Na Stanslaus Makendi- Mahakama Kuu, Dodoma
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, amewataka watumishi wa Mahakama kote nchini kuzingatia weledi na uwazi wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki ili kujenga dhana chanya ya uadilifu kwa wananchi.
Mhe, Chuma alitoa wito huo Oktoba 8, 2021 alipokuwa akizungumza na
watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kongwa na Mahakama ya Mwanzo Kongwa katika
ziara ya kikazi kukagua shughuli mbalimbali za utoaji haki. Amewasisitiza watumishi
wote kutekeleza kikamilifu maagizo na maelekezo yanayotolewa na viongozi wa
Mahakama ya Tanzania.
Msajili Mkuu alichukua nafasi hiyo pia kuwataka watumishi katika
Mahakama hizo kuimarisha ushirikiano baina yao pamoja na Taasisi au vyombo vingine
kwa kufuata utaratibu uliopo ili kutoathiri utendaji kazi wa Mhimili wa Mahakama.
Katika ziara yake ya siku moja kukagua shughuli za Mahakama katika Wilaya
ya Kongwa, Mhe. Chuma amewasisitizia watumishi hao kuhuisha mara kwa mara taarifa
za mashauri kwenye Mfumo wa Kusajili na Kuratibu
Mashauri kwa njia ya Kieletroniki (JSDS II) ili kurahisisha utendaji kazi wa Mahakama
na kuwa na taarifa zinazowezesha uongozi kufanya maamuzi.
Mhe. Chuma aliwapongeza watumishi wote kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya
na kubainisha kuwa ni vyema watumishi wote wakaelewa maendeleo na maboresho makubwa
yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania, hivyo kuwa sehemu ya kuhabarisha umma na kusimamia
utekelezaji wake.
Katika ziara hiyo, Msajili Mkuu pia alipata nafasi ya kumtembelea Mkuu wa
Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remedius Emmanuel, na kumwelezea umuhimu wa kushirikiana
katika kutoa elimu kwa Umma ili wananchi waelewe taratibu za Mahakama na huduma
zake, hususani katika eneo la mirathi, ndoa na talaka ambalo bado lina changamoto
nyingi.
Alisema kuwa kumekuwepo na changamoto nyingi katika mashauri hayo,
ikiwemo wasimamizi wa mirathi kuchelewa kufunga mirathi mahakamani, kugeuka na
kujiona ni warithi halali, hivyo kujimilikisha mali kinyume na taratibu.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzaniaakimwelezea jambo Mkuu wa wilaya ya Kongwa Bw. Remedius Emmanuel alipomtembelea ofisini kwake.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (katikati), akifurahia jambo baada ya kukamilisha ukaguzi wake katika Mahakama ya Mwanzo Kongwa. Kushoto kwake ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kongwa, Mhe. Kisasila Saguda, na kulia kwake ni Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Kongwa, Mhe. Somoe Kalanje
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma, (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Kongwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni