Jumatatu, 11 Oktoba 2021

RAIS SAMIA AMUAPISHA JAJI SIYANI KUWA JAJI KIONGOZI WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA

-Makamu wa Rais ataka hukumu za Mahakama kutekelezwa

Lydia Churi na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo Oktoba 11, 2021 amemwapisha Jaji Mustapher Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Jaji Siyani anakuwa Jaji Kiongozi wa kumi (10) na mwenye umri mdogo kuliko wote waliomtangulia kushika wadhifa huo na anachukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Jaji Dkt Eliezer Mbuki Feleshi, ambaye ameteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Hafla ya uapisho huo iliyofanyika Ikulu jijini Dodoma imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, Waziri wa Sheria na Katiba, Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mhe. Ummy Mwalimu.

Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhiria hafla hiyo ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Kelvin Mhina, huku Mhimili wa Bunge ukiwakilishwa na Naibu Spika, Mhe. Dr Tulia Ackson.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alimtaka Jaji Kiongozi mpya kutekeleza majukumu yake kwa haki kama inavyotakiwa, ikiwemo kuimarisha mfumo wa TEHAMA ili kurahisisha usikilizaji wa mashauri kwa kuzingatia ukubwa wa nchi ulivyo. Aliwakumbusha kuwa uongozi si zawadi, bali ni dhamana.

“Kama ni dhamana, uongozi una miiko yake. Hivyo macho yetu kwenu ni kuona kwamba viongozi mnakuwa mfano wa yale ambayo tunayakataza kwa kuzingatia sheria zetu kuwa sio mazuri kwa nchi yetu. Niwatakie kila la heri mlioapa, mkafanye kazi vyema na kushirikiana na wenzenu. Tunachohitaji ni maendeleo kwa Watanzania,” alisema.

Akimkaribisha Mhe. Rais kuzungumza na Watanzania kupita hafla hiyo, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesisitiza ushirikiano kati ya Mihimili ya dola na kushauri mamlaka zinazohusika kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mahakama ili kusimamia haki kwa Watanzania.

“Nilikumbana na kesi mbili hivi, Mahakama inaamua lakini hukumu haitekelezwi. Kwa hiyo unakaa unasema kitu gani hiki. Nataka niwaombe sana Wakuu wa Mikoa wote kuliangalia hili. Nyinyi ndiyo mnasimamia vyombo vya dola kwa niaba ya Rais kwenye Mikoa aliyowakabidhi,” alisema.

Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais aliwaomba Mahakimu pia kuliangalia suala hilo, kwa vile hatarajii kuona mambo yanaisha hivyo hivyo wanapomaliza kuandika hukumu zao.

“Mhe. Jaji Mkuu ni vizuri kuwa na namna ya kufuatilia kama hukumu zilizotolewa na Mahakama zinatekelezwa ili vyombo vinavyohusika viweze kusimamia haki kwa wananchi,” alisema na kuwapongeza wale wote walioapishwa na kuwaomba wakatimize matarajio ya Mhe. Rais aliyewaamini na matarajio ya watanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, aliwapongeza wote walioapishwa kwa kuaminiwa na kiongozi wa nchi kushika dhamana kwenye nafasi walizoteuliwa, jambo ambalo ni imani kubwa ambayo Mhe. Rais ameionesha kwao ya uwajibikaji.

“Wote nawatakia kazi njema. Niwaahidi nitawapa ushirikiano wa dhati katika kila sekta. Tunahitaji sekta hizi ziweze kushamiri kwenye utendaji wa kila siku, lakini tutapata mafanikio kwa sababu tunafanya kazi pamoja,” alisema.

Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia pia alimwapisha aliyekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na Mhe. Sofia Mjema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, ambaye amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt Philemon Sengati, ambaye uteuzi wake umetenguliwa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza mara baada ya kumuapisha Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani na Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Omar Othuman Makungu Ikulu Chamwino jijini Dodoma.


Mhe. Omar Othuman Makungu akiapa Ikulu Chamwino jijini Dodoma mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan cha kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.


Mhe. Mustapher Siyani akiapa Ikulu Chamwino jijini Dodoma mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan cha kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni