Jumatatu, 18 Oktoba 2021

MWENYEKITI MPYA ‘HAKI BULLETIN’ ATAKA HABARI ZENYE VIWANGO

Na Margreth Kinabo na Mary Gwera, Mahakama-Lushoto.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt John Utamwa, leo Oktoba 18, 2021 amefungua mafunzo ya Bodi ya Uhariri wa Jarida la Mahakama la ‘Haki Bulletin’ na kusisitiza wajumbe kuzingatia maadili, ubora na weledi ili kutoa habari zinazokidhi viwango. 

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku tano ambayo yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Bodi ya Uhariri ya Mahakama ya Tanzania na wengine, Dkt Utamwa, ambaye ndiye Mwenyekiti mpya wa Bodi hiyo, amesema kuwa utoaji wa habari zenye ubora na viwango vya hali ya juu kutakuza imani ya wananchi kwa Mahakama ya Tanzania na hata kuwapa nafasi ya kutoa maoni yao juu ya uboreshaji zaidi wa huduma zinazotolewa.

“Hivi sasa Mahakama ya Tanzania inafanya maboresho makubwa katika kuendeleza Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano. Mahakama pia inatekeleza mipango na sera mbalimbali za serikali katika eneo la utoaji haki. Maboresho haya yote yanawalenga wananchi. Kwa hiyo, kuuhabarisha umma juu ya maboresho hayo na shughuli nyingine za kimahakama ni wajibu wetu wa kikatiba ambao hatuwezi kuukwepa,” amesema Jaji Utamwa.

Dkt. Utamwa amebainisha kuwa Watanzania pia wanayo haki ya kikatiba ya kupata taarifa kuhusu Mahakama yao, hivyo uanzishaji na uimarishaji wa Jarida la Mahakama la ‘Haki Bulletin’ ni jambo muhimu kwa vile linaashiria juhudi za dhati za Mahakama ya Tanzania katika kuwapa Watanzania haki yao ya Kikatiba. “Ibara ya 18(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya 1977 inampa kila mtu, pamoja na mambo mengine, haki ya kupata taarifa au habari kuhusu masuala muhimu ya maisha, shughuli za watu na masuala nyeti kwa jamii. Huduma za kimahakama ni moja ya mambo haya,” alisema.

Kwa mujibu wa Jaji Utamwa, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano cha Mahakama ya Tanzania kina wajibu wa kutangaza na kutoa elimu kwa umma na wadau wa Mahakama kuhusu shughuli na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania, ambapo jukumu hilo hutekelezwa kwa njia mbalimbali likiwemo Jarida la ‘Haki Bulletin,’  alisisitiza.

Aliongeza kuwa jukumu hilo limekusudiwa kuupa umma wa Watanzania uelewa wa kutosha kuhusu shughuli mbalimbali za kimahakama. Hatua hii inaondoa changamoto ya uelewa hafifu wa Wadau wa Mahakama kuhusu taratibu na huduma za kimahakama.

Kadhalika, Jaji Utamwa alisema kuwa elimu hiyo itawapa wadau wetu ufahamu zaidi kuhusu namna Mahakama inavyotekeleza kwa vitendo Nguzo ya Tatu ya Mpango-Mkakati wake wa miaka mitano (The Judiciary Strategic Plan 2020/21 - 2024/25), inayosisitiza juu ya ushirikishwaji wa wadau wa katika shughuli za Mahakama. Kwa sababu hiyo, Dkt Utamwa alibainisha kuwa Jarida la ‘Haki Bulletin’ lina umuhimu zaidi kwa sasa kuliko ilivyokuwa awali na ni jukumu la wajumbe sasa, kufunga mikanda zaidi ili Jarida lifanye vizuri zaidi. 

Alisisitiza pia kuwa uandishi na uhariri wa habari zinazoihusu Mahakama unahitaji uangalifu zaidi kuliko kushughulikia habari nyingine, ambapo mara nyingi magazeti yanaandika habari bila kufahamu undani wake, jambo ambalo linaweza kuleta mtafaruku kati ya watu binafsi au Taasisi.

“Sina mashaka kabisa kwamba Uongozi wa Mahakama una imani kubwa na sisi sote na unathamini kazi yetu. Kushiriki kwetu katika mafunzo haya ni uthibitisho wa imani hiyo. Kuaminiwa huku kutaendelea kukua zaidi ikiwa tu viwango vyetu vya utendaji vitakuwa bora zaidi kuliko ilivyokuwa awali, kabla ya mafunzo haya. Ni matarajio yangu kwamba siku hizi tano za mafunzo haya zitakua za manufaa makubwa kwetu na kwa Mahakama ya Tanzania,” alisema.

Jarida la ‘Haki Bulletin’ lilianzishwa siku nyingi na kupata usajili Mwaka 2016 na baada ya hapo limeshika kasi na taratibu thabiti za kulisambaza na kuliratibu zimewekwa vizuri. Jaji Mfawidhi Utamwa alimpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Uhariri aliyetangulia, Mhe. Jaji Mustapher Siyani, ambaye kwa sasa ni Jaji Kiongozi, pamoja na wajumbe wote wa Bodi, kwa kufanikisha uhuishaji wa Jarida hilo.

“Hii ni changamoto kwangu mimi ambaye sasa ninapokea kijiti na kuvaa viatu vya Mwenyekiti aliyetangulia. Ingawa sina uhakika kama miguu yangu itavitosheleza viatu hivyo, mashaka yangu yanapungua kwa kuamini kuwa Wajumbe wa Bodi na Wanataaluma mpo na tutashirikiana kwa dhati ili kuendeleza huduma za Jarida pale ambapo Mwenyekiti wa awali alipoachia,” alisema.

Akitoa neno la utangulizi, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Charles Magesa, alisema kuwa Bodi ya Wahariri ya ‘Haki Bulletin’ ina Wajumbe nane (8) wenye ujuzi tofauti tofauti na kwamba Jarida hilo linalenga kuuhabarisha umma shughuli na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania. Alisema kuwa kufanyika kwa mafunzo hayo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha ufanisi wa kazi za wajumbe hao.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mwandamizi Victor Bigambo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) alisema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa na Uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo hicho ili kuwajengea uwezo washiriki wote katika kutekeleza majukumu yao vema na kwa ufanisi mkubwa. Mafunzo hayo pia yamehudhuriwa na watumishi kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama ‘IJA’ ili wapate ujuzi zaidi katika uandishi na uhariri, kwa kuzingatia kuwa kuna machapisho mengi yanayotolewa na Chuo hicho.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt John Utamwa akifungua mafunzo ya Bodi ya Wahariri wa Jarida la Mahakama la ‘Haki Bulletin’. Mhe. Dkt. Utamwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo amewasisitiza wajumbe wa Bodi  kuzingatia maadili, ubora na weledi ili kutoa habari zinazokidhi viwango. 
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni Mhariri wa Jarida la 'Haki Bulletin', Bi. Lydia Churi akizungumza jambo katika mafunzo hayo.

Sehemu ya Wajumbe wa Bodi ya Uhariri wa Jarida la 'Haki Bulletin' wakiwa katika Mafunzo hayo.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Charles Magesa akitoa neno la utangulizi. Mhe. Magesa, amesema kuwa Bodi ya Wahariri ya Jarida la ‘Haki Bulletin’ ina Wajumbe nane (8) wenye ujuzi tofauti tofauti na kwamba Jarida hilo linalenga kuuhabarisha umma shughuli na maboresho mbalimbali yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania. 
Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Victor Bigambo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) akizungumza jambo katika mafunzo hayo.
Mmoja wa Wawezeshaji wa Mafunzo ambaye ni Meneja Mawasiliano kutoka 'EWURA' Bw. Titus Kaguo akitoa Mada kwa Wajumbe wa Bodi ya Uhariri inayohusu Mambo muhimu ya kuzingatia katika Uandishi na Uhariri wa habari na makala.
Picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Uhariri ya Jarida la Mahakama ya Tanzania lijulikanalo kama 'Haki Bulletin'. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhe. Dkt John Utamwa ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Iringa.
Picha za pamoja kati ya Wajumbe wa Bodi ya Uhariri na baadhi ya Watumishi /Mahakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Lushoto.
Picha ya pamoja na baadhi ya Wawezeshaji wa Mafunzo hayo, wa kwanza kushoto ni Bw. Titus Kagua ambaye ni Meneja Mawasiliano wa 'EWURA' na kulia Bw. Oni Sigalla, Mhariri Mwandamizi wa Kiswahili kutoka Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA).






 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni