Alhamisi, 4 Novemba 2021

JAJI WA TANZANIA AUNGURUMA KWENYE MKUTANO WA KIMATAIFA MAJAJI WAKUU AFRIKA

 Na Faustine Kapama-Mahakama

Jaji wa Mahakama ya Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Deo Nangela leo tarehe 04 Novemba, 2021 ameuhutubia Mkutano wa Kimataifa wa Majaji Wakuu kutoka Bara la Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya TEHAMA mahakamani katika kurahisisha utoaji wa haki kwa wananchi.

Akizungumza katika Mkutano huo wenye Mada Kuu inayosema, “Kujenga Imani kwa Mahakama za Afrika”, Dkt. Nangela, ambaye amemwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amesema kuwa ili kuwezesha ufanisi na utoaji haki kwa wananchi ni lazima uwekezaji katika matumizi ya TEHAMA  uonekane kama lengo linalohitaji kufikiwa kwa gharama yoyote ile kwa sababu uwazi  ni moja ya nguzo muhimu katika kujenga imani ndani ya Mahakama.

 “Kimsingi, uwazi ndani ya Mahakama hauhitaji tu kuchukua hatua bali pia ushirikishwaji makini kwa kupitia utaratibu wa huduma za kimahakama unaozingatia haki za wananchi,” amesema Jaji Nangela, ambaye ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel katika Mkutano huo.

Amesema kuwa aina hiyo ya utaratibu wa utoaji haki sio tu inachangia katika kuimarisha utawala wa sheria, lakini pia huimarisha mamlaka ya Mahakama na uwezekano kwa umma kuwa na mawazo chanya kuhusu maadili ya msingi na kazi zinazofanywa na Mahakama, ambazo huenda zisingefahamika kwa wengi.

Dkt. Nangela aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kuwa tangu mwaka 2007 Mahakama ya Tanzania iliona umuhimu wa kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za kimahakama, hivyo kufanya suala hilo kuwa jambo la kipaumbele.

Amesema kuwa 2007 ulikuwa mwaka wa kihistoria ambao ulishuhudia kuongezeka kwa juhudi hizo za mabadiliko, hasa wakati Mahakama ya Tanzania ilipoitisha mkutano jijini Arusha chini ya kaulimbu iliyokuwa inasema ‘Jukumu la TEHAMA katika Utawala’.

 “Mkutano wa Arusha wa 2007 ulimalizika kwa azimio la kushirikisha Mshauri ili kuandaa Mwongozo kuhusu TEHAMA kwa ajili ya Mahakama ya Tanzania, ambao ulipitishwa na kutekelezwa bila ucheleweshaji wowote,” amesema.

Kupitia mwongozo huo, Mhe. Dkt Nangela alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania na Serikali kwa ujumla vilianza mpango wa mageuzi na uboreshaji wa sekta ya sheria, ambao ulihusisha upatikanaji wa vifaa vinavyohusiana na TEHAMA na mafunzo ili kuwapatia ujuzi na uelewa muhimu watumishi wa Mahakama kuhusu mfumo huo wa teknolojia.

Mwongozo uliopitishwa mwaka 2007 uliongeza zaidi mbinu mpya ya kutengeneza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama wenye malengo na matokeo yanayopimika, mbinu ambayo imewezesha kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa imani ya wananchi katika Mahakama.

Baada ya kuhutubia Mkutano huo, Jaji Nangela aliongoza jopo la Majaji kwenye majadiliano ya kina yaliyohusu uhuru wa Mahakama.

 

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa Majaji Wakuu Barani Afrika wakimsikiliza Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.
Deo Nangela (hayupo katika picha) aliyemwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye Mkutano huo leo tarehe 04.Novemba 2021 unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,  Mhe.  Dkt. Deo Nangela akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari mara baada ya kuhutubia Mkutano wa Kimataifa wa Majaji Wakuu kutoka Bara la Afrika leo tarehe 04 Novemba, 2021 jijini Dar es Salaam. Kushoto  ni Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, Prof Elisante Ole Gabriel.



 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni