Alhamisi, 4 Novemba 2021

WADAU WA MAHAKAMA KANDA YA MOROGORO WAKABIDHIWA OFISI KWENYE KITUO JUMUISHI

 Na Evelina Odemba-Morogoro

Wadau wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro wamekabidhiwa ofisi zao zilizopo ndani ya Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, huku Serikali ya Mkoa huo ikiahidi kuendelea kuheshimu uamuzi unaotolewa na Mahakama na kutoa ushirikiano wa dhati ili Mhimili huo wa dola uweze kutekeleza majukumu yake ya utoaji haki kikamilifu kwa wananchi.

Hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika tarehe 3 Novemba, 2021 ilihudhuriwa  na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigela na kuwashirikisha wawakilishi wa wadau hao wakiwemo Polisi, Magereza, Takukuru, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na Maafisa Ustawi wa Jamii.

Akizungumza katika kikao baada ya makabidhiano hayo, Mhe. Shigela aliipongeza Serikali kwa kuwezesha huduma ya Kituo hicho kupatikana katika Mkoa huo na kuahidi kutoa ushirikiano pindi watakapohitajika, kuheshimu na kutoingilia uamuzi unaotolewa na Mahakama zote zilizopo mkoani kwake na kote nchini.

Mkuu wa Mkoa huyo pia aligusia suala la mrundikano wa mahabusu gerezani na kusema kuwa watafanya tathmini kujua shida iko wapi, kwani jambo hilo linatia hasara serikali kutokana na mahabusu hao kutofanya kazi yoyote ya kuingiza kipato huku wakihudumiwa kwa chakula na maradhi.

Awali, akizungumza katika kikao hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe aliwataka wadau wa Mahakama kuwa wakweli, kujenga ushirikiano wa hali ya juu na kuwajibika ipasavyo ili kupafanya mahakamani pawe mahali patakatifu. Amesema kuwa anatamani kila mmoja awajibike kwenye eneo lake la kazi, kutekeleza wajibu wake kwa wakati na kufanya kazi kitaalamu.

“Mambo yanayokwaza jamii na viongozi wa Mihimili ya dola ni kuona mahali pakutolea haki, badala ya kuwa patakatifu pamejaa ufisadi, rushwa, ubabaishaji, utapeli, lugha za njoo kesho zisizoisha na kusababisha mateso kwa jamii inayohitaji huduma ya haki. Mambo hayo hayavumiliki sio tu kwa watumishi wa Mahakama wa ngazi zote bali pia Polisi, Takukuru, Magereza na wadau wengine,” alisema.

Mhe. Ngwembe alisisitiza kuwa lugha za njoo kesho zikivumiliwa mahakamani hapatakuwa mahali salama, hivyo aliwataka wadau wote kufanya kazi kwa weledi na uaminifu ili kuifanya Mahakama kuwa kimbilio la wananchi. Jaji Mfawidhi huyo pia aliwataka Mawakili wote wanaokwenda mahakamani kuhudhuria mashauri yao kujiandaa kwa ajili ya kuyasikiliza na si vinginevyo, kwani kumekuwepo na tabia ya baadhi yao kwenda mahakamani kuomba mashauri yao kutajwa.

“Tunataka kuhakikisha haki inatendeka, lazima tujipange kutekeleza hayo,” alisema.  Akizungumzia suala la kufikisha elimu ya sheria kwa wananchi, Mhe. Ngwembe amesema kuwa wamekusudia kutumia Runinga na Redio zilizopo mkoani Morogoro ili kuwafikia wananchi wengi. Hivyo aliwaasa wadau wote wa sheria kutoa ushirikiano wa karibu mara watakapohitajika.

Wadau pia walipata nafasi ya kutembelea ofisi mbalimbali zilizopo ndani ya jengo la Kituo hicho, huku wakiongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro Mhe. Arnold Kilekiano ambaye alitoa ufafanuzi wa kila ofisi husika pamoja na matumizi yake.

Kituo hicho kilichojengwa Morogoro ni miongoni mwa majengo ya kisasa ya vituo sita vilivyozinduliwa kwa pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan jijini Dodoma tarehe 06 Oktoba, 2021. Kituo hiki Jumuishi cha Utoaji Haki kinajumuisha ofisi za Majaji wa Mahakama ya Rufani, masjala ya Mahakama Kuu, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Mwanzo na Mahakama ya Watoto.

Pia kuna Ofisi za wadau wa sheria ambazo ni, Magereza, Polisi, Ustawi wa Jamii, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea na ofisi ya msaada wa sheria. Pia kuna huduma mbalimbali ikiwemo chumba kwa ajili ya kunyonyeshea watoto.

Kuanzishwa kwa Mahakama Kuu, Kanda ya Morogoro kutampunguzia mwananchi adha ya usafiri na kutumia muda mrefu kutafuta huduma za utoaji haki, ambapo awali wananchi walilazimika kuifuata huduma hiyo mkoani Dar es Salaam, jambo ambalo limewagharimu kwa kipindi kirefu.

Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe Arnold Kilekiano (wa kwanza kushoto) akitolea ufafanuzi wa vyumba vya wadau wa Mahakama kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe Martin Shigela (wa kwanza kulia), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu kanda ya Morogoro Paul Ngwembe (wa pili kulia) pamoja na wadau wa Mahakama. Hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika tarehe 3 Novemba, 2021.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Martin Shigela (wa pili kulia) pamoja na Majaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro (walioketi upande wa kushoto) wakifuatilia kikao cha wadau kanda ya Morogoro kilichofanyika ndani ya ukumbi wa mkutano wa kituo hicho. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe. Wa kwanza kushoto ni Mhe. Messe Chaba, Jaji wa  Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Morogoro, wa pili kushoto ni Mhe. Said Kalunde, Jaji wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Morogoro.
 
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe Martin Shigela  akiongea na wadau wa Mahakama (hawapo katika picha)  wakati alipotembelea ofisi za Kituo Jumuisho cha Utoaji Haki Morogoro. Kushoto ni
Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe, wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Wakili Albert Msando na wa pili kulia ni Bw. Erasmus Uisso, Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji-Mahakama ya Tanzania.

 Baadhi ya wadau wa Mahakama wakifuatilia hotuba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe (hayupo katika picha).


 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni