Lydia Churi na Innocent Kansha – Mahakama, Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma,
ameaninisha vigezo vilivyotumika kupendekeza jina miongoni mwa
Majaji 85 wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa Jaji Kiongozi, ikiwemo kutimiza sifa
zote za kikatiba, unyenyekevu, busara, na uelewa mpana wa mambo ya Mahakama.
Akizungumza katika hafla fupi ya uapisho uliofanywa leo
Oktoba 11, 2021 Ikulu jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Jaji Mkuu alimpongeza Jaji Mustapher Siyani kwa
kuteuliwa kuwa Jaji Kiongozi na kwamba ametimiza sifa zote za Katiba za kuweza
kushika nafasi hiyo.
Ameeleza kuwa kuna vigezo ambavyo vilitumiwa na Tume
ya Utumishi wa Mahakama kabla ya kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi huo kwa
kuzingatia kuwa Jaji Kiongozi ni mshauri Maalumu wa Jaji Mkuu na anabeba mzigo
mkubwa wa kusimamia Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama zote za chini.
“Ukiangalia idadi ya Mahakama Kuu ambapo kuna vituo 17 na divisheni nne za Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi 29, Mahakama za
Wilaya 139 na Mahakama za Mwanzo 960, kazi yako kwa kweli siyo nyepesi, kwa
sababu wewe ndiye msimamizi mkuu wa hayo maeneno na kila siku unatakiwa kujua
kitu gani kinaendelea katika ngazi hizi zote za Mahakama,” Prof. Juma
alimwambia Jaji Kiongozi huyo mpya.
Prof. Juma amesema kuwa kutokana na majukumu hayo
mazito, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilikuwa na vigezo mbalimbali ilivyokuwa
inaviangalia, ikiwemo uelewa mpana wa Mahakama na tamaduni zake za ndani kwa
kuzingatia kuwa katika taasisi yoyote, mambo mengi huwa yamejificha.
“Ni kama vile barafu, siku zote unaona ncha lakini uzito
wa barafu huuoni. Mimi naamini wewe unafahamu ndani ya barafu na unaifahamu
Mahakama. Ukifahamu undani wa Mahakama utakuwa katika nafasi nzuri sana ya
kufanya maboresho. Hiyo ilikuwa ni sifa ambayo
wewe na wengine ambao mlipelekwa kwa Mhe. Rais ulikuwa umeitimiza,”
alisema.
Vile vile Jaji Mkuu alimweleza Jaji Kiongozi mpya kuwa
anatakiwa kuelewa Mahakama sio kisiwa, ambacho hakiingiliani au hakishirikiani
na Mihimili mingine. Alisema kuwa Jaji Kiongozi anapaswa kuelewa mipaka ya
Mahakama na mipaka ya Mihimili mingine, ikiwemo changamoto zilizopo.
“Unatakiwa uwe na busara, umri wako ni mdogo, wewe ni
kiongozi. Utaongoza watu ambao wana umri mkubwa zaidi yako, (hivyo) busara,
hekima, utu na ubinadamu ni jambo ambalo
kiongozi yoyote katika nafasi yako anatakiwa kuwa nayo,” alisema Jaji Mkuu.
Kwa mujibu wa Prof. Juma, Jaji Kiongozi anapaswa pia
kuelewa Mahakama inapokwenda kwa vile wakati mwingine Majaji na Mahakimu huandika
hukumu bila kujua dunia inayowazunguka, ambapo baada ya kutekeleza majukumu yao
ya kutoa haki hudhani kwamba wajibu wao umeishia hapo, ilihali nchi na Mahakama
hufanya mambo mengine ambayo watu wengi hawayafahamu.
“Kwa hiyo wewe ni jukumu lako kutukumbusha sisi Majaji
wapi dunia inakwenda na wapi Mahakama inakwenda ili tuelewe, kwa sababu
usipoelewa nchi yako inakwenda wapi utakuwa siku zote kazi yako wewe ni kukosoa
yale ambayo yanafanyika,” alisema.
Prof. Juma alimkumbusha dhana ya safari ya kwenda Mahakama Mtandao ambayo
anapaswa kuielewa vizuri kwa vile jambo hilo ni dhahiri kwa kuzingatia vigezo
ambavyo Mahakama ya Tanzania imejiwekea ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika
TEHAMA. “Sasa ni wakati wa kufanya uwekezaji ule uzae matunda. Wewe ni
msimamizi ambaye ni muhimu sana katika hilo,” alisema.
Jaji Mkuu pia alitoa wito kwa Mhe. Siyani kuwa na uwezo
wa kujenga umoja, kwa sababu katika kila taasisi huwa kuna mashindano yenye
mwelekeo wa kutaka kujua nani alimaliza Chuo Kikuu kwanza, nani alipata ‘Division
One,’ nani alifaulu kibahati bahati.
“Kwa hiyo, kuna kule kudharauliana, kada nyingine
inajiona kuwa bora zaidi ya nyingine. Sasa wewe kazi yako ni kujenga umoja
baina ya watumishi wote kwa sababu kila mmoja ni muhimu katika kufikia malengo
ya Mahakama,” alisema Jaji Mkuu, huku akimshauri Mhe. Siyani kuwa na shauku ya
kujifunza ili kuongezea kiwango chake cha elimu, jambo ambalo ni jema na sifa
ya uongozi.
Hata hivyo, Prof. Juma alitoa angalizo kuwa sifa kama
hiyo isiwe zaidi ya kuheshimu taaluma, kwa sababu mtu anaweza kuwa amesoma sana
na kudharau taaluma zingine ambazo zinafanikisha kazi yake. Kwa hiyo, Jaji Mkuu
alimshauri Jaji Kiongozi mpya kuwa mnyenyekevu siku zote na kusikiliza utaalamu
uliopo kwa kuzingatia kuwa kuna utaalamu mwingi ndani ya Mahakama.
Jaji Mkuu pia alimwelekeza Mhe. Siyani kusimamia
vilivyo nguzo zote tatu za Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania. Amezitaja nguzo hizo kama Utawala bora,
Uwajibikaji na Usimamizi wa rasilimali; Upatikanaji wa haki kwa wakati na Kuimarisha
imani ya wananchi, kwa sababu bila imani ya wananchi ushirikiano wa wadau
wengine, Mahakama inakuwa haina faida.
Katika hafla hiyo, Mhe, Rais Samia alimuapisha pia aliyekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania. Kwa mujibu wa Prof. Juma, Mhe. Makungu amekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar kwa zaidi ya miaka 10.
“Karibu sana Mahakama ya Rufani ambapo kazi kubwa ni
kusimamia sheria na utatupa ladha ya Sheria za Zanzibar ambazo zitatusaidia ili
wananchi wote wa Tanzania waweze kufahamu sheria za Zanzibar,” alisema Jaji
Mkuu.
Alitoa pongezi pia kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga mpya,
Mhe. Sofia Mjema, ambaye kwa nafasi yake ni mdau mkubwa wa Mahakama.
“Ninaamini utakapofika Shinyanga, Jaji Mfawidhi na watendaji wengine wa
Mahakama watakutembelea na kukujulisha kuhusu changamoto mbalimbali ambazo
Mahakama inakumbana nazo,”alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni