Ijumaa, 8 Oktoba 2021

CHANGAMOTO UPUNGUFU WA HUDUMA ZA MAHAKAMA KIBAIGWA YATATULIWA

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Kibaigwa

Mahakama ya Tanzania imeanza kushughulikia changamoto ya ukosefu wa Mahakama za Mwanzo hapa nchini kufuatia hatua ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuzindua Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa Oktoba 7, 2021 iliyojengwa katika Wilaya ya Kongwa, Mkoa wa Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Juma alisema kuwa uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa ni muendelezo wa matukio ya uzinduzi wa majengo ya Mahakama yanayoendelea kujengwa kwenye maeneo mbalimbali nchini katika utekelezaji wa Programu ya Maboresho ya Mahakama inayolenga kupeleka huduma karibu na wananchi wa Tanzania.

“Ujenzi wa jengo hili umetimiza lengo la kuleta huduma karibu na wananchi na pia kuboresha mazingira ya utoaji haki. Ni dhahiri sasa wananchi waliokuwa wanalazimika kusafiri umbali wa kilomita 10 kutoka hapa Kibaigwa kwenda Kijiji cha Pandambili kwa ajili ya kutafuta huduma ya Mahakama watapata huduma hiyo hapa Kibaigwa,” amesema.

Aliwakumbusha wananchi kuwa uwepo wa huduma bora za Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini ni kichocheo cha amani, utulivu na maendeleo ya shughuli za kiuchumi na ustawi wa jamii, huku akionya kuwa hakutakuwepo na jamii inayoweza kupiga hatua za maendeleo ya kiuchumi kama hakuna Taasisi imara ya utoaji haki kama Mahakama.

Kwa mujibu wa Prof. Juma, jengo alilolizindua ni jengo la kisasa lenye vifaa na mahitaji yote muhimu kuwawezesha watumishi wote wa Mahakama kufanya kazi zao kwa ufanisi, hivyo ni imani yake wananchi na wadau wote watapata huduma za Mahakama zilizo bora na zinazokidhi matarajio yao.

“Jengo hili lina miundombinu yote muhimu ikiwemo vifaa vinavyowezesha matumizi ya TEHAMA na samani za kutosha. Ni matumaini yangu kwamba vifaa vya TEHAMA vilivyoko katika jengo hili vitatumika kurahisisha kazi za Mahakama na zile za wadau tunaowahudumia,” alisema.

Mhe. Jaji Mkuu aliwapongeza wananchi wa Mji Mdogo wa Kibaigwa kwa kupata jengo jipya na la kisasa ambapo Mahakama hiyo itatoa huduma za ambazo wananchi wamezisubiri kwa muda mrefu. Alisema kuwa ni imani yake kukamilika kwa jengo hilo kutaharakisha huduma za utoaji haki kwa wananchi wa Mji Mdogo wa Kibaigwa.

Akizungumza katika sherehe za ufunguzi huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, alisema kuwa ujenzi wa Mahakama hiyo yenye ukubwa wa mita za mraba 835 ulianza Mwezi Aprili 2020, ambapo ulitakiwa kukamilika mapema, lakini ulichelewa kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo uwepo wa ugonjwa wa UVICO-19.

Amesema kuwa Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa inaonekana kuwa tofauti na mahakama zingine kwa sababu jengo hilo limejengwa kimkakati kwa kuangalia mwelekeo wa mji mdogo wa Kibaigwa na kwa kuzingatia ukuaji na idadi kubwa ya wananchi katika eneo hilo, hivyo linaweza pia kufanya shughuli za Mahakama ya Wilaya.

Kwa mujibu wa Prof. Ole Gabriel, Mahakama hiyo ya Mwanzo imezingatia mahitaji mbalimbali ikiwemo masuala ya usalama, watu wa rika zote wakiwemo wenye mahitaji maalum kufika kwa urahisi na matumizi ya TEHAMA ambayo yatawezesha mashauri kusikilizwa kwa njia ya mtandao.

“Jengo hili limejengwa kwa teknolojia ya kisasa, yaani matumizi ya Molad kwa gharama nafuu ya kiasi cah 797,687,635/-. Tunasema ni gharama nafuu kwa sababu ukubwa wa jengo unaridhisha na pengine vitu ambavyo vimewekwa humo ndani navyo vitasaidia sana. Hadi hivi sasa Mkandarasi ameshalipwa 676,006,470/-,” alisema na kubainisha kuwa fedha iliyobaki inasubiri masuala mengine ikiwemo uwasilishaji wa vyeti baada ya kukamilisha ujenzi kulingana na mahitaji ya mkataba.

Akitoa utambulisho wa viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe za ufunguzi wa Mahakama hiyo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma, aliwaalika wananchi wote wanaosumbuka na kuelemewa na migogoro na Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa, kwa vile ipo tayari hivi sasa kutoa huduma za haki, itawapumzisha.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa uliofanyika jana katika mji mdogo wa Kibwaigwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma.
Baadhi ya wageni  waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa wakifuatilia shughuli hiyo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai wakisalimiana mara baada ya  kuwasili kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibwaigwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof.  Elisante Ole Gabriel akimuelezea jambo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati wa hafla ya  uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa .

Jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa.




(Picha na Mary Gwera na Lydia Churi)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni