Jumatano, 6 Oktoba 2021

TANZANIA NCHI YA KWANZA BARANI AFRIKA KUTOA HUDUMA JUMUISHI ZA HAKI

Na Lydia Churi-Mahakama, Dodoma 

Mahakama ya Tanzania imeandika historia mpya kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa vituo Jumuishi vya Utoaji Haki nchini na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutoa huduma jumuishi za haki ndani ya jengo moja.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa vituo sita Jumuishi vya Utoaji haki iliyofanyika leo jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema vituo hivyo vitasaidia uharakishwaji wa utoaji haki na hivyo kuchochea ushiriki wa wanachi katika shughuli za kiuchumi.  

Alisema kuanzishwa kwa huduma jumuishi kutawapunguzia wananchi na wadaawa gharama na muda wanaotumia katika kutafuta haki zao zinazotolewa na wadau wa aina tofauti kwa kuwa vituo hivyo vinawakutanisha wadau wa mnyororo wa utoaji haki ndani ya jengo moja.

Alisema vituo hivyo pia vitawezesha usimamizi na ufuatiliaji wa utoaji wa huduma za kimahakama kufanyika kwa haraka zaidi katika utaratibu wa kila siku au pale litakapojitokeza tatizo tofauti na hali ya sasa. Alisema awali tatizo likijitokeza huchukua muda au kusubiri ukaguzi unaofanywa katika kipindi cha miezi mitatu au robo mwaka.

“Vituo hivi vitasaidia kupunguza gharama za uendashaji wa shughuli za kiutawala na kimahakama kwa kuwa rasilimali itatumika katika jengo moja badala ya majengo matatu ya mahakama ya ngazi tofauti”, alisisitiza Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu alisema vituo jumuishi vitakuwa ni vitovu vya matumizi ya teknolojia kwa kuwa vitasogeza huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi. Aliongeza kuwa pamoja na kuwa huduma za ngazi zote za Mahakama zitapatikana ndani ya jengo moja, bado wananchi wengi watakuwa mbali na majengo haya hivyo mifumo ya Tehama itawasogeza wananchi hao karibu na huduma za Mahakama ikiwemo nakala za hukumu, na taarifa kuhusu mashauri yao.

Mbali na huduma za Mahakama, vituo hivi vitaiwezesha Tanzania kuongezewa alama za upimwaji wa utoaji wa huduma katika mizani ya wananchi kuridhishwa na huduma zitolewazo na Mahakama. Alitoa mifano ya vipimo hivyo kuwa ni pamoja na vipimo vya urahisi wa kufanya biashara (Doing Business), utafiti unaopima mitazamo ya jamii katika masuala mbalimbali ya uchumi na kijamii ikiwemo utawala wa sheria na utoaji na utoaji haki.

Akizungumza kituo cha Utoaji Haki Temeke ambacho ni maalum kwa mashauri ya Mirathi, Ndoa na Talaka, Jaji Mkuu alisema kituo hiki kimebeba kuwa mfumo wa utoaji haki una wajibu wa kuwainua watu wote katika jamii ambao hawapati nafasi saw ana wengine katika kufikia haki wakiwemo wanawake, Watoto na walemavu na watu wanaoishi kwenye mazingira magumu .

Alisema kituo hiki kilianzishwa kutokana na kuwepo kwa mashauri mengi yanayohusu masuala ya kifamilia yakiwemo mashauri ya mirathi. Alifafanua kuwa mkoa wa Dar es salaam ulikuwa na mashauri ya mirathi 7,600.  

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel akielezea miradi ya ujenzi wa majengo ya Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki alisema licha ya majengo hayo kukamilika, bado Mahakama ya Tanzania inakabiliwa na ukosefu wa huduma za Mahakama Kuu katika mikoa tisa (9) nchini ikiwemo Singida, Njombe, Songwe, Geita, Manyara, Pwani, Katavi, Lindi na Simiyu. Alisema lengo la Mahakama ni kuwa na Mahakama Kuu kwenye kila Mkoa ili kurahisisha shughuli za utoaji haki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki ambapo kituo kilichopo Dodoma kimewakilisha vituo vingine vilivyopo katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Morogoro na Dar es salaam (Temeke na Kinondoni). Vituo hivi vimejengwa kwa fedha za wananchi wa Tanzania kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia. Ujenzi wa vituo hivyo umegharimu fedha za kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 51.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma. Wa tatu kulia ni Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, wa pili kulia ni Mhe. Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  wa kwanza kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu, wa tatu kushoto ni Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na  Sheria, wa kwanza kushoto ni Mhe. Antony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na wa pili kushoto ni Mhe. Mustapher Siyani, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma (IJC-Dodoma).
Muonekano wa mbele ya moja kati ya majengo sita, ambayo yamezinduliwa na Mhe. Rais Samia. Uzinduzi wa Kituo hicho umewakilisha vituo vingine ambavyo vimejengwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam yenye majengo mawili (Kanda ya Temeke na Kanda ya Kinondoni). 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni