Ijumaa, 22 Oktoba 2021

KAIMU MKUU WA CHUO ATOA UJUMBE MZITO KWA BODI YA HAKI BULLETIN

Na Faustine Kapama-Mahakama, Lushoto.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Bw. Goodluck Chuwa ametoa rai kwa Wajumbe wa Bodi ya Jarida la Mahakama ya Tanzania la Haki Bulletin kuzingatia uaminifu, ukweli, uadilifu na weledi wanapotekeleza majukumu yao, ikiwemo kuuhabarisha umma juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na Mhimili huo.

Akizungumza katika kilele cha mafunzo ya Bodi hiyo yaliyofanyika katika Chuo hicho hivi karibuni, Bw. Chuwa alisema kazi ya uandishi wa habari na uhariri wa habari na makala ni kazi muhimu inayohitaji utulivu, nidhamu, umakini na weledi wa hali juu.

“Kwa hiyo, mnapaswa kutoa habari zenye ubora na viwango vya hali ya juu ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Mahakama ya Tanzania na hata kuwapa nafasi ya kutoa maoni yao juu ya uboreshaji zaidi wa huduma zitolewazo na Mahakama,” alisema.

Bw. Chuwa alibainisha kuwa kazi za uandishi wa habari na uhariri zina maadili yake, kama ilivyo Mahakama ambayo ina maadili na tamaduni zake. Amesema kuwa vyote hivyo vimejengeka kwa miaka mingi, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuendelea kuwa mlinzi wa tamaduni na maadili hayo.

“Katika kazi hii ya uhariri tuzingatie uaminifu, ukweli, uadilifu na weledi. Ni matumaini na rai yangu kuwa habari mtakazokuwa mnazitoa zitakuwa mfano bora kwa vyombo vingine vya habari jinsi 9ya kuandika habari za kimahakama,” aliwaambia Wajumbe wa Bodi hiyo.

Amesema kuwa maadili ya uandishi na uhariri wa habari au jarida na maadili ya kimahakama hayakinzani, ambapo habari inayohusisha pande mbili au zaidi zinazokinzana huandikwa baada ya kupata maelezo ya pande zote na kuchujwa ili kuepuka uandishi na uhariri wa kishabiki, hatua ambayo hufanywa pia na Mahakama kabla ya kutoa uamuzi wake.

Aidha, Bw. Chuwa alisema kuwa ni jambo lisilopingika kuwa uandishi na uhariri wa habari zinazohusu Mahakama unahitaji uangalifu zaidi kuliko kushughulikia habari nyingine. Ameeleza kuwa mara nyingi magazeti yamekuwa yakiandika habari bila kufahamu undani wake na mara nyingine bila kuwa na usahihi.

“Wakati mwingine, uandishi huo hauzingatii muktadha wala kutafakari mwananchi wa kawaida ataitafsiri vipi habari hiyo na hivyo kuitoa bila kutathmini athari zake. Hali hii inaweza kuleta mtafaruku kwa jamii, watu binafsi au taasisi. Sitegemei, hasa baada ya ninyi kupata mafunzo haya siku moja Msajili au kiongozi yeyote wa Mahakama atalazimika kujitokeza mbele ya vyombo vya habari kutolea ufafanuzi habari ambayo ninyi mtakuwa mmeitoa,” aliwaambia Wajumbe hao wa Bodi.

Kaimu Mkuu wa Chuo amesema pia kuwa elimu haina mwisho na hakuna elimu iliyokamilika, hivyo alitoa rai kwa wajumbe wasio na taaluma ya uandishi wa habari, wajifunze misingi ya taaluma hiyo na wale ambao hawana taaluma ya sheria wajifunze misingi ya sheria na uendeshaji wa shughuli za kimahakama.

Bw. Chuwa amebainisha kuwa Chuo cha Uongozi wa Mahakama kimewahi kuendesha mafunzo ya uandishi wa habari za kimahakama na kipo tayari, kwa kushirikiana na wadau, kuendelea kutoa mafunzo hayo kila yatakapohitajika. Hivyo, ni rai yake kuwa uongozi wa Mahakama utaendelea kufuatilia habari za kimahakama zinavyofikishwa kwa jamii na hatua stahiki zichukuliwe pale itakapoonekana kuna upotoshaji, aidha kwa makusudi au kwa kukosekana uelewa.

“Pale itakapobidi, kama hatua ya mwisho, Mahakama inaweza kuwataka waandishi wote wa habari za kimahakama wapate mafunzo mahsusi kama kigezo cha kuwaruhusu kuandika habari hizo, kama ilivyofanyika kwa Madalali wa Mahakama,” amesema.

Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto uliandaa mafunzo ya siku tano yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi ya Uhariri wa Jarida la Mahakama la Haki Bulletin na washiriki wengine kutoka chuo hicho. Wajumbe walipitishwa katika mada mbalimbali zilizogusa maeneo kadhaa, ikiwemo uhariri wa habari na makala, upigaji picha na uandishi wa maelezo ya picha na matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili katika jarida.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Uhariri, Mhe. Dkt. John Utamwa, ambaye ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu wa Tanzania, Kanda ya Iringa. Dkt. Utamwa amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Mustapher Siyani, ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wote, Mjumbe wa Bodi Benjamin Mlimbila aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania, chini ya Jaji Mkuu, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamisi Juma kwa kutoa kibali cha kufanyika kwa mafunzo hayo.

Aliwashukuru pia Wawezeshaji wote kwa mada nzuri walizotoa ambazo zimewawezesha kujifunza mambo mengi ambayo yataboresha utendaji wao wa kazi, hatua ambayo imewaongezea ufanisi na ujuzi wa kutosha katika utoaji wa taarifa za matukio na kazi mbalimbali zinazofanywa na Mahakama.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Bw. Goodluck Chuwa akizungumza na Washiriki wa Mafunzo ya Bodi ya Uhariri (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya kufunga Mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.Washiriki wa Mafunzo ya Bodi ya Uhariri ya 'Haki Bulletin' wakiwa katika Mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa ambaye pia ni Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Uhariri ya Haki Bulletin, Mhe. Dkt. John Utamwa (aliyeketi kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mafunzo ya Bodi hiyo. Aliyeketi katikati ni Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Bw. 
Goodluck Chuwa na kulia ni Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi hiyo, Mhe. Charles Magesa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni