Jumatano, 27 Oktoba 2021

RAIS SAMIA KUZINDUA KITABU CHA MWONGOZO WA MASHAURI KWA MAJAJI NA MAHAKIMU

 Na Lydia Churi- Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kesho Oktoba 28, 2021 anatarajiwa kuzindua Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kuhusu mashauri ya ukatili wa kijinsia. 

Uzinduzi wa Kitabu hicho, ‘The Gender Bench Book’ chenye sura sita utafanyika katika hafla fupi itakayofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanachama kutoka Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA). 

Kitabu hicho kimeandaliwa ili kuwaongezea uwezo Majaji na Mahakimu na wadau wengine wa sheria kutoa haki kwa kuzingatia jinsia kwa watanzania, hususan wanawake na watoto. Ingawa mafunzo kadhaa ya utoaji wa haki kwa kuzingatia masuala ya kijinsia yametolewa kwa maofisa wa Mahakama, imeonekana kuna umuhimu wa kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa manufaa ya wanawake na watoto.

Hivyo, Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri ya Jinsia kwa Majaji na Mahakimu kitawaongezea ujuzi maofisa wa Mahakama juu ya namna ya kuzingatia mienendo bora ya ndani ya nchi na ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mapendekezo ya kamati huru za wataalamu wanaofanya tathimini ya utekelezaji wa Mikataba mbalimbali ya Kimataifa (Treaty Bodies) kama vile Kamati ya Kutokomeza Unyanyasaji wa Wanawake  (The Committee on the Elimination of Discrimination Against Women- CEDAW Committee) kuhusu kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wanawake.

 Inaelezwa kuwa lengo kuu la Kitabu cha Mwongozo wa Mashauri ya Jinsia kwa Majaji na Mahakimu ni kufuata vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara. Katiba inaipa Mahakama jukumu la kutafsiri sheria na kulinda haki za watu wote.

Kitabu hicho pia kinagusia nyaraka mbalimbali (Conventions) za kimataifa na kikanda zinazohusu haki za wanawake na watoto. Hivyo, ni nyenzo ya kuongeza, kupanua na kuimarisha uelewa wa viwango vya kimataifa na kikanda kuhusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na namna zinavyotafsiriwa, kujumuishwa na kutumika katika muktadha wa kitaifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na baadhi ya wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) miaka kadhaa iliyopita mjini Zanzibar (Picha kwa hisani ya TAWJA)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni