Jumamosi, 30 Oktoba 2021

JAJI MKUU AMALIZA ZIARA KANDA YA MUSOMA NA KUTEMA CHECHE

 Na Faustine Kapama na Mary Gwera, Mahakama-Musoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Ibrahim Hamis Juma amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku nne ya Mahakama, Kanda ya Musoma kwa kutembelea Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Mahakama ya Wilaya na Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma kabla ya kuongea na watumishi wa Kanda hiyo kwenye kikao cha majumuisho na kuahidi kuchukua hatua kadhaa ili kurahisisha utoaji wa haki nchini.

Baadhi ya hatua hizo ni kuimarisha miundombinu ya Mahakama katika ngazi zote ikiwemo majengo na mfumo wa TEHAMA na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi kwa lengo la kuimarisha maslahi yao. Mhe. Prof. Juma pia aliwataka watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uaminifu na kutokuchelewesha haki kwa wananchi.

Akiwa katika Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini, Jaji MKuu alipokea taarifa ya utendaji kutoka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Prisia Mkeha inayoonesha Mahakama hiyo inavyohudumia wakazi wa kata 16 ambazo ni Kitaji, Mkendo, Mwigobero, Mwisenge, Makoko, Buhare, Kamunyonge, Nyasho, Nyakato, Mshikamano, Rwamlimi, Bweri, Kwangwa, Kigera, Iringo na Nyamatare.

Mhe. Mkeha alieleza kuwa pamoja na kuhudumia kata hizo, Mahakama yake inakabiliwa na upungufu wa watumishi ambapo mahitaji halisi ni 15, waliopo ni wanane, hivyo upungufu ni watumishi saba wa kada mbalimbali. Kuhusu hali ya mashauri, Hakimu Mfawidhi alimweza Jaji Mkuu kuwa mashauri yaliyobaki mwaka 2020 yalikuwa 139, mashauri 138 yameshasikilizwa na kumalizika na kuna shauri moja tu la mwaka 2020 ambalo ndio lililopo kwenye mlundikano. Alibainisha pia kuwa mashauri yaliyopokelewa na kusikilizwa kuanzia Januari mpaka Septemba 2021 yalikuwa 1,048, yaliyosikilizwa yapo 934 na mashauri yaliyobaki ni 114.

Kabla ya kutembelea Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Mhe. Prof. Juma alikutana na Mkuu wa Wilaya hiyo katika Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Dkt. Arufani Haule ambaye aliupongeza uongozi wa Mahakama kwa juhudi unazofanya katika kuimarisha mfumo wa utoaji wa haki kwa wananchi. Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alimfahamisha Jaji Mkuu kuwa Mahakama ya Mwanzo Musoma Mjini ndiyo Mahakama pekee inayohudumia Wilaya hiyo. Kwa kuzingatia wingi wa mashauri, idadi ya watu na matukio katika Wilaya, Dkt. Haule aliuomba Mhimili huo kuona uwezekano wa kupata Mahakama nyingine ya Mwanzo ili kupunguza mlundikano wa mashauri katika eneo moja.

Akiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Mhe. Prof. Juma alipokea taarifa ya utendaji iliyowasilikwa kwake na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Tumaini Marwa inayoonesha mashauri yaliyobaki mwezi Disemba 2020 yalikuwa 372, yaliyofunguliwa kati ya Januari na Septemba 2021 yalikuwa 2,581, mashauri yaliyoamuliwa katika kipindi hicho yalikuwa 2,545 na yaliyobaki ni 408.

Mhe. Marwa alibainisha pia kuwa hali ya uhuishaji wa mashauri katika mfumo wa JSDS II ni nzuri ambapo katika kipindi hicho jumla ya mashauri 417, sawa na asilimia 100 ya mashauri yote yaliyofunguliwa yaliingizwa katika mfumo huu. Aidha, kwa upande wa Mahakama za mwanzo, jumla ya mashauri 2,164 sawa na asilimia 100 ya mashauri yote yaliyofunguliwa katika kipindi hicho, yaliingizwa katika mfumo wa JSDS.

Baadaye, Jaji Mkuu alitembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma ambapo Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Frank Moshi ambaye pia ni Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, alitoa taarifa ya utendaji inayobainisha kuwa Mahakama hiyo inasimamia Mahakama za Wilaya sita ambapo kati ya hizo nne (Bunda, Tarime, Serengeti na Musoma) zinafanya kazi na mbili (Rorya na Butiama) zinasimamiwa na Wilaya mama za Tarime na Musoma. Aidha Mahakama za Mwanzo zipo 30 (zinazofanya kazi 28 na zisizofanya kazi ni mbili).

Katika taarifa yake, Mhe. Moshi alimweleza Jaji Mkuu, pamoja na mambo mengine, kuwa hadi kufikia mwezi Septemba 2021, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma ilikuwa na jumla ya watumishi 18, wakati mahitaji halisi ni watumishi 23 hivyo kuna upungufu wa watumishi watano. Alibainisha pia kuwa hali ya nidhamu ya watumishi ni ya kuridhisha, na katika kipindi cha mwezi Januari 2021 hadi Septemba 2021, hakuna mtumishi aliyepatikana na kosa la kukiuka maadili ya utumishi wa umma.

Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mhe. Prof. Juma alielekea Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma ambapo alifanya ukaguzi wa jengo jipya na la kisasa kabisa la karne ya 21 na kuwapongeza watumishi wote wa Mahakama hiyo, wakiongozwa na Jaji Mfawidhi, Mhe. John Kahyoza na Mtendaji wa Mahakama Kanda, Bw. Festo Chonya kwa kuendelea kulitunza na kuhifadhi mazingira katika eneo hilo. Baadaye alipokea taarifa ya utendaji wa miaka miwili wa Kanda hiyo iliyowasilishwa kwake na Jaji Mfawidhi.

Katika taarifa yake iliyosheheni mambo mengi, Mhe. Kahyoza alieleza kuwa katika kipindi cha Julai 2019 hadi Septemba 2021, majukumu mbalimbali ya usikilizwaji wa mashauri na uendeshaji wa ofisi yametekelezwa kwa kiasi kikubwa na katika kiwango cha kuridhisha. Alisema kuwa Julai 2019, Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ilikuwa na jumla ya watumishi 175 na hadi kufikia mwezi Septemba 2021, ilikuwa na jumla ya watumishi 199. Pamoja na idadi hiyo, Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa mahitaji halisi ni watumishi 366, hivyo kuna upungufu wa watumishi 167 sawa na asilimia 45.62.

Kuhusu hali ya mashauri katika ngazi ya Mahakama Kuu, Mhe. Kahyoza alieleza kuwa kipindi cha Mwaka 2020 walivuka na jumla ya mashauri 326, yalifunguliwa yalikuwa 1,122 na yaliyoamuliwa ni 1, 074 ambapo mashauri yaliyobaki yalikuwa 374 na kufanya “Clearance rate” kuwa wastani wa asilimia 95. Taarifa yake inaonesha pia kuwa kwa Mwaka 2021, Mahakama Kuu ilianza na mashauri 374 na hadi kufikia tarehe 18 October, 2021 yamefunguliwa jumla ya mashauri 824, yaliyoamuliwa ni 722 na yamebaki mashauri 476.  

Kuhusu Vikao vya mashauri ya Mahakama Kuu, Mhe. Kahyoza alimweleza Jaji Mkuu kuwa katika kipindi cha mwezi January hadi August 2021 vikao sita (6) kati ya vikao tisa (9) vilivyopangwa kwa Kalenda ya mwaka 2021 vimefanyika. Ameeleza kuwa vikao vimefanyika kama vilivyopangwa kwa mafanikio makubwa ambapo kati ya mashauri 96 yote yaliyokuwa yamepangwa kusikilizwa, ni mashauri mawili tu yaliyobaki kutokana na sababu za msingi na za kisheria ambapo iliamuriwa Mahabusu kwenda katika Taasisi ya Isanga Dodoma kwa ajili ya uchunguzi.

Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu aliambatana na viongozi mbalimbali kutoka Makao Makuu, wakiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi ambaye amemwakilisha Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mahakama Kuu, Masijala Kuu, Bw. Samson Mashalla, ambaye amemwakilisha Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha’

Wengine ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama, Malalamiko na Maadili, Mhe. Annah Magutu, Mkurugenzi Msaidizi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Machumu Essaba, Katibu wa Jaji Mkuu Adrian Kilimi, Katibu wa Msajili Mkuu, Bw. Jovin Constantine na Afisa Utumishi, Mahakama ya Tanzania, Bw. Juni Mdede.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, yupo Jaji Mfawidhi, Mhe. John Kahyoza, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mhe. Frank Moshi, ambaye pia ni Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo, Mtendaji wa Mahakama Kuu wa Kanda, Bw.  Festo Chonya na Afisa Utumishi, Bi. Francisca Swai.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma  (wa kwanza kulia) akiwasili Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma alipowasili kukagua Mahakama hiyo katika siku ya mwisho ya ziara yake.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma (waliosimama), wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. Ephery Kisanya, wa pili kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo katika Mahakama ya Mwanzo, Mhe. Dkt. Arufani Haule na wa kwanza kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma  (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Musoma mara baada ya kuzungumza nao wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi katika Kanda hiyo leo tarehe 29, Oktoba 2021. Wa pili kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza, wa pili kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. Ephery Kisanya, wa kwanza kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani, Bw. Solanus Nyimbi na wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Musoma) 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni