Na Lydia Churi na Stanslaus Makendi, Mahakama
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, amewataka watumishi wote wa Mahakama
kote nchini kufanya kazi kwa uadilifu ili kujenga Mahakama iliyo huru na
inayoaminika kwa Watanzania.
Mhe. Siyani alitoa wito huo
hivi karibuni katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi yaliyofanywa na
mtangulizi wake, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, katika Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki kilichopo jijini Dodoma.
“Hili suala la uadilifu
tutalisimamia kikamilifu. Yapo mambo mengi ambayo yanapaswa kufanyika ili watu
wawe na imani na Mahakama na maamuzi tunayoyatoa yasiwe na mashaka,”alisema na
kusisitiza kuwa ili kujenga Mahakama inayoaminika lazima iwe huru huku
watumishi wote wakifanya kazi kwa uadilifu mkubwa.
Jaji Kiongozi alisema, “Uwe
umekula kiapo au hujala kiapo. Kwa kuwa tu mtumishi wa Mahakama lazima kila
mmoja wetu awe mwaminifu. Mtendaji Mkuu
wa Mahakama anajua, kabla hata sijateuliwa, hata nyinyi wa Dodoma mnajua.
Hatutafanya mchezo kwenye suala la uadilifu kwa sababu tunaamini tukiwa na
watumishi waadilifu tutaifikia dira yetu.”
Mhe. Siyani alimshukuru
mtangulizi wake kwa kazi kubwa iliyofanyika. Hata hivyo, alibainisha kuwa kuna kazi
nyingine kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wanajenga Mahakama ambayo sio tu
inatimiza dira yake, lakini inayoaminika kwa Watanzania.
Akizungumza kuhusu usikilizaji wa mashauri, Jaji Siyani alimtaka kila mtumishi kwa nafasi yake
kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza ndoto ambayo Mahakama imejiwekea.
Alibainisha kuwa kuna takribani mashauri 8,000 ambayo yamepevuka, kwa maana
yamepita ukomo wa muda ambao Mahakama imejiwekea kuyamaliza.
“Msajili Mkuu yupo, Msajili
wa Mahakama Kuu yupo, hili ni eneo ambalo tunapaswa kulifanyia kazi. Lazima
tuwe na muda ambao tutajiwekea wenyewe na hatutarajii baada ya hapo kuwa na
mashauri ya mrundikano, na hili linawezekana kwa sababu tulipotoka tulikuwa na
mashauri mengi zaidi ya haya. Takwimu zinaonyesha kwamba tunakoelekea kuna
mafanikio, hivyo hatuwezi kurudi nyuma,” alisema.
Kwa upande wa Mahakama Kuu,
Kanda ya Dodoma aliyokuwa akifanya kazi kama Jaji Mfawidhi kabla ya uteuzi
wake, Jaji Kiongozi alielezea furaha yake kwa kuiacha Kanda hiyo ikiwa na
takwimu nzuri za usikilizaji wa mashauri.
Kwa mujibu wa Jaji Siyani, alipofika
kuhudumu katika Kanda hiyo kulikuwa na wastani wa mashauri 1,200, lakini mpaka anakabidhi
ofisi kwa Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. George Masaju, kulikuwepo na mashauri 835. “Idadi
ya mashauri yanayokwisha ni kubwa kuliko yale yanayosajiliwa. Jaji Masaju kazi
unayo kuhakikisha kwamba mwenendo huo haubadiliki, isipokuwa tunaongeza kasi,”
alisema.
Jaji Siyani aliahidi
kuendeleza kasi iliyoachwa na mtangulizi wake, Dkt Feleshi na kwamba kazi
kubwa aliyoifanya haitapotea. Hivyo, aliwashukuru Watumishi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, kwa
ushirikiano mkubwa waliompa, ambao pengine ndiyo uliosababisha aonekane kuwa
anafaa kushika nafasi hiyo mpya.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel,
alimpongeza Jaji Kiongozi mpya kwa kuteuliwa kushika nafasi hiyo na kuahidi
kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuimarisha maslahi ya watumishi na kuweka
ukaribu wa kazi za kimahakama na zile zisizo za kimahakama kwa lengo moja la
kuharakisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Alimuomba pia kuendelea
kutengeneza mfumo imara wa kuimarisha maadili kwa watumishi wote wa Mahakama ya
Tanzania. “Naomba nikiri wazi kwamba sina uvumulivu na uzembe. Ningetamani yale
maagizo ya Mhe. Rais aliyotupatia kusimamia maadili katika kazi
tunayatekeleza,” alisema.
Kwa upande wake, Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, naye aliahidi kutoa
ushirikiano wa kutosha kwa Jaji Kiongozi kwa kuwa yeye kama msimamizi mkuu wa
uendeshaji wa mashauri atakuwa naye bega kwa bega ili kuhakikisha Mahakama zote
zinatekeleza jukumu lake la msingi la utoaji haki kwa manufaa ya umma.
Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji Siyani amewaasa watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (Integrated Justice Centre – Dodoma) kutekeleza majukumu yao kwa weledi, bidii na ubunifu.
Akizungumza katika hafla ndogo ya kuagana na watumishi wa Kituo hicho iliyofanyika hivi karibuni Mahakamani hapo, Jaji Siyani pia aliwataka kuzingatia maadili wakati wa kuwahudumia wananchi na hivyo kutekeleza kwa vitendo azima ya utoaji wa haki kwa wakati.
"Nitaendelea kufuatilia kwa ukaribu utendaji kazi wa Mahakama zote za Kanda ya Dodoma. Hivyo, ninawataka muwe makini muda wote katika kazi, mtoe huduma bora kwa wateja huku mkizingatia Maadili ya Utumishi wa Umma,” alisema.
Baada ya nasaha hizo Kiongozi huyo aliwashukuru watumishi wote wa Mahakama za Kanda ya Dodoma kwa ushirikiano na utendaji kazi uliochagiza kupungua kwa mrundikano wa mashauri Mahakamani na kuwataka kuendelea na bidii hiyo katika kazi zao.
Watumishi wa Mahakama Kuu katika Kanda hiyo waliandaa hafla fupi kwa ajili ya kuagana naye kufuatia kuteuliwa kwake Oktoba 08, 2021 na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Katika hatua nyingine, Jaji Siyani amewasili
katika ofisi yake leo iliyopo Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam na kupokelewa
na watumishi waandamizi wa Mahakama hiyo, akiwemo Jaji aliyekuwa anakaimu nafasi
hiyo, Mhe, John Mgeta. Viongozi wengine waliokuwepo ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe,
Amir Mruma, Jaji Ilvin Mugeta, Jaji Zahra Maruma, Jaji Leila Mgonya na Jaji
Said Kalunde, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Msajili wa Mahakama Kuu na
Naibu Msajili Mwandamizi, Kanda ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla
hiyo fupi, Mhe. Jaji Siyani aliwashukuru wote kwa mapokezi ambayo hakuyategemea na
kubainisha kuwa kile alichokiona kinaashiria dhana nzuri ya ushirikiano katika
utekelezaji wa majukumu yaliyo mbele yao. Alisema kuwa kama wakifanikiwa
kutekeleza dira waliyojiwekea watakuwa wamefanikiwa wote, Hivyo amewaomba
Majaji, Wasajili na watumishi wa kada zote kushirikiana na kuendelea kuchapa
kazi kwa bidii.
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma
Mhe. Mustapher Siyani (Kwa sasa Jaji Kiongozi) akiwasili viwanja vya Kituo
Jumuishi cha Utoaji Haki – Dodoma mara baada ya shughuli za kuapishwa kwake
kukamilika Oktoba 11, 2021.
Sehemu ya watumishi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki wakimsikiliza Mhe. Jaji Siyani wakati wa hafla hiyo.
DAR ES SALAAM: Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani akizungumza na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu alipowasili leo Ofisini kwake Mahakama Kuu-Dar es Salaam.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani, akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na Wahe. Majaji, Wasajili na Watendaji wa Mahakama Kuu mara baada ya kuwasili ofisini kwake leo Oktoba 15, 2021.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni