Ijumaa, 8 Oktoba 2021

SOTE TUHESHIMU MAAMUZI YA MAHAKAMA-SPIKA NDUGAI

 Na Faustine Kapama – Mahakama, Kibaigwa

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai, ametoa wito kwa watendaji wa Serikali na wananchi kwa ujumla kuheshimu na kutekeleza maamuzi ya Mahakama ili mlolongo wa haki unaotolewa uweze kukamilika.

Mhe. Spika alitoa wito huo Oktoba 7, 2021 katika hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa uliofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Mahakama na Bunge. Mhe. Ndugai, ambaye ni Mbunge wa eneo hilo ambalo lipo ndani ya Jimbo la Kongwa, alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imekuwa ikijitahidi kutekeleza jukumu lake la kutoa haki kwa wananchi.

“(Lakini) inakuwa mtihani kule kwa watekelezaji unapokwenda kutekeleza haki hiyo. Mahakama imeshamaliza kazi yake na kumpa haki (fulani), kwamba nyumba hii ni ya huyu, huyu alidhulumiwa ng’ombe hawa, arudishiwe. Kwenda kupata hao ng’ombe sasa! Nitoe wito kwa watendaji wote wa serikali, tumalizie kile kipande cha haki, maamuzi ya Mahakama sote tuyaheshimu ili mlolongo wa haki ukamilike,” alisema.

Amebainisha kuwa katika wiki mbili zijazo watatembelea mahali fulani pamoja na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, ambapo Mahakama imeshamaliza mambo yake, lakini wananchi wanaohusika bado wanalilia haki yao waliyoipata haijatekelezeka. Hivyo, alisisitiza kuwa pale Mahakama ikishakamilisha mchakato wa utoaji haki, yule aliyeshindwa anapaswa kuheshimu maamuzi hayo, vinginevyo afuate utaratibu wa Mahakama kwa kukata rufaa.

Kwa mujibu wa Spika Ndugai, Mahakama ya Kibaigwa imejengwa kwa ajili ya kutoa haki, hivyo ni wajibu wa wananchi kuwaombea watumishi wote watakaokuwa kwenye Mahakama hiyo pamoja na watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla, akiwemo Jaji Mkuu mwenyewe, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu na wengine wote wanaoshughulika na masuala ya utoaji haki nchini.

“Kutoa haki, ndugu zangu ni mtihani mkubwa sana. Mtoa haki yoyote anatakiwa kuwekwa mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Niombe sana viongozi wa dini, zote tuwe tunakumbuka kuwaombea watoa haki wetu, kwa sababu wenyewe mnasema kila wakati kuwa nchi ikikosa haki, basi imekosa kuwa karibu na Mungu. Mjane apate haki yake, maskini apate haki yake, mwenye haki apate haki yake. Kama tunavyoambiwa, haki inayocheleweshwa ni kama vile imekosekana,” alisema.

Mhe. Ndugai pia alitumia hafla hiyo kurudia kutoa msimamo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa halitaingilia shughuli za Mahakama ya Tanzania na kwamba Bunge hilo litajitahidi kutunga sheria nzuri zinazotekelezeka ambazo zinaiongoza vizuri nchi yetu.

“Hatupendi hata mara moja kuingilia Muhimili wa Mahakama, wala hatujaingilia na tutajitahidi sana kuhakikisha kwamba tunakwenda na msimamo na utaratibu huo. Unajua sisi pale bungeni tupo mchanganyiko maalumu. Kuna mwingine anaweza kuamka kushoto, mwingine akaamka kulia. Kama ambavyo huwa nasema mara kwa mara, mkiona tumeteleza ulimi, hata kama ni mimi mwenyewe, basi mnatubonyeza tu ili turudi kwenye mstari,” alisema.

Spika wa Bunge pia aliiomba Mahakama kuwakumbusha pale wanapoona wanaenda kinyume kwenye mchakato wa utungaji wa sheria, kwa kuwa hakuna mwenye nia ya kutunga sheria mbaya. “Nia yetu ni kutunga sheria zinazotekelezeka, sheria nzuri zinazoweza kuingoza nchi yetu vizuri,” alisisitiza.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Najma Giga, aliushukuru uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano wanaotoa kwa Kamati yake. Alisema kuwa maendeleo yaliyofikiwa, ikiwemo miundombinu na mifumo ya Tehama katika majengo waliyotembelea yamejengwa kwa thamani halisi ya fedha.

“Nipo katika kamati hii kwa mwaka wa sita nikiwa kiongozi. Maendeleo yaliyofikiwa kwa namna zote, kuanzia miundombinu, utumiaji wa Tehama kwa kurahisisha kuendesha mashauri ni hatua kubwa sana. Kiuhalisia, majengo mengi tuliyotembelea yemejengwa kwa hadhi na thamani ya fedha iliyotumika. Kwa kweli hili ni jambo la uaminifu na inahitaji kupongezwa kwa dhati kabisa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remedius Emanuel, ameishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kukamilisha ujenzi wa Mahakama hiyo, ambayo itakuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi, hususan wakazi wa mji mdogo wa Kibaigwa ambao unakua kwa kasi. Amesema kuwa kabla ya kujengwa kwa Mahakama hiyo wananchi walikuwa wakitumia muda mrefu kutembea kufuata huduma za Mahakama katika maeneo mengine kama Kongwa na Bomba Mbili.

Habari hii Imehaririwa na Lydia Churi.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akizungumza wakati wa Hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa iliyoko katika wilaya ya Kongwa Dodoma. Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alizindua jengo hilo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa katika hafla iliyofanyika jana. Wa tatu kushoto ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai, wa kwanza kushoto ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. John Mgeta akifuatiwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani na kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa Bw. Remidius Emmanuel.

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai wakifungua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa katika hafla iliyofanyika jana Kibaigwa wilayani Kongwa mkoani Dodoma. 

 Jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa.


Baadhi wa wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Kongwa pamoja na wageni mbalimbali walioalikwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Kibaigwa iliyofanyika jana. 

 (Picha na Lydia Churi na Mary Gwera)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni