Jumatano, 6 Oktoba 2021

RAIS SAMIA AZINDUA VITUO JUMUISHI VYA UTOAJI HAKI NCHINI

-Ahimiza kasi ya usikilizaji wa mashauri

Na Faustine Kapama , Mahakama-Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo Oktoba 6, 2021 amezindua rasmi Vituo sita Jumuishi vya Utoaji Haki (Integrated Justice Centres) ambapo amewahimiza Majaji na Mahakimu kuharakisha usikilizaji wa mashauri ili kuongeza kasi ya utoaji haki nchini kwa wananchi.

Hafla maalum ya uzinduzi wa vituo hivyo imefanyika katika jengo mojawapo lililojengwa Jijini Dodoma, Mtaa wa NCC. Uzinduzi wa Kituo hicho umewakilisha vituo vingine vitano (5) ambavyo vimejengwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam yenye majengo mawili (Kanda ya Temeke na Kanda ya Kinondoni).

Katika vituo hivyo, kutakuwepo na huduma za utoaji haki kwa ngazi zote za Mahakama, yaani Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu, ambapo kwa baadhi ya majengo kutakuwepo pia sehemu iliyotengwa kwa ajili ya Mahakama ya Rufani. Vituo hivyo pia vinajumuisha huduma za wadau wengine katika mnyororo wa utoaji haki, kama Mkurugenzi wa Mashitaka, Wakili Mkuu, Magereza, Polisi, Ustawi wa Jamii na Mawakili wa Kujitegemea.

Akizungumza katika sherehe ya ufunguzi wa vituo hivyo, Mhe. Rais Samia alitoa wito kwa wadau wote wa mfumo wa utoaji haki kutimiza wajibu wao ipasavyo, ikiwemo kutochelewesha usikilizaji wa mashauri ili haki ipatikane kwa wananchi kwa wakati.

 “Natoa rai kwa Mahakama kushughulikia suala hili la ucheleweshaji  wa mashauri. Mkiamua inawezekana kufanyika hivyo. Nawasihi sana mlipe kipaumbele inavyostahiki ili haki iweze kutendeka kwa wakati. Msikubali kirahisi kubadilisha badilisha tarehe ya kusikiliza mashauri pasipokuwa na sababu za msingi, kwa kuwa hii ni moja ya sababu inayochelewesha,” amesisitiza.

Mhe. Rais ameeleza kuwa mfumo wa Tehama unaotumika hivi sasa Mahakamani unampa Jaji Kiongozi  kujua mashauri yapi yaliyosajiliwa yamekaa kwa muda gani bila kusikilizwa, naye kwa haraka humuuliza Jaji anayehusika kujua sababu iliyopelekea mashauri hayo kukwama. Alisema kuwa ufuatiliaji wa aina hiyo utasaidia wadau wengine kama Wapelelezi, Mawakili, Polisi na Magereza wanaochangia ucheleweshaji huo kuwajibika ipasavyo ili haki ipatikane kwa wakati.

Sambamba na ombi hilo, Mhe. Rais alieleza kuwa pamoja na ujenzi wa miundombinu ya Mahakama, ikiwemo vituo hivyo jumuishi vya utoaji wa haki, kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu, kuanzisha mahakama zinazotembea na kuimarisha matumizi ya Tehama, mafanikio yanayotarajiwa hayatapatikana, iwapo wasimamizi na wadau katika mfumo wa utoaji haki nchini hawatafanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, taratibu na pia kuongozwa  na nafsi katika kufanya kazi.

“Hii ina maana kwamba tunaweza kuwa na majengo mazuri sana yenye kila huduma, mfumo mzuri wa Tehama na kila kitu tunachokihitaji. Kama watendaji, Mahakimu na Majaji na wengine wanaowasaidia hawataongozwa na nafsi njema katika utoaji haki, bado haki inaweza isipatikane. Kwa hiyo, jambo kubwa hapa ni utashi wa nafsi zetu kutumika na kutoa haki kwa wananchi. Niwaombe watendaji, Mahakimu na Majaji kuwa na moyo huo,” amesema.

Rais Samia aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuiwezesha Mahakama ya Tanzania katika kutekeleza majukumu yake, iwe kwenye bajeti kutoka serikalini au kuzungumza na wadau ili kupata mikopo au misaada ili shughuli za Mahakama ziweze kufanyika kwa ufanisi,ikiwemo kuendelea na maboresho ya miundombinu mbalimbali. “Nafahamu kuwa ujenzi wa Makao Makuu bado haujakamilika.Tutawawezesha kukamilisha mradi huo ili ikiwezekana ukamilike kabla ya muda uliopangwa ambao ni Desemba 2022,” alisema.

Mhe. Rais pia aliahidi kuongeza watumishi wa Mahakama na kuboresha mazingira ya kazi kadri fursa zitakapopatikana ili haki ipatikane kwa wakati. Rais Samia aliipongeza Mahakama kwa kuimarisha matumizi ya Tehema ikiwemo kuanza kusajili na kusikiliza mashauri kwa njia ya mtandao, hatua ambayo ameielezea kama mapinduzi makubwa ambayo sio tu yamesaidia kuharakisha uendeshaji wa mashauri  na utoaji wa maamuzi, bali pia kuthibiti vitendo vya rushwa mahakamani.

“Natambua kuwa mnakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa njia ya mawasiliano ya kimtandao (bandwith) kutokana na gharama kuwa juu. Hivi sasa mna ‘bandwith’ yenye thamani ya millioni 100 kutoka kwenye mkongo wa Taifa wakati mahitaji yenu ni ‘bandwith’ yenye thamani ya million 400. Hivyo, naelekeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama kukutana na viongozi wa Wizara ya Mawasiliano  na Wizara ya Fedha ili kushughulikia swala hili,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi alieleza kuwa uzinduzi wa vituo hivyo unafanyika wakati Taifa linajiandaa kusherekea miaka 60 ya Uhuru, ambapo Tanzania imepiga hatua kubwa sana za maendeleo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo Mahakama.

“Leo tunasherekea miaka 60 ya Uhuru wetu tukiwa na Mahakama za kisasa na Mahakama bora ambazo sio tu bora Tanzania bali ni mfano wa kuigwa katika Bara la Afrika. Nchi hii ya Tanzania iliyokuwa nyuma kuliko zote wakati tunapata uhuru katika Afrika Mashariki na Kati, leo ni kiongozi, leo ni kinara, leo ni mfano wa kuigwa. Tunakupongeza sana Mhe. Rais kwa mafanikio haya,” alisema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa tatu kushoto) akifungua kitambaa kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma, pamoja naye ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. Wanaoshuhudia, wa kwanza kushoto ni Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania, wa pili kushoto ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, wa pili kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu n awa kwanza kulia ni Mhe. Jaji John Mgetta, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Uzinduzi wa Kituo hicho umewakilisha vituo vingine ambavyo vimejengwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Morogoro na Dar es Salaam yenye majengo mawili (Kanda ya Temeke na Kanda ya Kinondoni).

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki-Dodoma. Wa tatu kulia ni Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Tanzania, wa pili kulia ni Mhe. Job Ndugai, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  wa kwanza kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu, wa tatu kushoto ni Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Katiba na  Sheria, wa kwanza kushoto ni Mhe. Antony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na wa pili kushoto ni Mhe. Mustapher Siyani, Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma (IJC-Dodoma)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan (katikati) akipata maelezo ya jengo la 'IJC' Dodoma kutoka kwa Mhe. Zahra Maruma, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania (wa kwanza kulia) na Prof. Elisante Ole Gabriel, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania (kushoto). Wanaosikiliza ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kulia) na baadhi ya Viongozi wengine walioambatana na Mhe. Rais wakati akikagua jengo hilo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni