Na Lydia Churi- Mahakama
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Majaji na Mahakimu
nchini kutumia kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kuhusu mashauri
yanayohusu ukatili wa kijinsia kama moja ya miongozo katika usikilizaji wa mashauri
ya aina hiyo.
Rais Samia amezindua
kitabu hicho ‘The Tanzania Gender Bench Book on Women’s Rights’ jana
katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam kilichoandaliwa na Chama cha
Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) kwa ufadhili wa Shirika la Umoja
wa Mataifa linalojishughulisha na masuala wanawake UN Women na Ubalozi wa Sweeden nchini.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Rais Samia amesema kitabu hicho kitawapa Majaji na Mahakimu wanaosikiliza
mashauri yanayohusu ukatili wa kijinsia ujasiri wa kutoa uamuzi wa mashauri hayo
ambao pia utawezesha kuachwa kwa mila, desturi na imani potofu zinazokandamiza
na kupora haki za makundi maalumu katika
jamii ya watanzania.
“Katika kipindi cha
Uongozi wangu nitahakikisha ninajenga nchi inayozingatia na kuheshimu misingi
ya utawala wa sheria, haki za binadamu, na utawala bora kwa maendeleo ya nchi kiuchumi,
kisiasa na kijamii”, alisema Rais Samia.
Aidha, Mhe. Samia
amewapongeza wanachama wa TAWJA kwa kutayarisha kitabu hicho kinachotoa
mwongozo wa namna bora ya kulinda haki za Wanawake Watoto ikiwa ni pamoja na
kuimarisha utawala wa sheria nchini.
Rais Samia pia
amewaomba wanachama wa TAWJA pamoja na wadau wengine walioshiriki katika
kuandaa kitabu hicho kukitafsiri kwa lugha ya Kiswahili kinachoeleweka vizuri ili
kieleweke zaidi kwa wale wote wanaojishughulisha na suala la utoaji haki.
Kuhusu matumizi ya
lugha ya Kiswahili mahakamani, Mhe. Samia ameishauri Mahakama ya Tanzania
kutumia lugha hiyo katika kuandika hukumu kwa kuwa tayari Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania limeshafanya marekebisho ya sheria kuruhusu matumizi ya
lugha ya kiwswahili katika kuandika hukumu pamoja na nyaraka nyingine muhimu za
kimahakama.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizindua kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kuhusu mashauri ya Ukatili wa Kijinsia Ikulu jijini Dar es salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha Mwongozo wa Mashauri kwa Majaji na Mahakimu kuhusu mashauri ya Ukatili wa Kijinsia Ikulu jijini Dar es salaam. Jaji Siyani alimuwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye hafla hiyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello akizungumza kwenye hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni