Na Faustine Kapama, Mahakama
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. George Masaju amewataka watumishi waliochaguliwa kuhudumu katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma kufanya kazi kwa weledi na kwa wakati bila kuangalia sura na muonekano wa mtu ili huduma watakayotoa iwe bora kwa wananchi wote inayoakisi mazingira mazuri yanayowazunguka.
Mhe. Masaju alitoa wito huo tarehe 1 Novemba, 2021 alipokuwa akifungua mafunzo kwa watumishi 110 wa Mahakama ya Tanzania waliopangiwa kufanya kazi katika Kituo hicho Jumuishi jijini Dodoma na kusistiza kuwa huduma za kimahakama zitolewe kwa wakati kama ilivyo kauli mbiu ya Mahakama ya Tanzania inayosisitiza kutoa haki kwa wakati na kwa watu wote.
“Nyinyi ni miongoni mwa watumishi wachache sana ambao mmepitia katika mchakato mrefu wa kuwapata kwa kuangalia vigezo maalumu ambavyo Mahakama inatarajia na kuwa na matumaini kwenu ya kutoa huduma bora katika kituo hiki jumuishi. Tambueni kwamba katika kituo hiki mnapaswa kufanya kazi kwa weledi na kutoa huduma bora na kwa wakati, hivyo msiangalie sura au muonekano wa mtu, mfano mtu amevaa suti ndiyo anayepaswa kuhudumiwa haraka” alisema.
Kaimu Jaji Mfawidhi huyo amebainisha kuwa Mahakama ya Tanzania imekamilisha awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2014/2015-2020/2021) chini ya ufadhili wa Benki ya Dunia, ambao matunda yake ni uboreshaji mkubwa ya miundombinu ya Mahakama, masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, mafunzo mbalimbali ya muda mfupi na mrefu na mambo mengine mengi.
Amesema kuwa katika mpango mkakati wa Mahakama, moja ya malengo makuu ni kupeleka huduma karibu kwa wananchi. Kwa msingi huo, Mhe. Masaju alibainisha kuwa vimejengwa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki Dodoma, Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Arusha, Morogoro na Mwanza ambavyo malengo yake ni kutoa huduma za kimahakama katika ngazi zote katika jengo moja.
Aidha, Kaimu Jaji Mfawidhi huyo alisema pia kuwa mafunzo kwa watumishi walioko makazini (On the job training) ni moja ya mkakati wa Mahakama ya Tanzania katika kuwajengea uwezo watumishi ili wapate ujuzi na maarifa yatakayoboresha utendaji kazi na kuleta tija kama ambavyo dira ya Mahakama ya Tanzania inayosema kuhusu utoaji wa haki kwa wakati na kwa watu wote.
“Naomba mtambue kwamba hii imekuwa nafasi ya pekee ambapo tumeweza kukutana kwa ajili ya mafunzo kwa watumishi wote ambao wamepangwa kufanya kazi katika Kituo Jumuishi. Hii ni nafasi adhimu ambayo itawafanya washiriki wote wa mafunzo haya kutoa huduma zilizo bora kwa kiwango cha juu ili kumfanya mwananchi aweze kufurahia huduma zetu,” alisema.
Mhe. Masaju aliongeza kwa kusema, “Haitakuwa na maana yoyote kufanyia kazi katika majengo mazuri namna hii na ya kisasa, halafu huduma zetu zikawa zinalalamikiwa na wateja wetu na wananchi kwa ujumla.Sote tunapaswa kuiunga mkono Serikali yetu na Mahakama kwa ujumla kwa uboreshaji unaofanyika kote nchini. Uboreshaji huu ulete sura halisi kuanzia majengo na hata sisi watumishi wote.”
Akimnukuu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika nasaha alizozitoa kwenye Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania hivi karibuni, Jaji Masaju aliwaabia watumishi hao kuwa wafanyakazi ni lazima waelimishwe kuhusu mwelekeo ambao utabadili namna ya kufanya kazi katika Mahakama Mtandao (E-Judiciary).
Amesema kuwa nukuu hiyo ni kiashiria kwamba Mahakama ya Tanzania inakoelekea italazimisha watumishi kubadilika katika utendaji wao wa kazi kwa kutumia teknolojia ili kwenda na mabadiliko ya Dunia, hivyo katika mafunzo hayo watumishi watafundishwa juu ya kutumia mifumo mbalimbali ya kielektroniki.
“Tutalazimika kufanya kazi tofauti na tunavyofanya sasa hivi. Kwa sasa Mahakama ya Tanzania tunatumia TEHAMA kwa kiasi kidogo sana. Safari ya Mahakama ya Tanzania ni kufikia Mahakama Mtandao katika ngazi zake zote za utoaji haki na shughuli zote za kimahakama. Kwa msingi huo,mafunzo kama haya ni muhimu sana katika kuwajengea watumishi uwezo na uelewa zaidi,”amesema.
Mhe. Masaju alimshukuru Jaji Mkuu wa Tanzania na timu yake kwa kuweka utaratibu huo mzuri wa mafunzo kwa watumishi katika Kituo hicho jumuishi. Hali kadhalika, aliishukuru timu ya wawezeshaji na waandaaji wa mafunzo hayo ambayo yataleta manufaa makubwa kwa washiriki wote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni