Na Lydia Churi-Mahakama
Watumishi wote wa Mahakama nchini wenye nia ya kutaka
kuhama na kwenda kwenye Taasisi nyingine za Serikali kwa lengo la kutafuta mazingira
mazuri ya kufanyia kazi wameshauriwa kutokufanya hivyo kwa kuwa Mhimili huo
umedhamiria na unaendelea kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya
watumishi wake.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.
Elisante Ole Gabriel ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara pamoja na Mahakama ya wilaya ya Babati akiwa
katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kujitambulisha kwa watumishi wa
Mahakama na kutoa maelekezo ya utendaji kazi.
“Tunaboresha mazingira, wenye nia ya kuhama waache
hayo mawazo, tutengeneze nyumba yetu kwani hakuna mtu wa kututengenezea.
Nashauri hama unapodhani kuna umuhimu wa kufanya hivyo, usihame kwa kufuata
mkumbo”, alisema prof. Ole Gabriel.
Aidha, Mtendaji Mkuu wa Mahakama amewataka watumishi
wote wa Mahakama nchini kukwepa mambo matano muhimu ambayo ni rushwa na uzembe kazini,
ubadhirifu wa mali za Umma, lugha zisizo na staha hasa kwa wateja wanaofika
mahakamani, kubaguana na kuchelewesha kumalizika kwa mashauri pasipokuwa na sababu za msingi.
Prof. Ole Gabriel amewashauri watumishi hao
kujiendeleza kielimu ikiwezekana hata nje ya taaluma zao ili kuwaongezea ujuzi
mbalimbali utakaowezesha kuboresha utendaji kazi wao na akawataka viongozi wa
Mahakama kutowazuia watumishi wanaotaka kujiendeleza kielimu. “Wakubwa kuweni
na kauli nzuri kwa watumishi walio chini yenu, muwajali na kuheshimiana”,
alisisitiza.
Awali akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo
kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, Afisa
Tawala wa Mahakama hiyo Bw. Christopher Msagati alisema ili kuendana na kasi ya
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mahakama ya
Tanzania haina budi kuweka Maafisa Tehama katika ngazi za mikoa ili kurahisisha na
kuboresha utendaji kazi. Hivi sasa kazi za Tehama hufanywa na Maafisa waliopo
kwenye ngazi za kanda.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania anaendelea na ziara ya
kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama na kuzungumza na watumishi wa
Mahakama kwa lengo la kujitambulisha. Tayari amekagua ujenzi wa majengo
mbalimbali ya Mahakama na kuzungumza na watumishi wa Kanda ya Dodoma na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Mahakama ya wilaya ya Babati.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Mahakama ya wilaya ya Babati wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.
Waheshimiwa Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Mahakama ya wilaya ya Babati wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel .
Maafisa Tawala na Maafisa Utumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Mahakama ya wilaya ya Babati wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel .
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara na Mahakama ya wilaya ya Babati wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel .
Watumishi wa kada ya Madereva wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara wakiwa katika picha ya pamoja na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel .
Atende tu kama alivyoahidi maana watumishi tumezichoka ahadi.
JibuFuta