Alhamisi, 28 Oktoba 2021

UBORESHAJI MIUNDOMBINU YA MAHAKAMA WAPAMBA MOTO

Na Faustine Kapama na Mary Gwera, Mahakama-Tarime

Mahakama ya Tanzania imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Mahakama za Wilaya 19 katika maeneo mbalimbali nchini ili kusogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.

Akizungumza na Wakuu wa Wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara pamoja na watumishi wa Mahakama katika ziara yake ya kikazi leo tarehe 28 Oktoba, 2021, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe, Prof. Ibrahim Hamis Juma alibainisha kuwa Mahakama imetayarisha ramani ya nchi nzima pamoja na mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya miundombinu ambao umeainisha maeneo yote ya Tanzania ambayo yana changamoto za Mahakama katika ngazi mbalimbali.

“Tunajaribu kuweka ratiba ya kutekeleza mpango huo. Kwenye mpango huo utakuta Wilaya ya Rorya haina jengo na imewekewa ratiba ni lini lazima ipate jengo ndani ya miaka mitano, Wilaya ya Tarime wanasema jengo ni chakavu, linahitaji ukarabati mkubwa, Serengeti tumejionea wenyewe, ni chakavu na ni finyu na sio jengo ambalo linakidhi mahitaji ya Wilaya. Kwa hiyo tumeweza kutayarisha hata gharama za ujenzi. Kwa mfano, tukipata fedha leo tunajua tunaweza kutumia wapi  na kujenga wapi,” amesema.

Kwa mujibu wa Mhe. Prof. Juma, malengo ya Mahakama ya Tanzania ni kila Wilaya kuwa na Mahakama ya Wilaya na kwamba kila Tarafa iwe na Mahakama ya Mwanzo,  mpango ambao watajadiliana na Serikali Kuu ili kuona ni kwa namna gani  wanaweza kusogeza huduma za Mahakama hizo katika maeneo hayo na huenda siku moja miaka 20 au 30 ijayo kila Kata itakuwa na Mahakama ya Mwanzo, lengo hasa ni kusogeza  huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi.

Akijibu taarifa iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Jaji Mkuu alisema kuwa ni kweli Wilaya ya Tarime bado inahudumia Wilaya ya Rorya katika ngazi ya Mahakama ya Wilaya, lakini taarifa nzuri zilizopo zinaonesha tayari ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Rorya umeshaanza na sio Wilaya ya Rorya tu pamoja na Wilaya zingine 18 na kwa mujibu wa ramani iliyopo, ifikapo June mwaka ujao majengo hayo yawe tayari yamekamilika ili kusiwe na Wilaya ambayo haina Mahakama za Wilaya.

Kwa hiyo, Mhe. Prof. Juma aliwahakikishia wananchi wa Rorya alipokutana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Juma Chikoka kuwa huduma za Mahakama ya Wilaya zitawafikia hivi karibuni na hali waliyokuwa nayo haitakuwepo tena.  Mkuu wa Wilaya hiyo alimshukuru Jaji Mkuu na uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla kwa uamuzi walioufanya wa kujenga Mahakama ya kisasa, ambayo itasaidia katika kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Awali, akitoa taarifa fupi ya Wilaya yake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime aliupongeza Mhimili wa Mahakama nchini kwa juhudi kubwa za kuondosha mashauri na kutoa hukumu kwa wakati, jambo ambalo limepunguza mlundikano wa mashauri hayo pamoja na malalamiko kwa wananchi. Hata hivyo, Mhe. Kanali Mntenjele alibainisha baadhi ya changamoto ambazo anaamini zikipatiwa ufumbuzi zitaharakisha utoaji wa haki kwa haraka kwa wananchi.

Baadhi ya changamoto hizo ni Mahakama ya Wilaya ya Tarime kuhudumia pia Wilaya ya Rorya, kitendo ambacho kinaweza kusababisha mlundikano wa mashauri na ucheleweshaji, uchache wa Mahakama za Mwanzo, jambo ambalo husababisha wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma ya Mahakama na uwepo wa mlundikano wa mashauri.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya hiyo aliwasilisha ombi kwa Jaji Mkuu ili kuona namna ya kuharakisha usikilizaji wa mashauri yanayohusu ujauzito kwa wananfunzi, ubakaji na ulawiti na kutolewa uamuzi kwa wakati kwani kuahirishwa mara kwa mara kunaweza kupoteza ushahidi na mashahidi.

Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu ameambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi ambaye amemwakilisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mahakama Kuu, Masijala Kuu, Bw. Samson Mashalla, ambaye amemwakilisha Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha’

Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Adrian Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Mhe. Jovin Constantine na Afisa Utumishi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Juni Mdede.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. John Kahyoza, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mhe. Frank Moshi ambaye pia ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda, Bw.  Festo Chonya na Afisa Utumishi, Bi. Francisca Swai.

Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma anatarajia kukamilisha ziara yake ya kikazi kesho tarehe 29. 10.2021 ambapo atafanya ukaguzi katika Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na hatimaye kuhitimisha kwa kufanya majumuisho ya ziara hiyo.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe, Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akionyeshwa eneo la Kiwanja ambapo linajengwa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Rorya leo tarehe 28 Oktoba 2021 alipotembelea eneo hilo akiwa katika ziara ya kikazi. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mhe. Juma Chikoka.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe, Prof. Ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na  Mkuu wa Wilaya ya Tarime na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Mntenjele na baadhi ya Viongozi wengine wa Wilaya hiyo na Maafisa wa Mahakama walioambatana nae (hawapo katika picha).
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime,
Kanali Michael Mntenjele na baadhi ya Viongozi wengine wa Wilaya hiyo na Maafisa wa Mahakama walioambatana nae.
Mhe. Jaji Prof. Juma akizungumza jambo mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini.
Jaji Mkuu, Prof. Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Tarime Mjini. Walioketi kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza na kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.
Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime na baadhi ya Maafisa wa Mahakama kutoka Makao Makuu na Mahakama Kuu Musoma wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) wakati akizungumza nao alipotembelea Mahakama hiyo leo tarehe 28.10.2021.
Picha ya pamoja na Mahakimu Wakazi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime.
Picha ya pamoja na Makarani wa Mahakama ya Wilaya Tarime-Mara.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Muhsusi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime, Aliyeketi kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Mahimbali.
Picha ya pamoja na Wasaidizi wa Ofisi wa Mahakama ya Wilaya ya Tarime.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama- Tarime)
 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni