Na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis amehitimisha ziara yake ya kikazi tarehe 29 Oktoba 2021 ndani ya Mahakama Kanda ya Musoma huku akiwataka Viongozi wa Mahakama kushughulikia kero mbalimbali za Watumishi zilizoibuliwa katika kipindi cha ziara yake.
Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika Kanda hiyo, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Juma alisema kuwa kumekuwa na mwenendo wa baadhi ya Viongozi kuishia kuahidi kutatua kero za watumishi na baadae kutofanyia kazi malalamiko mbalimbali ya Watumishi hao yanayowasilishwa katika nyakati mbalimbali.
“Baada ya ziara yangu, nimegundua kuwa Kanda ya Musoma inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa watumishi, changamoto ya baadhi ya majengo duni kwa baadhi ya maeneo, baadhi ya watumishi kutopandishwa vyeo kwa muda mrefu, hivyo ni rai yangu kuwa yale yote yaliyowasilishwa na Watumishi yafanyiwe kazi ikiwemo kujibu barua za kumjulisha mtumishi mwenye kero yake kuhusu hatua iliyofikiwa katika utatuzi wa changamoto yake,” alisema Jaji Mkuu.
Akizungumzia kuhusu mpango wa ujenzi wa majengo ya Miundombinu ya Mahakama, Jaji Mkuu, Prof. Juma alieleza kuwa Mipango inayowekwa hususani ya ujenzi wa Mahakama nchini lazima iwe na uhalisia kwa kuainisha maeneo yenye uhitaji halisi wa ujenzi na ukarabati wa Mahakama.
Aliongeza pia kuomba ushirikiano wa wananchi na mamlaka husika kuunga mkono jitihada za Mahakama za kusogeza karibu huduma za utoaji haki karibu na wananchi kwa kutopandisha bei za viwanja/maeneo yanayonunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama.
Katika siku nne (4) za ziara yake ambayo ilianza tarehe 26 Oktoba 2021, Mhe. Prof. Juma alitembelea Mahakama ya Mwanzo Kukirango-Butiama, kukagua ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Butiama, kutembelea na kuzungumza na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda, Mahakama ya Mwanzo Robanda, Mahakama ya Wilaya ya Serengeti, Tarime, Rorya.
Mhe. Jaji Mkuu alikagua na kupokea taarifa za Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Wilaya Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na hatimaye kuhitimisha ziara yake kwa kukagua jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Musoma na kuzungumza na Watumishi wa Kanda hiyo.
Katika mazungumzo na Watumishi hao, Jaji Mkuu Prof. Juma alimpongeza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma pamoja na watumishi wote wa Kanda hiyo kwa kulitunza vyema jengo la Mahakama hiyo lililoanza kutumika miaka miwili iliyopita na kusema kuwa jengo hilo bado lipo katika hali nzuri licha ya kutumika kwa muda.
“Napenda kuwapongeza kwa dhati kwa utunzaji mzuri wa jengo ambalo kwakweli linapendeza, na ninafikiri hili pia ni eneo zuri kwa Watumishi wa Mahakama nyingine kuja kujifunza kupitia ninyi,” alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma mara baada ya kuzungumza nao wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi katika Kanda hiyo leo tarehe 29, Oktoba 2021. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. Ephery Kisanya, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma (hawapo katika picha) wakati wa mazungumzo ya kuhitimisha ziara yake ya siku nne katika Kanda hiyo.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama kutoka Makao Makuu (walioketi mstari wa mbele) walioambatana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu (hayupo katika picha) alipokuwa akizungumza nao katika Mkutano wa Majumuisho ya ziara yake.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (aliyesimama) akizungumza jambo na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma (hawapo katika picha). Katikati ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Bw. Solanus Nyimbi ambaye pia alimwakilisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu-Masjala Kuu, Bw. Samson Mashalla. anayemwakilisha Mtendaji wa Mahakama Kuu, Bw. Leonard Magacha.
Ukaguzi wa jengo la Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Musoma)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni