Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Omar
Othman Makungu ametoa wito kwa Watendaji wa Mahakama ya Tanzania kuendelea kushirikiana
na Mahakama Kuu Zanzibar katika suala la
utoaji haki ili wananchi waweze kupata haki kwa wakati.
Jaji Makungu ameyasema hayo leo alipokuwa katika ziara
yake kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji jijini Dodoma yenye lengo la kujifunza
kuhusu uendeshwaji wa vituo hivyo na pia kujionea maendeleo makubwa yaliyofikiwa
na Mahakama ya Tanzania katika uboreshaji wa huduma zake kwa wananchi.
Katika ziara hiyo, Jaji Makungu aliambatana na
Viongozi wa Mahakama Kuu Zanzibar akiwemo Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe.
Mohamed Ali Mohamed na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu Zanzibar Bw. Kai Mbaruk.
“Tukiwa na ushirikiano
mzuri mambo yatakwenda vizuri, wananchi watapata haki kwa wakati na watakuwa na
imani na Mahakama”, alisisitiza Mhe. Makungu.
Kiongozi huyo ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa mafanikio
makubwa iliyopata baada ya kukamilisha ujenzi wa majengo sita ya Vituo Jumuishi
vya Utoaji haki na kuongeza kuwa hatua hiyo itaharakisha usikilizwaji wa
mashauri mahakamani. Ametoa wito kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania kuyatunza
majengo hayo mapya na ya kisasa ili yaweze kudumu na kutumika kama
ilivyokusudiwa.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Abdi Kagomba amesisitiza kuimarishwa kwa ushirikiano
kati ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama Kuu Zanzibar katika suala zima la
utoaji haki. “Mahakama si ya Muungano japokuwa tunakutana na Zanzibar kwenye
Mahakama ya Rufani lakini utoaji haki ni suala la Muungano”, alisema.
Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel ameishauri Mahakama Kuu
Zanzibar kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika eneo la kubadilishana
uzoefu wa kazi kwa watendaji wa Mahakama kutoka pande zote mbili. “Nashauri ikiwezekana
chukueni baadhi ya watumishi Zanzibar waje kupata uzoefu huku ili ushirikiano
uwe imara zaidi, utakuwa ni ushirikiano wa vitendo zaidi”, alisema.
Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alizindua vituo sita Jumuishi vya Utoaji haki vilivyojengwa katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Dodoma, Morogoro na Dar es salaam katika wilaya za Kinondoni na Temeke.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Leonard Magacha akielezea jambo mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Omar Othman Makungu (mwenye suti nyeusi) pamoja na Viongozi wengine wa Mahakama Kuu Zanzibar na Mahakama ya Tanzania walipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki jijini Dodoma leo.Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akimuelezea jambo Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Omar Othman Makungu alipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki leo jijini Dodoma.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania na wa Mahakama Kuu Zanzibar wakifurahia jambo
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Omar Othman Makungu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama ya Tanzania pamoja na Mahakama Kuu Zanzibar. Wa pili kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Abdi Kagomba na wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel. Kushoto ni Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar Mhe. Mohamed Ali Mohamed na kulia ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama Kuu Zanzibar Bw. Kai Mbaruk.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Omar Othman Makungu akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma.
Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Omar Othman Makungu akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma wakiwemo Naibu Msajili, Mtendaji na Mahakimu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni