Na Lydia
Churi- Mahakama
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert
Chuma ametoa wito kwa viongozi wa Mahakama kusimamia kikamilifu suala la
kukutana na wadau wa haki jinai na haki madai ili kuondoa mlundikano wa
mashauri mahakamani.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa
Mahakama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama ya Wilaya ya Maswa,
Mhe. Chuma aliwataka Viongozi hao kuweka msisitizo katika matumizi ya
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kurahisisha usikilizaji wa mashauri
hayo.
Aidha, Msajili Mkuu pia amewahimiza Viongozi wa
Mahakama kuendelea kutoa elimu kuhusu taratibu za kushughulikia mashauri
mbalimbali yanayosajiliwa mahakamani, hususani yale yanayohusu masuala ya
mirathi.
Amewataka viongozi hao kuwaelimisha watumishi wa
Mahakama taratibu mbalimbali na miundo ya kiutumishi ili waweze kufahamu haki
zao za msingi pamoja na majukumu yao katika utumishi. Alisema kuwa viongozi
hawana budi kuyapa kipaumbele maslahi ya watumishi wao.
Kuhusu suala la kuongeza ujuzi, Msajili Mkuu
amewashauri watumishi hao kujenga utamaduni wa kujiendeleza kielimu kupitia fursa
mbalimbali za muda mfupi na mrefu, hasa zile zinazotolewa na Chuo cha Uongozi
wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa njia ya mtandao ili kuongeza tija na ufanisi
katika kazi.
Katika juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO
19, Mhe. Chuma amewataka watumishi wote wa Mahakama kuchukua tahadhari na
kujikinga dhidi ya ugonjwa huo huku wakiendelea kuchapa kazi kwa bidii na kwa
ufanisi na kuwashauri wanaopenda kuchanjwa chanjo ya UVIKO 19 kufanya hivyo.
Msajili Mkuu alifanya ziara katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Simiyu pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Maswa kwa lengo la kukagua
utendaji kazi na utekelezaji wa shughuli za Mahakama. Katika ziara hiyo, Mhe.
Chuma pia alipata nafasi ya kukagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya
Busega unaoendelea.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akikagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Busega ulioanza hivi karibuni wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama mkoani Shinyanga.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akiangalia tofali wakati alipofanya ukaguzi katika mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Busega ulioanza hivi karibuni.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga Mhe. Seif Mwinshehe Kulita (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma (mbele kulia) na Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu mara baada ya kuzungumza nao hivi karibuni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni