Na Mary Gwera, Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameridhishwa
na ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji haki nchini kutokana na ubora aliojionea
katika uzinduzi alioufanya leo Oktoba 06, 2021 jijini Dodoma unaoakisi thamani halisi
ya fedha iliyotumika.
Ujenzi wa Vituo hivyo sita (6) vilivyojengwa katika mikoa ya Dar es
Salaam (Kinondoni na Temeke), Dodoma, Arusha, Mwanza na Morogoro umegharimu zaidi
ya bilioni 51 za kitanzania ambapo jengo la Dodoma alilolizindua na Mhe. Rais
Samia Suluhu Hassan limetumia zaidi ya bilioni 9.
“Ndugu zangu nimepata fursa ya kukagua jengo hili, jengo ni zuri na
kusema ukweli linaendana na hadhi ya karne ya 21. Nimeliangalia wakati napata
maelezo nikaambiwa bilioni 9 nikanyanyua uso na kuangalia zimeingia wapi,
lakini nilivyoingia ndani nimeziona bilioni 9 zilivyotumika, kwa hiyo kwenye
jengo hili thamani ya fedha kwa jengo iko sawasawa,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisifu mpangilio wa jengo kwa kuwa na huduma za watu wenye
mahitaji maalum pamoja na vyumba vya kunyonyesha watoto, jambo ambapo amekiri kufurahishwa
navyo.
“Ukilinganisha na Mahakama tulizonazo sasa kabla ya hizi, Mama
anayenyonyesha hutakiwa kujifiche kwenye kichochoro ndio anyonyeshe mtoto wake na
kusababisha usumbufu, kwahiyo yaliyomo kwenye jengo hili nikiri yamenifurahisha
sana,” alieleza Rais Samia.
Aidha, Mhe. Rais amewashukuru Wadau wa Maendeleo hususani Benki ya Dunia
(World Bank) kwa kufadhili mradi wa maboresho ya Mahakama, ikiwemo ujenzi wa
Vituo hivyo kupitia fedha za mkopo.
Sherehe za uzinduzi wa vituo hivyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali,
akiwemo Spika wa Bunge, Mhe, Job Ndugai, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof.
Palamagamba Kabudi, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Makungu, Jaji Mkuu wa
Tanzania mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.
Antony Mtaka na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Wananchi walianza kumiminika katika viwanja vya Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki kilichopo mtaa wa NCC, karibu na Benki Kuu, Dodoma majira ya saa
moja na nusu na baadaye kupata burudani mbalimbali za ngoma kutoka kikundi cha
Changamoto na nyimbo za kusisimua zilizoimbwa na Kwaya ya Mahakama ya
Tanzania. Wimbo wa kuhamasisha chanjo kwa Watanzania ulionesha kukonga nyoyo za
wananchi waliohudhuria sherehe hizo.
Mgeni rasmi katika sherehe za ufunguzi wa vituo hivyo aliwasili katika
viwanja vya mahakama majira ya saa nne asubuhi na kupokelewa na mwenyeji wake
Jaji Mkuu wa Tanzania pamoja na wageni wengine kutoka meza kuu na baadae
alipata maelezo mafupi ya usanifu wa majengo hayo kabla ya kuzindua rasmi vituo hivyo kwa kufungua kitambaa na kukata utepe kwa kushirikiana na
Mhe, Jaji Mkuu wa Tanzania.
Mhe. Rais aliingia ndani ya jengo ili kujionea uhalisia aliousikia huku
akipata maelezo ya kina kutoka kwa Mtendaji Mkii wa Mahakama ya Tanzania, Prof.
Elisante Ole Gabriel na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Maboresho,
Jaji Zahra Maruma.
Baada ya kukagua jengo hilo kwa ndani, Mhe. Rais alikaribishwa kwenye
jukwaa kuu ambapo wimbo wa Taifa ulipigwa na kufuatiwa na wimbo wa Aftrika
Mashariki. Baadaye, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbard Chuma,
alitoa utambulisho wa viongozi waliohudhuria hafla hiyo, huku Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelezo ya mradi mzima
unaohusiana na ujenzi wa vituo hivyo.
Ulifika wakati wa Waziri wa Katiba na Sheria ambaye alitoa neno juu ya
ujenzi wa vituo hivyo na maendeleo ya Mahakama ya Tanzania tangu uhuru mwaka
1961 na baadaye Jaji Mkuu wa Tanzania alitoa salamu na kisha kumkaribisha Mhe,
Rais kuzungumza na Watanzania kupitia hafla hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni