na kutoa Elimu kupitia vyombo vya Habari kama Televisheni na Radio mfano; Azam Televisheni, Channel Ten, ITV, Ayo TV na Radio za Clouds FM, TBC, KISS FM na RFA zilitumika kufikisha elimu hii kwa umma, katika mchakato huo jumla ya vipindi tisa vilirushwa hewani.

Mhe. Kihawa aliongeza kuwa, Kampeni ilifanikisha kutoa elimu kwa Viongozi wa Serikali za Mtaa na Kata, ikiwemo viongozi wa Chama cha Mapinduzi wa ngazi zote wapatao 633, wanafunzi wa shule za Sekondari kuanzia kidato cha tatu na nane wanaokadiriwa kufikia 4853 ndani ya Manispaa ya Temeke.

Aidha, kampeni hii imesaidia kufanikisha utunzaji wa majalada ya mirathi kwa njia ya TEHAMA kwa kuorodhesha mashauri ya Mirathi yaliyofunguliwa katika Mahakama zote katika mfumo wa ndani kwa majalada ya Mirathi ya mwaka 2017, 2018, 2019, 2020 na 2021 yameorodheshwa.

Kupitia elimu hiyo imefanikisha kuandaa na kuchapisha kijitabu chenye maswali hamsini (50) yaliyoulizwa mara nyingi na wadau wakati wa kampeni ya haki mirathi na kuvisambaza kwa watendaji katika Kata zote za Manispaa ya Temeke, alisema Mhe. Kihawa.

Mhe. Kihawa aliongeza kuwa, kupita kampeni hiyo timu ya elimu ilifanikiwa kugawa vitabu vya sheria ya mirathi, vitini na kablasha za kujisomea kwa wadau mbalimbali waliofikiwa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha club za wanafunzi katika shule za sekondari za kutoa elimu ya mirathi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Joketi Mwegelo aliupongeza uongozi wa Mahakama na viongozi wote wa Wilaya ya Temeke waliohusika kuratibu na kufanikisha kampeni hiyo imetoa mchango mkubwa wa kutatua kero ya wananchi waliokuwa hawafahamu waanzie wapi kutatua changamoto za kisheria kwenye masuala ya mirathi.

“Mara zote mwananchi anapofuata huduma anatarajia kupata majawabu yaliyo sahihi kutoka kwa wataalam na jukumu kubwa la wataalam ni kutengeneza mfumo utakao mrahisishia mwananchi kupata haki kwa wakati na kama mfumo unakwamisha au kuchelewesha kupata haki basi ubalishwe ili mwananchi apate haki yake na ndilo jukumu letu sote”, aliongeza Mkuu huyo wa Wilaya.

Kampeni hiyo iliratibiwa na Ungozi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ofisi ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Temeke pamoja na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke Mhe. Nyigulila Mwaseba akitoa hotuba ya kufunga kampeni ya Haki Mirathi wajibu wangu katika ukumbi wa mikutano wa Iddi Nyundo uliopo Manispaa ya Temeke na kuwashirikisha wadau Jana Septemba 3, 2021. Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Joketi Mwegelo na kulia ni Wakili wa Serikali kutoa RITA Salvius Rwechungura.

 

Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Joketi Mwegelo akitoa neno wakati wa kufunga Kampeni ya Haki Mirathi wajibu wangu, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke, Mhe. Nyingulila Mwaseba na kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke Arnold Peter

Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Temeke Mhe. Susan Kihawa akisoma ripoti ya utekelezaji wa kampeni hiyo.

 

    Baadhi ya wadau walioshiriki kwenye mkutano huo wa Haki Mirathi wajibu wangu.

 Baadhi ya wadau walioshiriki kwenye mkutano huo wa Haki Mirathi wajibu wangu.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke Mhe. Nyigulila Mwaseba akimkabidhi tuzo ya ushiriki kwenye kampeni ya Haki Mirathi wajibu wangu  Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Joketi Mwegelo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke Mhe. Nyigulila Mwaseba akimkabidhi cheti cha ushiriki kwenye kampeni ya Haki Mirathi wajibu wangu mmoja ya mwanafunzi aliyefanya vizuri.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke Mhe. Nyigulila Mwaseba (wa pili kulia walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mahakimu walioshiriki kutoa elimu ya haki mirathi, wengine ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bi. Joketi Mwegelo (wa pili kushoto), Wakili wa Serikali kutoa RITA Salvius Rwechungura (kulia) na kushoto ni  Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke Arnold Peter

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda Maalumu ya Temeke Mhe. Nyigulila Mwaseba (wa pili kulia walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na Walimu na Wanafunzi wa shule za sekondari za Manispaa ya Temeke walioshiriki na kufanya vizuri katika elimu ya haki mirathi, wengine ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama  ya Wilaya ya Temeke Mhe. Susan Kihawa  (wa pili kushoto), Wakili wa Serikali kutoa RITA Salvius Rwechungura (kulia) na kushoto ni  Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke Arnold Peter.

Picha na Innocent Kansha - Mahakama.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni