Na Mary Gwera, Mahakama-Mugumu-Serengeti
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma anaendelea na ziara yake ya kikazi Mahakama Kanda ya Musoma ikiwa leo tarehe 27 Oktoba, 2021 ni siku ya pili ya ziara hiyo ambapo ametembelea jengo la Mahakama ya Mwanzo Robanda-Serengeti, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Serengeti pamoja na kuzungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti.
Akiwa Mahakama ya Mwanzo Robanda, Jaji Mkuu, Prof. Juma alipokea taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama hiyo kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Akinyi Mlowa ambaye katika taarifa yake amebainisha kuwa Mahakama hiyo haina mlundikano wa mashauri.
“Mhe. Jaji Mkuu kama inavyofahamika jukumu kuu la Mahakama ni utoaji wa haki, Mahakama ya Mwanzo Robanda kwa mwaka 2020 hatukuvuka na mashauri, na kuanzia Januari mpaka Septemba 2021 tumesajili mashauri 17 ambapo mchanganuo wake ni kama ifuatavyo Mashauri ya jinai ni Matano (5), Mashauri ya madai ni manne (4), Mashauri ya talaka ni manne (4), Mashauri ya Mirathi ni manne (4), Rufaa kutoka Baraza la Kata ni sifuri (0), hakuna mashauri yanayoendelea,” alisema Mhe. Mlowa.
Aidha, Mhe. Mlowa alibainisha kuwa licha ya mafanikio ya uondoshaji wa mashauri, Mahakama hiyo inakabiliwa na upungufu wa Watumishi huku akieleza kuwa kwa sasa wapo Watumishi wawili tu ambao ni yeye pamoja na Mlinzi mmoja (1).
Akizungumza katika Mahakama hiyo mara baada ya kupokea Taarifa, Mhe. Prof. Juma aliahidi kushughulikia changamoto ya uhaba wa Watumishi katika Mahakama hiyo.
Hali kadhalika, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma alipata fursa ya kukagua jengo hilo la Mahakama ya Mwanzo Robanda ambapo mara baada ya ukaguzi alifika kuonana na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti kwa salaam na kueleza lengo la ziara yake katika Kanda ya Musoma.
Katika hatua nyingine, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amefanya mazungumzo na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti ambapo amewataka kuendelea kufanya kazi kwa kutumia TEHAMA kwa kuwa ndipo dunia ilipo.
Aliongeza kwa kuwataka Watumishi hao kuzingatia masharti yote muhimu ya kujikinga na Ugongwa wa Uviko 19 huku akiwashauri pia kuchanja.
Katika siku ya tatu ya ziara yake ambayo ni kesho tarehe 28 Oktoba 2021, Mhe. Prof. Juma atatembelea Mahakama ya Wilaya Tarime na Rorya ambapo atazungumza pia na Watumishi wa Mahakama hizo. Ziara yake itafikia ukingoni tarehe 29 Oktoba 2021 ambapo atafanya majumuisho kwa kuzungumza na Watumishi wote wa Mahakama Kanda ya Musoma.
Picha ya pamoja na Watumishi wa kada mbalimbali wa Mahakama ya Wilaya ya Serengeti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni